tangazo

Monday, August 13, 2012

Kesi kuzama Mv. Skagit yasimamishwa

                                                                             Mv skagit
 
 
 
 KESI ya kuzama kwa meli ya Mv Skagit, inayowakabili watendaji watatu wa Kampuni ya Meli ya Seagul, imesimamishwa kuendelea mahakamani kwa muda usiojulikana.
Hatua hiyo ni kwa ajili ya kuipa nafasi Tume ya uchunguzi iliyoundwa na Rais wa Zanzibar kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.
Tume hiyo imeundwa kufuatia kuzama kwa meli ya Mv Skagit na kusababisha vifo vya watu 139 waliokuwemo ndani ya meli hiyo iliyotokea Julai 18 mwaka huu karibu na maeneo ya kisiwa cha Chumbe wilaya ya Magharibi Unguja.
Uamuzi wa kusimamishwa kwa kesi hiyo umetolewa na Naibu Mrajis wa Mahakama Kuu Ali Ameir Haji, wakati alipokuwa akitolea uamuzi juu ya suala hilo, lililosikilizwa Agosti 7 mwaka huu.
Katika maamuzi hayo Naibu Mrajis amesema kuwa, mahakama yake haioni sababu ya kuendelea na kesi hiyo, kutokana na kwamba upande wa serikali tayari umeshaunda Tume ya kuchunguza ajali iliyosababishwa na meli hiyo.
Amefahamisha kuwa anaamini kwamba mara baada ya Tume hiyo kukamilisha uchunguzi wake itaibua mambo mengi yatakayohitajika kuchukuliwa hatua kwa wahusika wake.
Akiyatilia mkazo maamuzi yake hayo, Naibu Mrajis asema kuwa jambo hilo si geni katika mahakama hiyo, kwani Mrajis wa Mahakama Kuu George Joseph Kazi tayari ameshawahi kuiondosha kwa muda kesi kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islanders I, ambayo inayofafana kimazingira na kesi hiyo.
Alisema kuwa, uamuzi huo umechukuliwa ni kutokana na mahakama hiyo kupewa baadhi ya mamlaka ya kisheria ya kutoa maamuzi kabla kesi hiyo haijafikishwa Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye uwezo wa kisheria wa kuisikiliza kesi hiyo.
Alifahamisha, kimsingi kesi zote za Mahakama Kuu kabla ya kufikishwa huko ni lazima zipitie mahakama za chini, ambazo kwa upande wake kuna baadhi ya mambo inaweza kuyatolea maamuzi ya kisheria.
Hivyo kutokana na hoja hizo, Naibu Mrajis huyo wa Mahakama Kuu amelazimika kuisimamisha kesi kuendelea mahakamani hapo kwa muda usiojulikana.
"Ijapokuwa kesi hiii imesimamishwa lakini bado ipo mahakamani, kwa wakati wote huo washitakiwa mtakuwa nje kwa dhamana na mtaitwa mahakamani mara mtakapohitajiwa", alifahamisha Naibu Mrajis.
Kusimamishwa kwa kesi hiyo, ni nafasi ya pekee kwa upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi wake ambao hadi hivi sasa bado haujakamilika, na pia ni fursa kwa Tume hiyo ya Uchunguzi kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.
Katika kikao kilichopita upande wa utetezi ulioongozwa na Wakili wa kujitegemea Abdallah Juma wa Kampuni ya AJM Solicitors & Advocate Chamber ya mjini Unguja, ameiomba mahakama hiyo kuisimamisha kwa muda kesi hiyo kutokana na serikali kuunda Tume ya uchunguzi pamoja na kuupa nafasi upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi wake.
Hoja hiyo ilipingwa na Mwanasheria wa serikali Sabra Mselem Khamis kwa madai kuwa Tume hiyo haihusiani kabisa na kesi hiyo iliyokuwepo mahakamani hapo, kwani washitakiwa wa kesi hiyo wameshitakiwa kwa kosa la kuua bila ya kukusudia.
Washitakiwa wa kesi hiyo kwa pamoja wameshitakiwa kwa kosa la kuua bila ya kukusudia kinyume na vifungu cha 195 na 198 vya kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Washitakiwa hao ni Kepteni wa Mv Skagit Mussa Makame Mussa (49) mkaazi wa Kazole, Said Abdulrahman Juma (46) wa Mwembetanga ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ya Seagull, pamoja na Meneja wake wa tawi la Dar es salaam Omar Hassan Nkonje (50) anayeishi Magomeni.
Wote hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 60 ya kuua watu waliokuwemo ndani ya meli hiyo, tukio ambalo lilitokea karibu na maeneo ya kisiwa cha Chumbe kilichopo wilaya ya Magharibi Unguja, tukio lililotokea majira ya saa 7:30 za mchana wa Julai 18 mwaka huu.
Katika maelezo yaliyotolewa mahakamani hapo ilifahamishwa kuwa, washitakiwa wote hao wakiwa na dhamana na majukumu ya kuchukuwa abiria na mizigo yao, kwa uzembe walishindwa kuchukua tahadhari katika majukumu yao pasi na kuzingatia usalama na kusababisha meli hiyo kuzama na kusababisha vifo vya abiria hao.
Washitakiwa wote wapo nje kwa dhamana ya fedha taslimu shilingi 5,000,000 pamoja na wadhamini wawili kila mmoja waliosaini bondi ya kima kama hicho cha fedha, na mmoja kati ya wadhamini hao ni mfanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

No comments:

Translate