Mkurugenzi wa Habari na Uenezi (CHADEMA), John Mnyika (Mb).
KATIKA mitandao ya kijamii kumesambazwa habari zikimnukuu msemaji wa
CCM kutoa madai mbalimbali ya uzushi katika mkutano na waandishi wa
habari kuhusu CHADEMA baada ya CHADEMA kuendelea kutekeleza mikakati na
mipango yake ya kuwaunganisha watanzania kupitia falsafa ya ‘nguvu ya
umma’ katika kuchangia vuguvugu la mabadiliko (M4C) katika maeneo
mbalimbali nchini. Nitatoa tamko kamili na kueleza hatua za ziada baada
ya kupata taarifa iliyotolewa kwa ukamilifu, hata hivyo kuhusu madai
yaliyokwisha sambazwa kwenye mitandao ya kijamii na CCM nachukua fursa
hii kutoa kauli ya awali kama ifuatavyo:
Kuibuka huku kwa CCM na
kufanya propaganda chafu ni ishara ya kwamba CCM inaumizwa na namna
ambavyo watanzania wanajitokeza kuunga mkono CHADEMA kwa hali na mali
hivyo CCM sasa inatapatapa kujaribu kudhibiti wimbi la mabadiliko kwa
kutumia siasa chafu. Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete anapaswa
kueleza watanzania iwapo mikakati hiyo michafu ina baraka zake na za
serikali anayoiongoza kwa kurejea pia madai yaliyotolewa na Waziri wa
Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Steven Wassira kuwa CHADEMA
itasambaratishwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa mbinu mbalimbali.
CCM kwa kuwa imekuwa na kawaida ya kufanya usanii kuhalalisha fedha
haramu kama ilivyofanya kwenye chaguzi zilizopita baada ya viongozi
waandamizi wa CCM na makada wake kuchota fedha za chafu kifisadi kama
zile za kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na vyanzo vingine
vichafu na kuzisafisha kupitia harambee za hadaa zilizofanywa na CCM
kwa nyakati mbalimbali; inataka kuichafua CHADEMA inayopata fedha
kutoka vyanzo halali kwa njia za wazi ili kukatisha tamaa umma wa
watanzania unaochangia vuguvugu la mabadiliko.
Viongozi wa
CCM wameamua kujidanganya, kuidanganya Serikali yao na kujaribu
kuwapotosha watanzania lakini CHADEMA inatambua kwamba watu wachache
wanaweza kudanganyika kwa muda mchache lakini si watu wote wakati wote;
na kwamba watanzania wa leo kwa uwingi wao hawawezi kudanganyika na
uzushi wa kijinga wa CCM.
Ni ukweli ulio wazi kwamba CHADEMA
imekuwa ikifanya harambee kwa uwazi kwa nyakati mbalimbali katika kumbi
na katika mikutano ya hadhara ikiwemo ya vijijini ambapo michango
hutolewa kwa uwazi, aidha michango kwa njia ya simu inaweza kufuatiliwa
na kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba watanzania wameamua kuchangia
mabadiliko ya kweli.
Madai ya CCM kuwa CHADEMA imepokea au
itapokea mabilioni ya shilingi kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi na
narudia kwa mara nyingine tena kuitaka CCM itaje majina ya serikali,
taasisi ama makampuni ya nje ambayo CCM inadai kwamba CHADEMA imepokea
mabilioni ya shilingi katika siku za karibuni au inatarajia kupokea.
Badala ya CCM kuisingizia CHADEMA ilipaswa CCM ieleze watanzania orodha
ya vigogo wa Serikali inayoongozwa na wanachama waandamizi wa CCM ambao
wanaelezwa kuwa na akaunti nchini Uswisi na nchi zingine wakituhumiwa
kupewa fedha za kifisadi kutoka kwa makampuni ya utafutaji wa mafuta,
gesi asili pamoja na uchimbaji wa madini.
CCM ilipaswa ieleze
watanzania sababu za kuendelea kusuasua kujivua magamba ya ufisadi
kinyume na maazimio ya CCM yaliyofikiwa baada ya msukumo wa CHADEMA
kutaja orodha ya mafisadi kwa kuwa kati ya mafisadi hao ni pamoja na
viongozi wa CCM walioiingiza nchi katika mikataba mibovu.
Ikumbukwe kwamba madai haya si mapya kutolewa na CCM, yaliwahi kutolewa
na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Sophia Simba mara baada
ya uchaguzi mkuu wa 2010 akidai kuwa CHADEMA imepokea fedha kutoka
mataifa ya ulaya kwa ajili ya kufanya maandamano ya kuiondoa CCM
madarakani.
Itakumbukwa kwamba wakati huo nilimtaka ataje nchi
hizo na kueleza kusudio la kumchukulia hatua zaidi na kwa upande
mwingine niliyataka mataifa hayo ya Ulaya yatoe kauli kuhusu madai
hayo. Izingatiwe kwamba mataifa hayo yalikanusha madai hayo ya CCM na
Sophia Simba mwenyewe alikana kuwa hakuna madai hayo dhidi ya CHADEMA.
Nimeelezwa kuwa CCM imetoa madai mengine ya uzushi kuwa CHADEMA inapewa
mabilioni toka nje kwa kuwa nchi imegundua rasilimali za mafuta na gesi
na kudai kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiweka nchi rehani.
Madai haya yaliwahi kutolewa pia na Katibu wa CCM wa Fedha na Uchumi
Mwigulu Nchemba na nikamtaka Waziri wa Mambo ya Nje Benard Membe kutaja
nchi hizo na mikataba hiyo hata hivyo mpaka sasa hakuna kiongozi yoyote
wa CCM na Serikali aliyejitokeza kutaja CHADEMA imepokea au itapokea
mabilioni kutoka nchi gani na kwa mikataba gani.
CCM inatoa
madai hayo kuhamisha mjadala baada ya CHADEMA wa uongozi bora, sera
makini, mikakati sahihi na oganizesheni thabiti kuwa mstari wa mbele
katika kutetea rasilimali za taifa na watanzania kutambua kwamba taifa
letu litaepushwa kutumbukia kwenye laana ya rasilimali kwa kuiondoa CCM
madarakani katika chaguzi za mwaka 2014 na 2015 na kuichagua CHADEMA.
CCM na Serikali yake ndiyo imekuwa kinara wa kupokea fedha kutoka nje
kwa kisingizio cha misaada na kuingia mikataba mibovu na mataifa ya nje
pamoja na makampuni ya kigeni na kuachia mianya ya uporaji wa
rasilimali za nchi na CHADEMA imeanika hali hii kwenye orodha ya
mafisadi kwa kutaja majina ya viongozi waliohusika kwenye mikataba ya
madini na tutaendelea kufanya hivyo hata katika masuala ya mafuta na
gesi ambayo tayari vigogo wa Serikali inayoongozwa na CCM wameshaanza
kuingia mikataba mibovu na kuingiziwa fedha katika akaunti zao za nje
ya nchi.
Hivyo, badala ya CCM kutoa madai ya uzushi kuhusu
CHADEMA kuingia mikataba na serikali au makampuni ya nje, CCM ieleze
watanzania imechukua hatua gani mpaka sasa juu ya viongozi na wanachama
wake waliongia mikataba mibovu kwenye rasilimali muhimu nchini ikiwemo
madini, mafuta, gesi na maliasili zingine za taifa letu na kutoa
mikataba hiyo hadharani ili watanzania waweze kuchukua hatua za kufanya
mabadiliko ya kweli.
Hivi karibuni Rais Kikwete ambaye pia ni
mwenyekiti wa CCM alisema kwamba serikali inayoongozwa na CCM
haitarudia makosa ya kuachia mianya ya ufisadi kwenye gesi; hivyo CCM
ilipaswa wakati huu kuwaomba radhi watanzania kwa ufisadi uliofanyika
kwenye madini na rasilimali nyingine na kuishukuru CHADEMA kwa
kuendelea kuwaunganisha watanzania wakati wote kusimamia mabadiliko ya
kweli.
CCM badala ya kutishia kuwa ina mikataba inayoihusu
CHADEMA ingetoa mikataba hiyo na hali hii ya CCM inayoongoza Serikali
kudai CHADEMA kufanya mikakati, mipango na shughuli iliyo kinyume cha
sheria bila vyombo vya dola kuchukua hatua ni ishara ya CCM kukiri wazi
kuwa chama legelege chenye serikali legelege kimeshindwa kuongoza nchi
na badala yake kimejikita katika propaganda chafu.
CHADEMA
tangu kuanzishwa kwake imekuwa na makubaliano ya ushirikiano (MOU) bila
masharti yoyote na vyama rafiki vya ndani ya Afrika na duniani na
makubaliano hayo yamekuwa yakifikiwa kwa uwazi ikiwa ni sehemu ya
CHADEMA kuwa na mtandao wa kimataifa na hayajawahi kuhusisha wala
hayatawahi kuhusisha CHADEMA kusaidiwa mabilioni ya shilingi kwa ajili
ya kufanya kazi zake kama inavyodaiwa na CCM.
CHADEMA
kimekuwa chama kiongozi kwa nyakati mbalimbali kueleza viwango cha
matumizi yake ya fedha na vyanzo vya fedha husika huku kikitegemea kwa
kiwango kikubwa michango ya wanachama na wapenzi wa chama hapa nchini
pamoja na kutumia kwa ufanisi ruzuku inayotolewa kwa vyama vya siasa.
CCM imekuwa na kawaida ya kutoa madai ya uzushi wakati mwingine
yakiambatana na kutoa nyaraka za kughushi inazodai kuwa ni za CHADEMA.
Ikumbukwe kwamba wakati wa uchaguzi wa mdogo wa Igunga, CCM ilitoa
madai ya uzushi kuwa CHADEMA inafadhiliwa na nchi za nje ikiwemo kupewa
mafunzo ya ugaidi na kudai kuwa tayari magaidi wameingizwa na CHADEMA
toka nje katika uchaguzi huo; hata hivyo katika mwenendo wa kesi ya
uchaguzi ya Igunga Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama aliyetoa madai hayo
alitoa ushahidi mahakamani kwamba CHADEMA haijawahi kuleta magaidi bali
kauli hizo za CCM zilikuwa ni za siasa za uchaguzi.
Hivi
karibuni, CCM imeghushi waraka mwingine na kuusambaza kile ilichodai
kuwa ni maazimio ya kamati kuu ya CHADEMA ya kupanga migomo ya walimu,
madaktari na mipango mingine ya kuhujumu serikali; hata hivyo waraka
huo ulidhihirika wazi kuwa ni wa kughushi.
Mikakati yote
hiyo michafu hupangwa na CCM mara kwa mara wakati ambapo CHADEMA
inaanza operesheni Sangara na mikakati mingine ya kuleta mabadiliko
nchini na kujipanga kuiondoa CCM madarakani kama ilivyo sasa ambapo
CHADEMA inaendelea na operesheni katika mkoa wa Morogoro hivyo
watanzania wanapaswa kuipuuza CCM na kuendelea kujiunga CHADEMA na
kuchangia mabadiliko kwa hali na mali mpaka kieleweke.
John Mnyika (Mb) Mkurugenzi wa Habari na Uenezi 12/08/2012- Dodoma