tangazo

Friday, August 17, 2012

Yondan, Chombo wasubiri rungu la kamati




KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imesema itasimama kwenye mstari ulionyoka kutoa uamuzi kwa wachezaji wataonekana katika orodha ya usajili zaidi ya timu moja.

Akizungumza na Mwananchi jana, mwenyekiti wa kamati hiyo, Alex Mgongolwa alisema hakutakuwa na upendeleo katika kutoa uamuzi wa utata wa wachezaji.

Mgongolwa alisema, kamati yake inatambua hali halisi ya zoezi zima la usajili kwa klabu za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza, hivyo watakuwa makini.

"Nia yetu siyo kuendeleza matatizo, tunachotaka kwa sasa ni kumaliza utata wa usajili kwa haki, na tutafanya hivyo bila upendeleo," alisema uliopo Mgongolwa.

Kuhusu madai kutoka kwa baadhi ya watu kuituhumu kamati yake kutoa umauzi wa upendeleo hasa kwa klabu ya Yanga, alisema: "Hapa tunafuata kanuni, suala la upendeleo hakuna. Hapa hakuna Simba wala Yanga."

"Tutaangalia kanuni zinasemaje kama mchezaji amesaini zaidi ya timu moja, tutangalia pia mazingira yaliyotumika,  hatutaibeba klabu yoyote katika hili, wengi wamekuwa wakisema Yanga imekuwa ikipendelewa siyo," alisema.

Kauli ya Mgongolwa imekuja siku chache kupita tangu Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Aden Rage, ambaye pia alikuwa mjumbe kwenye kamati Mgongolwa, kutangaza kujiuzulu.

Katika madai yake, Rage aliseme amefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa, kamati hiyo imekosa uaminifu kwa vile imekuwa ikitoa uamuzi kwa upendeleo na kwamba siku zote imekuwa ikiikandamiza klabu yake.

Tayari suala mgongano wa usajili wa klabu tatu kubwa, Simba, Yanga na Azam limeshaonekana kufuatia majina ya wachezaji watatu kuonekana kwenye orodha ya timu hizo.

Beki Kelvin Yondan aliyesajiliwa na Yanga kutoka Simba, jina lake liko kwenye orodha ya timu zote mbili zilizowasilishwa Jumatano wiki hii.

Vilevile, jina la mchezaji Ramadhan Chombo, ambaye Simba wanadai kumsajili kutoka Azam FC, limo kwenye orodha ya Wekundu hao wa Msimbazi kama ilivyo kwa Azam.

Wakati huohuo, timu zote zitakazoshiriki Ligi Kuu msimu wa 2012\2013, zimewakilisha usajili wao mpaka kufikia jana asubuhi.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema timu tano tu za Daraja la Kwanza ndizo zilizowasilisha usajili kufikia jana kati ya 24 zilizopaswa kufanya hivyo.

Osiah, alikiri kuwapo na utata wa usajili wa baadhi ya wachezaji na kusema suala hilo litatolewa uamuzi mapema na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi ya Wachezaji.

"Kuna utata umejitokeza kwa baadhi ya fomu za usajili kwa wachezaji wa timu za Simba ,Yanga na Azam, kamati husika katika hilo itatoa ufafanuzi," alisema Osiah.

Kuhusu timu za Daraja la Kwanza zilizowasilisha majina ni pamoja na Tesema, Polisi na Transit Camp (Dar es Salaam), Mkamba, Moro United (Morogoro).

No comments:

Translate