Mv skagit
KESI ya kuzama kwa meli ya Mv Skagit, inayowakabili watendaji watatu wa
Kampuni ya Meli ya Seagul, imesimamishwa kuendelea mahakamani kwa muda
usiojulikana.
Hatua hiyo ni kwa ajili ya kuipa nafasi Tume ya uchunguzi iliyoundwa na Rais wa Zanzibar kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.
Tume hiyo imeundwa kufuatia kuzama kwa meli ya Mv Skagit na kusababisha
vifo vya watu 139 waliokuwemo ndani ya meli hiyo iliyotokea Julai 18
mwaka huu karibu na maeneo ya kisiwa cha Chumbe wilaya ya Magharibi
Unguja.
Uamuzi wa kusimamishwa kwa kesi hiyo umetolewa na Naibu Mrajis wa
Mahakama Kuu Ali Ameir Haji, wakati alipokuwa akitolea uamuzi juu ya
suala hilo, lililosikilizwa Agosti 7 mwaka huu.
Katika maamuzi hayo Naibu Mrajis amesema kuwa, mahakama yake haioni
sababu ya kuendelea na kesi hiyo, kutokana na kwamba upande wa serikali
tayari umeshaunda Tume ya kuchunguza ajali iliyosababishwa na meli hiyo.
Amefahamisha kuwa anaamini kwamba mara baada ya Tume hiyo kukamilisha
uchunguzi wake itaibua mambo mengi yatakayohitajika kuchukuliwa hatua
kwa wahusika wake.
Akiyatilia mkazo maamuzi yake hayo, Naibu Mrajis asema kuwa jambo hilo
si geni katika mahakama hiyo, kwani Mrajis wa Mahakama Kuu George Joseph
Kazi tayari ameshawahi kuiondosha kwa muda kesi kuzama kwa meli ya Mv.
Spice Islanders I, ambayo inayofafana kimazingira na kesi hiyo.
Alisema kuwa, uamuzi huo umechukuliwa ni kutokana na mahakama hiyo
kupewa baadhi ya mamlaka ya kisheria ya kutoa maamuzi kabla kesi hiyo
haijafikishwa Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye uwezo wa kisheria wa
kuisikiliza kesi hiyo.
Alifahamisha, kimsingi kesi zote za Mahakama Kuu kabla ya kufikishwa
huko ni lazima zipitie mahakama za chini, ambazo kwa upande wake kuna
baadhi ya mambo inaweza kuyatolea maamuzi ya kisheria.
Hivyo kutokana na hoja hizo, Naibu Mrajis huyo wa Mahakama Kuu
amelazimika kuisimamisha kesi kuendelea mahakamani hapo kwa muda
usiojulikana.
"Ijapokuwa kesi hiii imesimamishwa lakini bado ipo mahakamani, kwa
wakati wote huo washitakiwa mtakuwa nje kwa dhamana na mtaitwa
mahakamani mara mtakapohitajiwa", alifahamisha Naibu Mrajis.
Kusimamishwa kwa kesi hiyo, ni nafasi ya pekee kwa upande wa mashitaka
kukamilisha upelelezi wake ambao hadi hivi sasa bado haujakamilika, na
pia ni fursa kwa Tume hiyo ya Uchunguzi kufanya kazi zake kwa ufanisi
zaidi.
Katika kikao kilichopita upande wa utetezi ulioongozwa na Wakili wa
kujitegemea Abdallah Juma wa Kampuni ya AJM Solicitors & Advocate
Chamber ya mjini Unguja, ameiomba mahakama hiyo kuisimamisha kwa muda
kesi hiyo kutokana na serikali kuunda Tume ya uchunguzi pamoja na kuupa
nafasi upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi wake.
Hoja hiyo ilipingwa na Mwanasheria wa serikali Sabra Mselem Khamis kwa
madai kuwa Tume hiyo haihusiani kabisa na kesi hiyo iliyokuwepo
mahakamani hapo, kwani washitakiwa wa kesi hiyo wameshitakiwa kwa kosa
la kuua bila ya kukusudia.
Washitakiwa wa kesi hiyo kwa pamoja wameshitakiwa kwa kosa la kuua bila
ya kukusudia kinyume na vifungu cha 195 na 198 vya kanuni ya adhabu
sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Washitakiwa hao ni Kepteni wa Mv Skagit Mussa Makame Mussa (49) mkaazi
wa Kazole, Said Abdulrahman Juma (46) wa Mwembetanga ambaye ni
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ya Seagull, pamoja na Meneja wake wa tawi la
Dar es salaam Omar Hassan Nkonje (50) anayeishi Magomeni.
Wote hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 60 ya kuua watu
waliokuwemo ndani ya meli hiyo, tukio ambalo lilitokea karibu na maeneo
ya kisiwa cha Chumbe kilichopo wilaya ya Magharibi Unguja, tukio
lililotokea majira ya saa 7:30 za mchana wa Julai 18 mwaka huu.
Katika maelezo yaliyotolewa mahakamani hapo ilifahamishwa kuwa,
washitakiwa wote hao wakiwa na dhamana na majukumu ya kuchukuwa abiria
na mizigo yao, kwa uzembe walishindwa kuchukua tahadhari katika majukumu
yao pasi na kuzingatia usalama na kusababisha meli hiyo kuzama na
kusababisha vifo vya abiria hao.
Washitakiwa wote wapo nje kwa dhamana ya fedha taslimu shilingi
5,000,000 pamoja na wadhamini wawili kila mmoja waliosaini bondi ya kima
kama hicho cha fedha, na mmoja kati ya wadhamini hao ni mfanyakazi wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
No comments:
Post a Comment