tangazo

Tuesday, July 9, 2013

MJUKUU WA MANDELA AZUA TAFRANI JENGINE...ATAKA KUMSHTAKI WAKILI.

Mjukuu wa Mandela 

Johannesburg. Wakili wa mjukuu wa Mandela, Gary Jansen anatarajia kumfungulia mashtaka wakili wa familia ya Mandela kwa kuidanganya mahakama kuhusu afya ya Mandela.
Jansen alisema angefungua kesi hiyo jana ingawa hadi muda wa mahakama unakwisha alikuwa hajafungua shtaka lolote dhidi ya wanafamilia ya Mandela na wakili wao.
“Mteja wangu amejisikia vibaya, alipenda na anaheshimu matakwa ya babu yake na wala hakutaka haya mambo yawe hadharani hadi kwenye vyombo vya habari,” alisema Smith Wakili wa familia ya Mandela, David Smith ambaye anawasimamia binti mkubwa wa Mandela, Makaziwe, mke wa sasa Graca Machel na mke wa zamani, Winnie Madikizela Mandela aliiambia mahakama Juni 26, kupitia haki ya kiapo kuwa shujaa huyo wa Afrika, yu mahututi kiasi cha madakatri kushauri mashine ya kupumulia iondolewe.
Tuhuma za kuwa Mandela yupo mahututi na huenda akafariki wakati wowote, ilimsababisha hakimu kufanya uamuzi wa haraka ya kusikilizwa kwa kesi hiyo na hatimaye miili ya watoto watatu wa Mandela kufukuliwa kisha kuzikwa upya huko Qunu.
Hatua hiyo ya mahakama ilifanyika baada ya kuonekana kuwa Mandela aliwahi kutamka kuwa angependa kuzikwa katika eneo ambalo watoto wake wengine wamezikwa.
Gerald Bloem, Mwenyekiti wa Baraza la Mahakama ya Eastern Cape Bar alisema wachunguzi wanaweza kuwaita wanafamilia ya Mandela kutoa ushahidi kama mashauri ya kinidhamu dhidi ya wakili wa familia yataendelea.
Hata hivyo, Bloem alieleza kuwa wakili Smith huenda akakumbana na mkondo wa sheria iwapo itabainika kuwa aliidanganya mahakama kuhusu afya ya Mandela na atatakiwa kutoa ushahidi ambao madaktari watakosa pa kuupata.
Wanafamilia hao, walikataa kuzungumza lolote juu ya hatua za Jansen na mteja wake, Mandla zinazotarajiwa kuchukuliwa ingawa Denis Goldberg, rafiki wa karibu wa Mandela, alipomtembelea wiki iliyompita alithibitisha kuwa hakuwa mahututi na aliweza kunyanyua viungo vyake, sambamba na kutambua sauti.
Goldberg alizungumza na waandishi wa habari na kuthibitisha kuwa madaktari wamekataa Mandela asiondolewe mashine ya kupumulia kwani afya si mbaya hadi pale moja ya ogani zake itakaposhindwa kufanya kazi kabisa.
Wakati huo huo, Mandla amemcheka Mfalme wa Wazulu, AbaThembu, Buyelekhaya Dalindyebo ambaye alitangaza kumng’oa Uchifu, kuwa hana sifa za kufanya hivyo.
Dalindyebo alitangaza kumvua Uchifu Mandla kwa madai kuwa amepoteza heshima yake baada ya kuwa na mgogoro na wanafamilia wenzake kuhusu mabaki ya miili ya watoto watatu wa Mandela.
Mfalme huyo alisema Mandla hafai kuongoza watu wa Mvezo kwa kuwa ameipoteza heshima yake ambayo aliipata awali na kutawazwa kuwa chifu baada ya kulichafua jina la familia inayoheshimika ya Mandela.

Hata hivyo, Mandla aliikebehi kauli ya mfalme Dalindyebo akisema kuwa mfalme huyo hana msimamo na hekima.
Msemaji wa Mandla, Freddy Pilusa alisema kumfukuza Chifu kunahitaji mchakato mrefu na ushahidi wa makosa aliyoyafanya na si kuamka na kuamua kuwa unamfukuza Chifu.
“Huwezi tu kuamka siku moja na kuitisha mkutano na kufanya uamuzi kama huo,” alisema Pilusa.
Hata hivyo, msemaji wa nyumba ya kifalme, ya kabila la Abathembu, Nkos Daludumo Mtirara alisema: “Sisi tunaona kauli ya Dalindyebo kama utani tu, kwa sababu alikwishaondolewa kwenye cheo hicho miezi tisa iliyopita.
“Tunamtambua Mandla kuwa bado ni chifu kwa sababu, bado Serikali haijamuondoa Mandla katika cheo chake na anaendelea kupata haki na heshima yake kama kawaida.”
Mtirara alisema kauli ya Zwelibanzi ni ya kuharibu mila na tamaduni, kuchonganisha na kukuza jambo hili kwa sababu hata yeye hana mamlaka.
“Tunajua kuwa Zwelibanzi anavuta sana ‘Dagga’ na tunafahamu kuwa Zwelibanzi yupo katika operesheni ya kuivuruga familia ya Mandela” alisema Mtirara.

No comments:

Translate