tangazo

Monday, August 27, 2012

KUMBE MATESO YA VENGU WACHAWI NI WENZIE WA ORIGINAL COMEDY NDIO CHANZO.

MUIGIZAJI Joseph Shamba ‘Vengu’, ameugua kwa muda mrefu. Ukitazama tukio la msanii huyo kuumwa, unaweza kuhisi kuwa wenzake kwenye kundi hilo walikuwa pamoja naye. Si kweli, wao ndiyo sababu ya mateso yake.

Vengu hajawahi kuwa na furaha akiwa na Kundi la Orijino Komedi. Wenzake walimtenga na kumfanyia mambo mengi ya kuumiza. Maskini ya Mungu, Vengu akaona kujipoza na machungu ya kutengwa, kunyanyaswa na wenzake ni kuwa mlevi.

Makala haya, shabaha yake ni kuwafanya Orijino Komedi kuwa wamoja. Wajione kwamba kila mmoja kwenye kundi hilo ana haki sawa. Si kubaguana na kutendeana mambo ya kuumiza kama alivyotendwa Vengu kwa muda mrefu.

Kama memba wengine wa Orijino Komedi, Isaya Mwakilasa ‘Wakuvwanga’, Mjuni Silvery ‘Mpoki’, Lucas Mhuvile ‘Joti’, Emanuel Mgaya ‘Masanja’ na Alex Chalamila ‘McRegan’ wangemfanya Vengu kuwa sehemu ya maisha yao, asingeteseka kama ilivyotokea.

Ingewezekana kabisa kwa memba wa kundi hilo kumpa faraja, badala ya kumtenga na kumsababishia aishi kwa mawazo. Kitendo cha kumbagua kilisababisha aone pombe ndiyo kimbilio lake. Kabla hajazidiwa, alipenda kulewa akiamini ndiyo faraja yake.

Mimi na Vengu tumewahi kufanya vikao kadhaa na kuzungumzia yale yanayomsibu. Alipenda sana kuficha ukweli unaomuumiza kwamba kuna baadhi ya wasanii wenzake wanamtenda ndivyo sivyo. Maskini Vengu, namuombea kwa Mungu azidi kumpa afua, apone kabisa.

Mungu mwingi wa rehema zote, kubwa na ndogo, atamponya Vengu. Bila shaka atarudi kwenye hali yake ya kawaida. Ninaamini kuwa hata hali yake ya kutawaliwa na msongo wa mawazo, itapona. Hatakuwa mlevi tena kama ilivyokuwa mwanzo.

Ugonjwa wa Vengu una matawi mengi. Kwa nafasi yangu ya uandishi wa habari pendwa, nilinasa taarifa za awali kuhusu kuumwa kwa Vengu. Kuna baadhi ya watu hawakutaka kuelewa chochote zaidi ya kushikilia kwamba msanii huyo ameshughulikiwa na wenzake.

Yupo msanii mmoja wa Kundi la Orijino Komedi alitajwa mno. Hata hivyo, hilo la uchawi sikulipa nafasi ndiyo maana hata habari hiyo hatukuwahi kuiripoti. Sisi Global Publishers tumestaarabika, hatuamini uchawi. Nilimshauri mtoa habari akazanie huduma za hospitali.

Wakati huo Vengu amelazwa Hospitali ya Taifa, Muhimbili. Mara kadhaa nyakati za jioni, nilikutana na mtoa habari za uchawi (kwamba msanii wa kundi hilo kamroga Vengu). Kwa busara, nikawa namshauri taratibu ili aondokane na imani hizo. Nauchukia ushirikina.

Hata hivyo, wakati mwingine inakuwa rahisi kupata picha kuwa mtindo wa maisha ya wasanii hao dhidi ya mwenzao ndiyo sababu ya kuibuka kwa hisia za uchawi. Wangempenda na kumjali siku zote ndani ya kundi hilo, asingehisi kama anarogwa. Ndugu na rafiki zake, wasingewahisi vibaya wenzake.

Sijawahi kusikia malalamiko kutoka kwa ndugu zake wakisema Vengu amerogwa. Zaidi marafiki ndiyo walikuwa wakieneza habari hizo. Inawezekana kwa marafiki kwa sababu ndiyo aliochangia nao mazungumzo na hata vikao vya baa.

Bila shaka, hata wale marafiki zake waliokuwa hawataki kuelewa kwamba Vengu anaumwa na siyo uchawi, leo hii watakuwa mashahidi. Kwa wakati ule, kuna mtu (simtaji jina kwa sasa), alinishutuma kwamba mimi ni muoga, eti kwa sababu nilisema sitaandika habari ya Vengu kurogwa.

Awamu nyingine niliambiwa nimehongwa. Tuhuma zote hizo nilizibeba kwa sababu sikutaka niwaridhishe watu kwa muda, nikasahu maumivu ya baadaye itakapothibitika kwamba niliandika habari ya uongo ambayo sitaweza kuitetea. Siku zote uchawi hauthibitishiki.

 Wakati mwingine nilicheka kwa sababu sikumuona mwenye ubavu wa kunihonga kuzuia habari hiyo. Nilikataa habari kwa maana ingeweza kuibua matokeo mabaya. Kusema Vengu amerogwa kwa hali aliyokuwa nayo, ni uchochezi usiovumilika.

Unaweza kumuona Vengu ni wa kawaida kwako, lakini kwa wengine (hususan wazazi na ndugu zake) ni kila kitu kwao. Kuandika Vengu amerogwa, siyo tu ingeibua chuki kati ya ndugu zake na wasanii wa Orijino

Komedi, bali pia ndugu wangeweza kumtorosha kumpeleka kwa ‘babu’.
Sisi Global huwa tunaangalia maeneo yote hayo kabla ya kuchapisha habari zetu. Hekima hizo ndizo zimetufikisha hapa tulipo. Kila habari inapimwa kwenye mzani, pumba zinawekwa pembeni halafu ukweli unatangulizwa mbele.

Leo ninapogusia uchawi, namaanisha kwamba wasanii wa kundi hilo wanatakiwa kuishi vizuri. Wasitengane, kwani hali hiyo ndiyo chanzo cha kuibua hisia mbaya miongoni mwao. Orijino Komedi wanapaswa kujirudi kwa Vengu.

Je, unajua kwamba wakati wasanii wa kundi hilo wakiwa bado wanafanya kazi zao kwenye Televisheni ya Channe 5 (EATV), walipewa nyumba ya kuishi na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi? Nyumba hiyo ipo Kunduchi, Dar es Salaam.

Vengu alifukuzwa kwenye nyumba hiyo, akiwaacha wenzake wanatanua. Habari hiyo iliandikwa, kumbukumbu tunazo. Haikuishi hapo, walipohamia TBC1, walipewa magari lakini baada ya muda mfupi,
Vengu alinyng’anywa gari, akawa anatembea kwa daladala, wenzake wana magari yao.

Utakubaliana na mimi kwamba wasanii wenzake walimpa unyonge mkubwa kiasi kwamba mwenyewe akawa hana la kutuliza akili zaidi ya kunywa pombe. Tuna mlolongo wa matukio mengi ya msanii huyo kuharibikiwa baada ya kuzidiwa na kiwango kikubwa cha pombe alichokunywa. Ametendwa sana!
 
Imeandaliwa na Luqman Maloto

No comments:

Translate