Stori: Makongoro Oging’BADO
tupo mwanzoni mwa mwaka lakini tukio la maiti ya kichanga kugeuka jogoo
ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Mwananyamala,
jijini Dar es Salaam linaweza kuongoza mengine yote ya ajabu yanayoweza
kujiri ndani ya 2013.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela.
Mwananyama ni hospitali yenye hadhi ya mkoa kitabibu, ina rekodi za
kuwa na matukio ya ajabu, ila hili siyo tu kwamba linaingia miongoni mwa
hayo bali pia linaweza kutia fora.
Asubuhi ya Jumatano iliyopita,
ilikuwa kizaazaa pale jokofu lililotumika kuhifadhi maiti ya kichanga
cha mtoto, kukutwa kuna jogoo.
Mshangao zaidi ni kwamba ndani ya lile jokofu, pembeni ya yule jogoo, kulikuwa na hirizi pamoja na tunguri.
TUKIO LILIKUWA HIVIHabari kutoka vyanzo vyetu,
zimewekwa wazi kuwa Jumanne iliyopita, saa 7 mchana, polisi walipigiwa
simu, wakataarifiwa kuhusu maiti ya mtoto iliyokuwa imetelekezwa eneo la
Kigogo, Mbuyuni, Dar es Salaam.
Vyanzo vyetu vimebainisha kuwa
polisi baada ya kupata taarifa hizo walifika eneo la tukio na kukuta
maiti hiyo ya kichanga ikiwa imefunikwa kwa kuzungushiwa sanda.
ETI, KILIKUWA KICHANGA CHA KIKEKwa mujibu wa
Moses Madilu, mkazi wa Kigogo, aliyedai kushuhudia tukio hilo, polisi
walipofika eneo la tukio waliikagua maiti hiyo na kubaini kwamba ni ya
kike.
Chanzo chetu kikaeleza kuwa baadhi ya mashuhuda, hususan
wanawake, walitokwa na machozi kwa masikitiko kwamba itakuwa mtu
alijifungua halafu akakinyonga kichanga hicho kabla ya kukitelekeza eneo
hilo.
“Baada ya kujiridhisha kwa kazi yao, polisi waliichukua maiti
hiyo ya kichanga, wakaipakia kwenye ‘difenda’, wakaipeleka Hospitali ya
Mwananyamala,” kilieleza chanzo chetu.
HOSPITALI YA MWANANYAMALANdani ya hospitali
hiyo, mwandishi wetu alielezwa kuwa polisi walipofika, walishusha maiti
hiyo na kumkabidhi mganga wa zamu aliyejulikana kwa jina moja la Dk.
Liwa.
Muuguzi mmoja wa hospitali hiyo (jina tunalo) alisema: “Dk. Liwa aliwaambia wale polisi wapeleke maiti hiyo mochwari.
“Polisi
walifanya hivyo lakini kule mochwari walimkuta msimamizi mkuu, Omar
Buyoya aliyekataa kuipokea kwa vile daktari hakuthibitisha kama kile
kichanga kilikufa au kilikuwa hai.
“Polisi na Buyoya walivutana kwa
muda mrefu, alitokea mhudumu mwingine wa mochwari aliyekuwa akijuana na
polisi mmoja aliyebeba ile maiti, alikubali kuupokea mwili huo na
kuingiza ndani kwenye jokofu la kuhifadhia maiti.”
Muuguzi huyo
aliendelea kusema kuwa siku iliyofuata, Dk. Liwa alifika mochwari na
alipofungua jokofu na kufunua sanda, badala ya kukuta maiti ya kichanga,
alikuta jogoo, tunguri na hirizi.
“Dk.Liwa alipatwa na mshangao
mkubwa huku jasho likimtoka kutokana na uoga, aliwaita wafanyakazi ambao
walijazana hapo mochwari kushuhudia.
“Baadhi ya wafanyakazi
walipigwa na butwaa huku wengine wakicheka hadi kudondoka chini na
wakawa wanajiuliza kama kweli polisi wanaweza kupeleka jogoo hospitali
au ni mambo ya kishirikina,” alisema muuguzi huyo.
Dk. Liwa na wafanyakazi wenzake waliondoka mochwari na kuacha hilo jogoo katika chumba cha maiti huku wakishindwa la kufanya.
MGANGA MKUU ANENAGazeti hili lilimtafuta Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Sophinias Ngonyani ambaye
alikiri kuonekana kwa jogoo badala ya maiti ya kichanga.
“Polisi
walituletea kifurushi wakiamini kuwa ni maiti ya kitoto kichanga ambapo
tulikipokea lakini ilipotazamwa na daktari, tulikuta jogoo, hirizi na
tunguri, tuliamua kumchoma moto kwa sababu kile ni chumba cha kuhifadhi
maiti siyo cha kuhifadhia mizoga ya kuku, ng’ombe au mbwa,” alisema Dk.
Ngonyani.
POLISI WANENANaye Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa
Kinondoni, ACP Charles Kenyela alipoulizwa juu ya sakata hilo alisema
kwamba wao kama jeshi la polisi walipigiwa simu na raia mwema kuwa kuna
maiti ya kichanga ambapo askari waliondoka hadi eneo la tukio na
kuichukua mpaka Hospitali ya Mwananyamala.
“Polisi waliichukua hadi
Hospitali ya Mwananyamala kwa wataalamu na baada ya kuikabidhi
waliondoka na kuendelea na shughuli nyingine, nami nashangaa kusikia
kwamba madaktari walikuta bonge la jogoo,” alisema Kenyela.
MASWALI MATANOJe, ni kweli polisi waliikagua maiti na kugundua ni kichanga cha kike?
Kama ndiyo, ilikuwaje kikageuka jogoo?
Kwa nini daktari hakuipima ile maiti, badala yake akaelekeza ipelekwe mochwari?
Je, au polisi walibeba mzoga wa jogoo, wakampakia kwenye difenda wakidhani ni maiti ya kichanga?
Mkweli nani, polisi wanaodai kupeleka maiti ya kichanga, au hospitali wanaosema walipelekewa mzoga wa kuku, tunguri na hirizi?