tangazo

Tuesday, July 9, 2013

CHADEMA WASUSIA KONGAMANO LA TCD.

MAPIGANOARUSHA CHADEMA11 a80f6

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema hakitashiriki kongamano la amani lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), chini ya ufadhili wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaila, alisema chama chake kinazo sababu nyingi za kususia kongamano hilo.

Katika taarifa hiyo, Kigaila alimtuhumu Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia, kwamba amekiuka maazimio ya kikao cha kuteua mwezeshaji wa mkutano huo na badala yake amefungamana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uteuzi.Alisema Chadema haitashiriki kwa sababu amani ya nchi haijadiliwi na watu 70, bali amani inatengenezwa kwa kuzingatia uwepo wa mazingira ya haki na usawa.


Kigaila alisema Serikali, ambayo inatuhumiwa kwa uvunjifu wa haki za binadamu, haiwezi kujisuluhisha yenyewe na kuongeza kwamba amani si mali ya vyama vya siasa, bali ni tunu inayohusisha wadau mbalimbali.Alisema Pinda, ambaye amekuwa mstari wa mbele kutoa lugha za uchochezi, chuki, uhasama, ubabe, ukiukwaji na za vitisho, hawezi kuwa na fursa ya kuwa mwenyekiti wa kongamano la amani.Kigaila alisema chama chake hakitashiriki kwa sababu Serikali ya CCM imejaa unafiki, kwani imekuwa ikihubiri amani mchana wakati usiku inachochea udini na kuwagawa Watanzania kwa misingi ya imani za kidini na vyama.“Tumepokea barua saa saba leo (jana) kutoka TCD ikitualika kushiriki kongamano la amani, tumekutana kwa dharura kujadili mwaliko huo wa ghafla.“Tunataka umma utuelewe kwamba tuna dhamira ya dhati ya kuona Tanzania inakuwa kisiwa cha amani, lakini hatukubali kushiriki katika vikao ambavyo viongozi hawana dhamira nzuri, hatutaki kutumia gharama ya Sh milioni 400 ambazo ni kodi za Watanzania wanyonge bila mafanikio,” alisema.Mbatia atoa ufafanuzi Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia, aliishangaa Chadema kwa uwamuzi huo na kusema kuwa tuhuma zilizoelekezwa kwake ni za uwongo.Mbatia, ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema Pinda hawezi kuendesha kongamano hilo kwa kuwa yupo katika safari ya kikazi mkoani Njombe.“Ni vema wenzetu wasusia wafanye hivyo kwa jambo la msingi, lakini si katika hili. Kwanza nawashangaa wanasusiaje wakati wao walishiriki kikao cha kupanga kongamano hili Februari 7, mwaka huu Dodoma,” alisema.Kwa mujibu wa Mbatia, mada zilizopangwa kujadiliwa ni amani na demokrasia itakayowasilishwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ole Gabriel na vyombo vya habari na usalama itakayowasilishwa na mwandishi wa habari mkongwe, Ayoub Rioba.

No comments:

Translate