Gari ambalo marehemu Aliungua Nalo
TUKIO
la mwanamke Rehema Nungu kukutwa ameteketea kwa moto ndani ya gari aina
ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T 883 BLA katika msitu wa
Mabwepande, jijini Dar Agosti 1, 2012 linazidi kugusa akili za wengi
hasa kutokana na utata wa tukio lenyewe na hii ndiyo ripoti kamili.
Taarifa zilizopenyezwa na ndugu mmoja wa Simon Sakilu ambaye ni mume wa
marehemu, zinadai kuwa kabla ya tukio hilo, Rehema na mumewe walikuwa
kwenye ugomvi mzito usiokuwa na dalili ya kumalizika.
MAELEZO YA UPANDE WA MWANAUME
Habari zinadai kwamba marehemu
alikuwa akidaiwa fedha na mfanyabiashara mmoja (hakutajwa jina) lakini
mumewe hakulijua deni hilo mpaka siku za mwisho za uhai wa Rehema ambapo
hata hivyo hakumuuliza.
Aidha, ikadaiwa kwamba mfanyabiashara huyo
alikuwa akimdai marehemu kwa vitisho kwamba asipolipa atamwambia mumewe,
jambo ambalo mwanamke huyo hakutaka litokee.
Siku ya tukio, habari
zinadai kuwa marehemu aliamka mapema na kufanya shughuli za nyumbani na
baada ya muda inadaiwa alikunywa sumu ambayo haikujulikana ni ya aina
gani.
Ikazidi kudaiwa kuwa baada ya kitendo hicho, mumewe alifanya
juhudi za kumnywesha maziwa ili kuokoa uhai wake lakini ilishindikana
kufuatia mke kumzidi nguvu mumewe na kukimbilia kwenye gari na kuondoka
nyumbani kwenda kusikojulikana.
“Mwanamke alipokunywa sumu, mumewe
(Simon)alifanya juhudi za kumpa maziwa ili kuokoa maisha yake lakini
alizidiwa nguvu, mke akatoka na gari na kwenda kusikojulikana.
“Simon alikwenda kukutana na mdai wa mkewe na kumlipa fedha zake
akiamini mkewe alikunywa sumu kwa sababu ya deni, baada ya malipo
akampigia simu mkewe ili kumtaarifu lakini simu hiyo ilikuwa inaita na
kukatika, baadaye haikupatikana kabisa,” alisema ndugu huyo ambaye
aliomba hifadhi ya jina lake gazetini.
Kuanzia hapo, ndugu walianza
kumsaka Rehema mpaka Agosti 2 mwaka huu habari zilipopatikana habari
kwamba kuna gari limekutwa limeteketea kwa moto kwenye msitu wa
Mabwepande. Mtu aliyedaiwa ndiye alikuwa dereva naye alikuwa ameungua na
kubaki majivu na fuvu likiwa sehemu ya kiti.
Hata hivyo, ndugu
hawakutaka kuweka msiba wakiamini aliyefariki dunia kwa moto huo anaweza
asiwe Rehema. Ili kujiridhisha na hilo, walichukua mabaki hayo na
kuyapeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa vipimo vya DNA.
MUME ANA SIRI NZITO?
Habari zaidi kutoka ndani ya familia hiyo zinadai kuwa huenda Simon ana
siri nzito juu ya kifo cha mkewe Rehema kwani haingii akilini mume
kuzidiwa nguvu na mkewe wakati wa kumsaidia kumnywesha maziwa.
Aidha, mpenyesha habari huyo aliendelea kufunguka kwamba ilikuwa ni
kawaida kwa wanandoa hao kutibuana na mke kwenda anakojua hata kwa siku
tatu bila mwanaume kujishughulisha kumtafuta.
MAELEZO UPANDE WA MKE
Agosti 6, 2012 mapaparazi wetu walifika nyumbani kwa marehemu Rehema,
Mbezi Beach, Dar na kukuta watu wachache ikidaiwa hali hiyo ilitokana na
wengi kutoamini kama Rehema alifariki dunia. Mume wa marehemu hakuwepo
msibani hapo bila kujulikana alikokwenda.
Alipotafutwa ndugu wa
marehemu kuzungumzia suala hilo, kila mmoja aliruka na kudai mwenye
uwezo wa kuzungumzia jambo hilo ni mama mzazi ambaye naye aligoma kusema
lolote.
“Mwenye uwezo wa kuzungumzia suala hilo ni mama mzazi
lakini amegoma kwa madai kuwa hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa vile
anahisi kuna mchezo mchafu umefanyika,” alisema ndugu mmoja.
Hata
hivyo, mtu mmoja wa karibu na familia ya marehemu alisema kuwa habari
kamili juu ya msiba huo zitapatikana mara baada ya kupata vipimo kutoka
kwa mkemia mkuu kubaini kama kweli aliyekutwa ameteketea kwa moto ndani
ya gari ni Rehema.
“Ni vigumu kulizungumzia suala hili kwani
linatatanisha, unaweza kusema aliyekufa ni Rehema na matokeo ya mkemia
mkuu yakitoka yakaonesha tofauti, inaweza kuleta shida, tusubiri majibu
kwanza,” alisema mtu huyo bila kutaja jina lake.
MAJIBU YA MKEMIA MKUU YATOKA
Agosti 10, 2012 mmoja wa ndugu wa marehemu alimpigia simu mwanahabari
wetu na kumweleza kuwa majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali yametoka na
kubaini kwamba aliyekufa ni Rehema Nungu.
“Kama unavyosikia vilio
hivyo, nipo msibani, majibu ya mkemia mkuu yamebaini aliyekufa ni Rehema
Nungu, taratibu za mazishi zinafanywa sasa ila naomba muende nyumbani
kwa Simon mtapata habari kamili,” alisema ndugu huyo na kusisitiza kuwa
kama msiba utafanyika kwa mume wa marehemu, hawatakwenda ila watakwenda
makaburini tu.
NYUMBANI KWA SIMON
Baada ya kupata taarifa
hizo, waandishi wetu walifika nyumbani kwa Simon, Tegeta Nyuki, Dar na
kumkuta msemaji wa familia hiyo aliyejulikana kwa jina moja la Dedu.
Dedu alipopewa pole ya msiba na kutakiwa kueleza sababu za kifo cha
marehemu, alisema waulizwe polisi yeye hawezi kusema chochote licha ya
kukutwa na picha ya marehemu mkononi.
“Siwezi kusema chochote,
kamuoneni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ana habari zote za msiba huu,
naomba mniache niendelee na taratibu za hapa,” alisema Dedu.
HUYU HAPA KAMANDA WA MKOA WA PWANI
Agosti 10, 2012 mwandishi wetu alitinga katika ofisi ya Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu kwa lengo la kujua chochote kuhusu
kifo cha mwanamke huyo lakini hakuwepo, ikabidi apigiwe simu yake ya
kiganjani ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Ni kweli majibu ya
tukio hilo yametoka, mtu aliyeteketea kwa moto ndani ya gari ni Rehema
lakini sipo katika nafasi nzuri ya kuongea kwani niko Muhimbili
nashughulikia majeruhi wa ajali ya wanakwaya wa kutoka Kenya.
“Hata
kesho (Agosti 11) sitakuwa ofisini kwani nitakuwa bado nashughulikia
suala hilo, waliofariki ni raia wa nje hivyo ni vyema nikahakikisha
wanasafirishwa kurudi kwao,” alisema Kamanda Mangu.
UTATA
Asubuhi ya Agosti 11, 2012, wanahabari wetu walidamkia nyumbani kwa Simon ili kutaka kujua taratibu za mazishi.
Nje ya nyumba alikuwepo Dedu na mzee mmoja ambaye hakutaka kutaja jina
lake, akasema yeye ni makamu mwenyekiti wa kamati ya mazishi. Wawili hao
waligoma kuongea chochote kwa madai yaleyale, suala liko polisi.
Hata hivyo, muda huohuo simu ya Dedu iliita, alipopokea ilionekana
kupigwa na ndugu mmoja wa marehemu ambaye alisema mazishi ya mabaki ya
mwili wa Rehema (fuvu na majivu) yangefanyika Jumamosi au Jumapili
iliyopita lakini baada ya kupata kibali kutoka kwa mkemia mkuu.
Baadaye habari kutoka ndani ya familia ya Rehema zilisema kibali cha
kuzika masalia ya mwili wa marehemu kilikuwa kipatikane jana Jumatatu.
Marehemu Rehema ameacha watoto wawili, Ngimba na Muheri.