Wananchi wamekumbwa na wasiwasi
kwani Mandela amekuwa akitibiwa ugonjwa wa mapafu
Rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson
Mandela, yuko hospitalini kwa siku ya tatu kwa matibabu ya ugonjwa. Hadi sasa
hakuna taarifa zozote kuhusu muda ataokuwa hospitalini.
Siku ya Ijumaa Mandela aliripotiwa
kuendelea vyema na matibabu yake lakini hakuna taarifa mpya kuhusu hali yake.
Hapo jana maafisa wa utawala nchini Afrika Kusini walisema kuwa Mandela alikuwa
anaendelea vyema na matibabu baada ya kulazwa hospitalini kwa siku ya pili
akiwa na maradhi ya kifua.
Taarifa kutoka rais wa nchi hiyo Jacob Zuma zilisema kuwa hali ya Mandela
inaendelea kuimarika na kwamba hata aliweza kula vyema kiamsha kinywa chake.
Mapema leo Jacob Zuma, aliwahakikishia wananchi wa Afrika Kusini kuwa rais
mstaafu Nelson Mandela anatibiwa ugonjwa wa mapafu ambao umekuwa ukitokea mara
kwa mara.
Katika mahojiano na BBC , bwana Zuma alisema kuwa watu hawapaswi kuwa na
wasiwasi kwani Mandela anaendelea kupokea matibabu.
Mandela mwenye umri wa miaka 94 alilazwa hospitalini kabla ya Jumatano usiku.
Alikuwa hospitalini kwa siku 18 mnamo mwezi Disemba, akipokea matibabu ya
mapafu na kibofu.
Katika taarifa yake iliyotolewa mapema, Zuma alisema kuwa Mandela anaendelea
kupokea matibabu.
Rais Zuma hata hivyo hajaelezea alikolazwa Mandela.
Miaka
muhimu katika maisha ya Mandela
- 1918 Alizaliwa mkoa wa Eastern Cape
- 1943 Ndipo alijiunga na chama cha African National
Congress
- 1956 Alishtakiwa kwa kosa la uhaini , ingawa mahakama
ilitupilia mbali mashtaka hayo
- 1962 Alikamatwa na kushtakiwa kwa kosa la hujuma na
kufungwa jela kwa miaka mitano.
- 1964 Alishtakiwa tena na kufungwa maisha jela
- 1990 Aliachiliwa huru kutoka jela
- 1993 Ashinda tuzo ya amani ya Nobel
- 1994 Alichaguliwa rais wa kwanza mwafrika mweusi nchini
Afrika Kusini
- 1999 Aling'atuka mamlakani kama kiongozi kwa hiari
- 2004 Astaafu
- 2005 Atangaza kuwa mwanawe alifariki kutokana na
maradhi ya ukimwi
Akiongea na mwandishi wa BBC Lerato
Mbele, bwana Zuma alisema kuwa watu wanapaswa kuwa watulivu.
"ndio, nimekuwa nikiwambia watu kukubali kuwa Mandela sio kijana tena na
ikiwa atakwenda hospitalini mwara kwa mara kwa ukaguzi wa kiafya, sidhani hilo
linapaswa kuwaweka watu wasiwasi. Ningependa kusema kuwa watu hawapaswi kuwa na
wasiwasi hata kidogo,'' alisema Zuma
Mandela anasifika na kujulikana kama Madiba jina la utani.
Alipohojiwa kuhusu ikiwa watu wa Afrika Kusini wajiandae kwa lolote , Zuma
alijibu kusema kuwa ''ikiwa mzee anafariki, watu husema kuwa ameenda
nyumbani.Nadhani hayo ndio baadhi ya mambo ambayo tunapaswa kutafakari.''
Lakini alisisitiza kuwa bwana Mandela ameweza kupokea matibabu vyema.
Bwana Mandela anatazamiwa na wengi kama baba wa taifa kwa kupambana dhidi ya
enzi ya ubaguzi wa rangi.
Mandela alifungwa jela miaka 27
lakini aliachiliwa baada ya kuhudumu miaka 18
Ni mara ya nne kwa Mandela kulazwa
hospitalini katika muda wa miaka miwili.
Aliugua kifua kikuu mapema miaka ya themanini, alipofungwa jela katika kisiwa
cha Robben Island, kwa miaka 18.
Mapafu yake inaarifiwa yaliathirika pakubwa kwa sababu ya kufanya kazi katika
machimbo ya mawe alipokuwa anahudumia kifungo chake.
Licha ya kufungwa kwa miaka mingi ,Mandela aliwasamehe maadui wake wa zamani
alipokuwa rais na kuwataka wanachi wote wa Afrika kusini licha ya rangi yao,
kusameheana.