Akina mama wakilia baada ya kifo cha ghafla cha Padri Evarist Mushi
kilichotokea jana asubuhi kwa kupigwa risasi muda mfupi kabla ya kuanza
misa ya Jumapili kwenye Kanisa Katoliki la Kigango cha Mtoni,
PADRI wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili lililoko Mji
Mkongwe Zanzibar, Evaristus Mushi ameuawa kwa kupigwa risasi na watu
wasiojulikana jana asubuhi wakati akielekea kanisani kuendesha ibada.
Tukio hilo limetokea majira ya saa moja asubuhi
wakati padri huyo akijitayarisha kwenda kuongoza ibada ya Jumapili
katika Kanisa la Mtoni nje kidogo na Mji wa Zanzibar.
Hilo ni tukio la pili kutokea kwa padri kupigwa
risasi Zanzibar baada ya Desemba 26, mwaka jana Padri Ambros Mkenda wa
Kanisa Katoliki, Mjini Zanzibar kupigwa risasi na watu wasiojulikana nje
ya nyumba yake saa 1:45 jioni wakati akitokea kanisani.
Akizungumzia tukio la jana, Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini (IGP), Said Mwema pamoja na kuthibitisha, alisema ametuma
timu ya wapelelezi kwenda Zanzibar kuchunguza kwa undani kuhusu tukio
hilo.
“Watu wasiojulikana wamempiga risasi Padri Mushi,
na baada ya tukio alipelekwa Hospitali ya Mnazi Mmoja na kufariki dunia.
Polisi inaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo,” alisema IGP Mwema.
Alisema hadi sasa watu watatu wameshakamatwa kuhusiana na tukio hilo na msako mkali unaendelea na kuchunguza tukio zima.
IGP Mwema alisema ametuma timu Zanzibar
itakayoongozwa na Manaibu Kamishna wa Polisi wawili ambao ni Samson
Kasalla na Peter Kivuyo wakiwa pamoja na Kamanda wa Operesheni wa jeshi
hilo, Simon Sirro.
“Tumekuwa tukifuatilia nyendo hizi na hivi sasa
tutapambana na wahalifu ipasavyo, vurugu zozote zile lazima tupambane
nazo ipasavyo,” alisema Mwema na kuongeza: “Kama kwenye tukio hili
kutakuwa na masuala ya kigaidi nayo tutachunguza.”
Alisema watawatafuta kwa udi na uvumba wale wote wanaochochea au kufadhili yanayotokea kwa kuwa wanachokifanya ni uhalifu.
Mwili wa padri huyo sasa umehifadhiwa katika mochwari ya Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Katika
Kanisa la Minara Miwili, Mji Mkongwe waumini walikusanyika wakionyesha
hali ya kuchanganyikiwa baada ya kupata taarifa za kifo hicho cha
ghafla.
Wakizungumza kwa masikitiko waumini hao wamesema hawakuwa
wakijua chochote kilichotokea hadi hapo walipofika katika kanisa kwa
ajili ya kufanya ibada.
“Tumetoka nyumbani tukiwa na matumaini
makubwa ya kufanya ibada zetu kwa amani, lakini tulipofika hapa
tumepokea taarifa kuwa padri wetu amepigwa risasi, jamani Mungu hiki ni
nini, mbona Zanzibar imegeuka kuwa nchi isiyo na amani, vipi tutaishi
katika hali kama hii ya kuhofu na wasiwasi...Mungu tusaidie waja wako
sisi,” alisema mama mmoja huku akilia kwa majonzi.”
Mashuhuda
Walioshuhudia
tukio hilo wanasema kawaida Padri Mushi huwa anakwenda kusalisha katika
Kanisa la Mtoni na kwamba jana, baada ya kufika kanisani hapo wakati
akitaka kuegesha gari lake walifika watu kwenye gari lake na kumfyatulia
risasi na kisha kukimbia kusikojulikana.
Makamu Askofu wa kanisa
hilo Zanzibar, John Mfoi alisema kuwa watu waliompiga risasi Padri Mushi
walikuwa wapo kwenye pikipiki aina ya Vespa na walikuwa wakimfuatilia
kwa nyuma wakati akieleke kanisani.
“Baada ya kufika karibu na kanisa
alipigwa risasi na gari kupoteza mwelekeo kisha kwenda kuonga
nyumba,”alisema na kuongeza: “Uchunguzi wa hospitali umegundua alipigwa
risasi tatu mbili zimetolewa kichwani na nyingine haijulikani iliko.”
Matukio
kama hayo ya kihalifu yamekuwa yakitokea mara kwa mara Zanzibar ambapo
katika kipindi cha mwezi mmoja watu watatu walipigwa risasi maeneo ya
Bububu na Mbweni, lakini hii ni mara ya pili kwa padri kupigwa risasi
katika historia ya Zanzibar.
TEC wasikitika
Makamu wa Rais wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),Severin Niwemugizi alisema
tukio hilo linatia mashaka kwa kuwa mauaji hayo yanaonyesha kuwa ni ya
kupanga.
“Nimepata taarifa kwamba kuna mwenzetu ameuawa huko, lakini
inaonekana ni mauaji ya kupangwa kwa kadiri ya hamasa ambazo zinatolewa
na dini fulani, kwani waliwahi kusema hatutaifurahia Pasaka, nadhani
ndiyo wanatekeleza hilo,” alisema Niwemugizi.
Alisema tukio hilo ni la kuogopesha na linaonyesha
nchi inakoelekea si kuzuri kwa kuwa kikundi fulani kimeachiwa na
kinafanya mauaji na kuwatendea maovu wengine lakini viongozi wamekaa
kimya.
“Hii ni ishara mbaya kwani Serikali ipo hivyo
tunahitaji kauli yao kuhusu haya mambo, kwa kweli nina mashaka na
yanayotokea ili yasije yakatufikisha kwenye mauaji ya kimbari
yaliyotokea Rwanda,”alisema Niwemugizi.
JK atuma rambirambi
Rais Jakaya Kikwete alisema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa kwa Padri Mushi.
“Nimeligiza Jeshi la Polisi nchini kukusanya nguvu
zake zote na maarifa yake yote kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina na wa
haraka sana unafanyika ili kubaini mhusika ama wahusika na kuwakamata
ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.”
Alisema pia ameagiza polisi washirikiane na vyombo vingine vya
usalama nchini na mashirika ya upepelezi ya nchi rafiki katika kufanya
uchunguzi wa mauaji hayo.
Amesisitiza Rais Kikwete: “Nataka ukweli
wake ujulikane ili kama kuna jambo lolote zaidi liweze kushughulikiwa na
kukata mzizi wa fitina.”
Dk Nchimbi asema ni ugaidi
Waziri
wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi alisema kuwa mauaji hayo ni ya
kigaidi hivyo Serikali itachukua hatua kali kuhakikisha waliohusika
wanakamatwa.
“Tutahakikisha kuwa Serikali inawakamata waliohusika na kuwatia mbaroni,”alisema Dk Nchimbi.
Mwinyi aonya
Rais mstaafu, Ali
Hassan Mwinyi amewaonya viongozi wa dini kuhusiana na matukio ya vurugu
yanayoendelea kujitokeza nchini akisema kuwa Tanzania ni sawa na gunia
lililokusanya mchanyanyiko wa watu wenye kufuata mikondo ya dini
inayotofautiana. Hivyo hakuna dini inayoweza kujigamba ni bora zaidi ya
nyingine.
Aliwataka viongozi wa dini kuwakemea waumini
wanaojihusisha na mienendo korofi kwa kuwa bila kufanya hivyo taifa
linaweza kutumbukia kwenye mgogoro wa kidini na kusababisha upotevu wa
hali ya amani na mshikamano.
Rais mstaafu Mwinyi ambaye alikuwa akizungumza
kwenye sherehe za Maulidi iliyoadhimishwa jana na waumini wa Madhehebu
ya Shia, alisema kuwa Tanzania iko kwenye wakati mgumu ikiandamwa na
misukosuko ya aina mbalimbali ikiwemo ile yenye sura za kidini na
kisiasa.
Alisema kuwa Tanzania iliyosifikia duniani kwa ustaarabu
wake wa amani na mshikamano sasa inaanza kupoteza mwelekeo kwa raia wake
kuingia kwenye maisha ya hofu na kushindwa kuaminiana.
“Ngoja niwapeni mfano mmoja hata kama mfano huu
utakuwa mbaya kwenu, lakini nataka muelewe maana yangu… Tanzania ni sawa
na gunia lililokusanya watu wa aina mbalimbali, wapo wale wenye dini,
kuna wale hawana dini na wapo ambao wana dini inayotofautiana na dini
nyingine...Hakuna upande unaoweza kujivuna kuwa ni bora kushinda
mwenzake,” alisema na kuongeza;
“Ni wajibu wote tuliomo ndani ya gunia hili
kushikamana na kuvumiliana kwani tukisema huyu ni bora zaidi ya
mwingine, hatutafika mbali.”
Alisema kuwa Watanzania wanapawa kujenga tabia ya
kuvumiliana na kutatua tofauti zao kwa njia ya majadiliano bila
kujiingiza katika matukio yanayoweza kuharibu amani ya nchi.
“Waswahili
walisema, maneno matamu humtoa nyoka pangoni. Hivyo nawatamanieni
viongozi wa dini kazaneni kuwahimiza waumini wenu kutojihusisha na
mienendo hatarishi kwa amani yetu,” alieleza Mwinyi, ambaye alioongoza
Tanzania kuanzia mwaka 1985 hadi 1995.
Sheikh DSM aonya
Akizungumzia
tukio la mauaji ya padri huyo, Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Alhaji
Mussa Salum pamoja na kulitaka Jeshi la Polisi kuharakisha uchunguzi wa
tukio hilo.
Alisema kuwa hali ya hewa visiwani humo imechafuka na kuonyesha wasiwasi wake kuhusiana na kujitokeza kwa matukio hayo.
Alisema kuna haja kwa mamlaka kutafakari kwa
makini na kujiuliza kwa nini matukio hayo yanajitokeza wakati huu ambapo
baadhi ya viongozi wa dini wameendelea kushikiliwa kizuizini.
“Kwangu
mimi haya ya Zanzibar yanajadilika, pia lazima tujiulize kwa nini
matukio haya ya mashambulizi yanajitokeza zaidi wakati huu,” alisema.
Lowassa: Waislamu, Wakristo waunganeWaziri
Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amewataka Waislamu na Wakristo wote
nchini kuungana kwa pamoja kuitetea na kuilinda amani iliyopo kwa
vitendo.
Akizungumza katika Harambee ya Kanisa la Moravian Kanda ya
Magharibi iliyofanyika katika Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, Lowassa
alisema kuwa waumini hao kwa pamoja wanapaswa kuungana na kuwa kitu
kimoja katika kuitetea amani iliyopo kwa vitendo.
Aliendelea
kusisitiza kwamba kwa sasa kuna baadhi ya Watanzania wanaichezea amani
iliyopo kwa sasa hapa nchini na kufanya mauaji ya watumishi wa Mungu.
“Hii ni Tanzania tunayoitaka kwa Waislamu na Wakristo kushirikiana katika ibada kama hii leo hapa kanisani,” alisema Lowassa.
Lowassa aliendelea kusisitiza kwamba Watanzania
wanapaswa kuhakikisha kila siku wanamuomba Mungu, ili kuendeleza amani
hapa nchini inadumishwa kwa hali na mali.
Alisema kwamba watu wanaomsema vibaya kila kukicha
waendelea kufanya hivyo, kwani kwa kufanya hivyo wanaendelea
kumuimarisha kiimani na nguvu kubwa ya ushawishi kwa watu wa Mungu ambao
ndiyo wamekuwa wakimuunga mkono kila siku katika kazi ya Mungu.
Alirudia kauli yake aliyoitoa mkoani Mbeya hivi
karibuni, “Mimi ni tajiri wa watu na siyo tajiri wa fedha kama
wanavyosema huko mitaani na watu wasiokuwa na mapenzi mema na
Mungu,”alisema Lowassa.
Katika harambee walikuwapo baadhi ya Waislamu
kutoka Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora pamoja na viongozi
mbalimbali wa siasa kutoka sehemu mbalimbli hapa nchini.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian Kanda ya
Magharibi, Issack Nicodemo alisema kuwa Waislamu na Wakristo hapa nchini
ni ndugu kutokana na uhusiano uliopo tangu zamani.
Alisema kuwa vitendo vinavyoendelea kufanyika hapa nchini vya mauaji kwa viongozi wa dini ni vya kulaaniwa.