tangazo

Friday, August 17, 2012

Kikwete azitaka Barca, Madrid kuja nchini






RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa bado Serikali ina dhamira ya kuileta moja ya timu za Ligi Kuu ya Soka ya Hispania, 'La Liga' kuja Tanzania na amemtaka Balozi mpya wa Hispania nchini kusaidia kufanikisha mpango huo.
Aidha, Kikwete ameipongeza Hispania kwa kufanikiwa kutetea ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Ulaya katika mashindano yaliyomalizika mwezi uliopita nchini Poland na Ukraine.


Rais Kiwete alisema hayo jana Ikulu, jijini Dar es Salaam katika hafla ya utambulisho wa balozi mpya wa Hispania nchini, Luis Manuel Cuesta Civis.

Kikwete alisema: “Wananchi wa Tanzania, ambako timu za Hispania, zina washabiki na wafuasi wengi, bado wanasubiri kwa hamu ziara ya moja ya timu kubwa za Ligi Kuu ya Soka ya Hispania. Tunataka ije hapa, icheze mechi moja ama mbili na itembelee mbunga zetu maarufu za wanyama.”

Aliongeza:“Kama utakavyokuja kuthibitisha mwenyewe, Watanzania ni watu wanaopenda michezo na hasa soka na ni wafuatiliaji wakubwa wa Ligi Kuu ya Hispania ambako timu zenye mvuto zaidi ni Real Madrid na Barcelona.”
“Tunawapongeza sana kwa kuweka historia. Kwanza mlishinda Kombe la Mataifa ya Ulaya, kisha mkashinda Kombe la Dunia. Sasa mmeweza kutetea Kombe la Ulaya. Hili halijapata kutokea kwa nchi moja kushikilia
vikombe vyote viwili vikubwa vya soka duniani kwa wakati mmoja ama nchi kutetea Kombe la Ulaya.”
Wakati huohuo, serikali imesema imeridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wanamichezo walioshiriki michezo ya Olimpiki iliyomalizika Jumapili iliyopita, London, England.

Pamoja na wanamichezo hao kurudi bila medali, lakini serikali imesema wanastahili pongezi kwa vile walijitahidi kushindana kadri walivyoweza.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Leonard Thadeo wakati wa hafla ya chakula
cha usiku kwa wanamichezo iliyofanyika muda mfupi baada ya kuwasili.

"Mmetujengea heshima kubwa Olimpiki, miaka ya nyuma wanamichezo wetu waliokuwa wakituwakilisha baada ya mashindano wanazamia uko, lakini nyinyi hakufanya hivyo" alisema Thadeo.Mbali na

kuwapongeza wanamichezo hao, pia Thadeo aliwakabidhi vyeti na medali za ushiriki kwenye michezo ya Olimpiki.

Katika michezo hiyo, Tanzania iliwakilishwa na wanamichezo wa masumbwi, riadha na kuogelea, ambapo waliishia hatua ya makundi.

No comments:

Translate