Huenda akaichezea Man City katika mechi dhidi ya QPR siku ya Jumamosi
Scott Sinclair ameihama klabu ya ligi kuu ya Premier
ya Swansea, na kujiunga na Manchester City, kwa kutia saini mkataba wa
miaka minne.
Klabu hiyo ya Wales awali ilikataa pauni milioni 6.2 kutoka kwa Man City, lakini hatimaye baada ya nyongezanyongeza, hatimaye kwa jumla Man City ikafikisha pauni milioni 8.
Sinclair, mwenye umri wa miaka 23, hivi majuzi aliichezea Uingereza katika mashindano ya Olimpiki, na huenda akawa katika kikosi cha meneja Roberto Mancini ambacho kitapambana na Queen Park Rangers siku ya Jumamosi.
"Ninafurahi sana kwamba yote yametulia, na sasa mimi ni mchezaji wa City....ni vigumu hata kusubiri," alielezea Sinclair.
"Kulikuwa na nyakati ambazo nilifikiria hayo hayatawezekana, kwa hiyo nimeridhika kwamba hatimaye nimefika hapa."
"Kucheza ukiwa na baadhi ya wachezaji maarufu zaidi ulimwenguni ni jambo ambalo linasisimua. Wakati unapotizama ratiba na kuona mechi mbili dhidi ya Real Madrid katika ligi kuu ya klabu bingwa, basi unahisi ukweli wa yote haya."
Meneja wa Swansea, Michael Laudrup, alisema "Scott anaelekea kwa klabu kubwa ambayo ina wachezaji maarufu. Yeye ana maarifa mengi, lakini itabidi ashindanie nafasi ya wachezaji 11 watakaokuwa uwanjani mara kwa mara."
Sinclair zamani alikuwa akiichezea timu ya is England ya vijana chini ya umri wa miaka 21, na alianzia Bristol Rovers, kabla ya kujiunga na Chelsea.
Lakini baada ya kutoweza kushirikishwa katika mechi mara kwa mara katika uwanja wa Stamford Bridge, alihama kwa mkopo katika timu ya Plymouth, na pia kuzichezea QPR, Charlton, Crystal Palace, Birmingham na Wigan, kabla ya Swansea kuamua kumchukua mwezi Agosti, mwaka 2010, kwa pauni 500,000.
Sinclair alicheza mechi 82 chini ya klabu ya Swansea, na alifunga magoli 28.
No comments:
Post a Comment