Rais Chama cha Walimu nchini (CWT) Gratian Mukoba.
NDUGU
zangu, wiki nzima iliyopita nchi imejikuta ikitikisika kutokana na
mgomo wa walimu uliotanda sehemu mbalimbali nchini wakiishinikiza
serikali kuwalipa stahiki zao, huku ukiathiri sekta ya elimu katika
ngazi za shule za msingi na sekondari za umma kwa kiasi kikubwa.
Kutokana
na taarifa mbalimbali ukweli ni kwamba katika sehemu nyingi za nchi
walimu waligoma kuingia madarasani na wengine walifika tu kazini na
kusaini vitabu vya mahudhurio kisha kuondoka. Kama mzazi, hii inauma
sana!
Inauma kwa sababu watoto wetu wanakosa elimu na wengine wapo
darasa la saba huku wengine wakiwa kidato cha nne au cha sita, wote
siku zijazo watafanya mitihani bila kujali kama walikuwa wakifundishwa
au la.
Wahenga walisema tembo wawili wapiganapo, ziumiazo nyasi.
Ndivyo ilivyo, walimu na serikali wanapogombana watakaoumia ni
wanafunzi. Ni wazi wengi watafeli mitihani yao kwani watakuwa nyuma ya
silabasi.
Cha ajabu ni kwamba licha ya walimu kugoma, wanafunzi katika baadhi ya shule za msingi walifanya maandamano kupinga hatua hiyo.
Wengi
walionekana katika vyombo vya habari wakiandamana na kupiga kelele
wakisema mgomo huo ulikuwa unawanyima haki yao ya msingi ya kupata
elimu.
Picha za luninga na magazeti zilionyesha madarasa katika
baadhi ya shule yakiwa matupu au yakiwa na wanafunzi lakini bila kuwapo
walimu. Picha nyingine zilionyesha wanafunzi wakiwa madarasani
wakifundishwa na wenzao waliochukua nafasi za walimu wao.
Wengi
tunajiuliza, nani aliwahamasisha wanafunzi hao kufanya maandamano nchi
nzima? Ni swali gumu la kitendawili ambacho huenda itakuwa vigumu
kukitegua katika siku zijazo kwani halihitaji majibu mepesi.
Kinachonishangaza
mimi bila shaka na Watanzania wengine ni hatua ya jeshi la polisi
kumwaga askari wenye silaha za moto barabarani kukabiliana na watoto
hao wa shule waliokuwa wakiandamana.
Ilisemwa kuwa walikuwa
wakielekea katika ofisi za mamlaka husika kupinga mgomo huo ambao Chama
cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema hautakuwa na kikomo.
Tuliona
katika magazeti baadhi ya polisi wakitumia nguvu kupita kiasi
kuwakamata wanafunzi hao kama wanavyofanya wanapowakamata majambazi
wenye silaha za moto au za kivita.
Hapa ndugu zangu natoa
ushauri wa nini kifanyike licha ya serikali kujiona imeshinda
mahakamani dhidi ya walimu, warudi katika meza ya mazungumzo kwa lengo
la kupata maridhiano.
Kwanza, niseme wazi kuwa walioishauri
serikali kupeleka suala hilo mahakamani hawakutumia busara kwa kuwa
lilikuwa bado linazungumzika.
Kusema kweli haitoi picha nzuri hata
kidogo kwa serikali kukimbilia mahakamani kila inapoingia katika
migogoro na wafanyakazi na haipaswi kuiona mahakama kama kimbilio pekee
kila wakati Tume ya Usuluhishi na Uamuzi inaposhindwa kutatua mgogoro
katika muda mfupi.
Sehemu nyingi duniani tumekuwa tukiona kwamba
utatuzi wa migogoro unahitaji uvumilivu na subira kubwa kwa pande
zinazopatanishwa.
Msisitizo hapa ni kwamba, mchakato mzima wa
kumaliza mgogoro wowote ule unahitaji kuvumiliana, kusikilizana na
kuheshimiana. Kwa maana ya kila upande kujaribu kuelewa hoja za
mshindani wake.
Lakini pia kila upande katika mgogoro unatakiwa
kutambua na kukubali ukweli kuwa, katika mapatano ya usuluhishi hakuna
upande unaoweza kupata kila kitu unachotaka.
Kwa mfano, katika
mgogoro huu ulio mbele yetu, walimu lazima waelewe kwamba hawawezi
kuongezewa mshahara kwa asilimia 100 kama wanavyotaka.
Kwa mtu
anayefikiri kwa kina na kutafakari mambo, atagundua utamaduni wa
serikali kukimbilia mahakamani badala ya kutafuta maridhiano na
wafanyakazi ni uthibitisho kwamba sheria za kazi zina mapungufu makubwa.
Kwa
mfano, inakuwaje Kifungu cha 83(4)g cha Sheria ya Ajira na Mahusiano
Kazini Namba 6 ya mwaka 2004 itamke kwamba mwajiri hatalazimika kulipa
mshahara kwa mtumishi aliyeshiriki katika mgomo, hata pale ambapo chama
cha wafanyakazi kitakuwa kimefuata sheria na taratibu zote za kutangaza
mgomo?
Katika sakata la mgogoro huu serikali imesema mgomo wa
walimu uliokuwa ukiendelea ni batili kwa sababu shauri lake lilikuwa
mahakamani.
Kwa tafsiri na wasomi na watu wanaotafakari mambo mazito
ni kwamba pengine kitendo cha serikali kukimbilia mahakamani kuzuia
wafanyakazi wasitekeleze haki yao ya kugoma baada ya kufuata sheria na
taratibu zote zilizowekwa ni matumizi mabaya ya mhimili huo wa dola
maana sheria ni msumeno.
Njia pekee ya kumaliza mgogoro ni wizara ya
elimu chini ya Waziri Dk. Shukuru Kawambwa kukaa meza moja na CWT chni
na kiongozi wao, Gratian Mkoba kujadiliana. Hata watu wanaopigana vita
hufanya hivyo, kwa nini serikali na CWT washindwe? Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
No comments:
Post a Comment