Mkurugenzi
wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari BASATA Godfrey Mungereza akitoa
ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu sekta ya muziki nchini.
Mdau
wa Sanaa na mkongwe wa muziki wa dansi nchini John Kitime (kushoto)
akisistiza jambo wakati akiwasilisha mada kuhusu Historia ya Muziki
nchini kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa
Idaya ya Ukuzaji Sanaa BASATA Vivian Shalua na Mkurugenzi wa Idara ya
Utafiti, Mafunzo na Habari Godfrey Mungereza.
Rais
wa Shindano la Urembo la Miss Utalii Gideon Chipungahelo naye hakuwa
nyuma katika kuchangia juu ya tasnia ya muziki nchini.
Mzee Kassim Mapili aliwaeleza vijana hali ya tasnia ya muziki ilivyokuwa huko nyuma na mabadiliko yaliyopo sasa.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limevitaka vyombo vya habari kuwa
mstari wa mbele katika kudhibiti kazi za Sanaa zisizo na maadili kabla
ya kwenda hewani ili kuepuka mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Wito huo umetolewa mapema wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji
Sanaa BASATA Vivian Shalua wakati akiiahirisha programu ya Jukwaa la
Sanaa inayofanyika kila wiki kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif
Shamba jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa, wakati Baraza limefikia hatua nzuri ya kudhibiti hali
hiyo, wadau wakuu katika kumaliza tatizo hili ni wasanii wanaotakiwa
kutunga kazi bora na zenye maadili huku vyombo vya habari vikiwa na
wajibu wa kuchuja kila kazi ya Sanaa inayopokelewa kabla ya kuirusha
hewani.
“Basata imeshaviandikia vyombo vya habari kuvielekeza kuwa na kamati
za ndani za kudhibiti maadili kwenye kazi za sanaa kabla ya hazijaenda
hewani. Hili ni muhimu sana katika kujenga maadili ya mtanzania”
alisisitiza Shalua.
Awali akiwasilisha mada kuhusu Historia ya Muziki nchini na hatua
zake mkongwe wa muziki wa dansi nchini John Kitime alisema kuwa,
kumekuwa na changamoto mbalimbali miongoni mwa wasanii wa fani hiyo hali
inayoufanya usifike mbali.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na wasanii
kutozingatia sheria ya hakimiliki na hakishiriki iliyopo, kuiga midundo
ya muziki kutoka nje hali inayosababisha kutokuwepo kwa muziki wenye
utambulisho wa Tanzania kama ilivyo kwa
mataifa mengine ya Afrika hususan Afrika Kusini.
“Tatizo kubwa ni wasanii wetu kuiga miziki na hata tamaduni za
kigeni, hatuwezi kuandaa kazi za Sanaa kufurahisha wazungu au watu
kutoka nje tu, tutapotea” alionya Kitime.
Kwa upande wake Rais wa Shindano la ulimbwende la Utalii (Miss
Utalii) Gideon Chipungahelo alisema kuwa, kihistoria wanamuziki wetu
ukianza na wakongwe waliopo walijikita katika kuiga miziki ya Zaire
hivyo kinachofanywa na wasanii wetu wa sasa ni mwendelezo tu.
“Ni wazi kazi iliyopo sasa ni kuwafanya wasanii kujikita katika
utajiri mwingi wa makabila yenye midundo mbalimbali tuliojaaliwa. Hapa
ndipo tunapaswa kusisitiza” alishauri Chipungajelo.
Mzee Kassim Mapili aliwaeleza vijana hali ya tasnia ya muziki ilivyokuwa huko nyuma na mabadiliko yaliyopo sasa.
No comments:
Post a Comment