tangazo

Thursday, January 17, 2013

Madaraka ya Rais yawagawa vigogo

Waziri Mkuu Mstaafu John Malecela akizungumza na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliokutana nao jana, ili kutoa maoni yake kuhusu Katiba Mpya. Kulia ni Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani na Mjumbe wa Tume Prof. Mwesiga Baregu.Picha ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba 

VIONGOZI waandamizi wastaafu wa Serikali, John Malecela, Frederick Sumaye na Barnabas Samatta wametofautiana kuhusu madaraka ya Rais yanavyostahili kuwa katika Katiba Mpya.
Katika maoni waliyotoa jana mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mawaziri Wakuu wastaafu, Malecela na Sumaye walitoa misimamo hiyo inayopingana kwa nyakati tofauti jana.

Wakati Malecela akitaka Katiba Mpya isiguse madaraka ya Rais kwa namna yoyote ile, Sumaye amependekeza viongozi anaowateua mkuu huyo wa nchi, wathibitishwe na vyombo vingine.

Msimamo wa Sumaye haukutofautiana sana na ule wa Jaji Mkuu mstaafu, Samatta ambaye amependekeza madaraka ya Rais yaangaliwe upya katika kipengele cha uteuzi wa viongozi wa umma na utaratibu wa kuwapata majaji.

“Napendekeza kwamba Katiba Mpya iangalie upya madaraka ya Rais katika uteuzi wa viongozi wa umma, lakini masuala mengine yanayomhusu Rais katika utendaji kazi wake yabaki kama yalivyo kuwa sasa,” alisema Jaji Samatta.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuwasilisha maoni yake kwa Tume ya Katiba, Jaji Samatta alisema anataka Katiba Mpya itazame upya madaraka ya Rais katika uteuzi wa viongozi wa umma ili kuwe na mgawanyo mzuri katika nafasi hizo.

Jaji Samatta alipendekeza pia utaratibu wa kuwapata majaji utazamwe upya na Katiba Mpya iseme kwamba mawaziri hawapaswi kuwa wabunge.

“Kama tunataka maendeleo katika Mhimili wa Mahakama ni vyema Katiba Mpya ikaweka utaratibu mpya wa kuwapata majaji. Napendekeza Katiba Mpya iweke utaratibu wa kuwapata majaji ili kuhakikisha tunaboresha upande wa Mahakama zetu.”
“Utaratibu huo utasaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha Mahakama zetu jambo ambalo litakuwa jema kwani zitafanya kazi kwa kiwango cha juu.”

Viongozi wabanwe
Jaji Samatta alisema Katiba Mpya ni vyema ikaunda chombo maalumu kitakachokuwa kinawabana viongozi wa umma ambao hawafanyi kazi zao ipasavyo.
Alisema chombo hicho kama kitatambulika kikatiba, kitasaidia kuondoa matatizo mbalimbali ya utendaji wa viongozi wa umma katika masuala ya maendeleo.

“Kumekuwa na malalamiko mengi ambayo yanawahusisha viongozi wa umma hasa kwa kutowajibika kwa wananchi, sasa ni vyema Katiba Mpya ikaunda chombo kitakachokuwa kinawabana viongozi wasiofanya kazi zao ipasavyo,” alisema.
Pia Jaji Samatta alipendekeza Katiba Mpya ikataze mawaziri kuwa wabunge ili kila mmoja afanye kazi zake ipasavyo.

Sumaye
Sumaye alitaka viongozi wanaoteuliwa na Rais wathibitishwe na vyombo vingine akitolea mfano uteuzi wa majaji na watumishi mbalimbali wa juu katika Serikali... “Rais anaweza kuwateua, lakini Bunge linaweza kushiriki kuwapitisha watu hao.”

Pia alipendekeza nafasi za wakuu wa wilaya ziendelee kuwepo lakini zisiwe za kisiasa.

Malecela
Akizungumzia madaraka ya Rais, Malecela alisema anawashangaa watu wanaotaka Rais apunguziwe madaraka na akapendekeza Katiba Mpya kumpa nguvu ili aendelee na madaraka aliyonayo sasa.

Alisema haoni kama kuna haja ya kumpunguzia Rais madaraka kwani tayari kuna mihimili mingine ya dola.

“Nawashangaa watu wanaotaka Rais apunguziwe madaraka. Mimi naona hakuna haja ya kufanya hivyo kwani tayari kuna mihimili mingine ya dola ambayo inafanya kazi zake kwa kujitegemea,” alisema Malecela na kuongeza:
“Wanaotaka Rais apunguziwe madaraka ni vyema wangetuambia ni madaraka gani hayo wanayotaka apunguziwe.” Alisema Rais ndiye anayewaunganisha wananchi.
Malecela pia amependekeza Katiba Mpya iweke mfumo mzuri wa kuwapata wabunge wanawake kupitia viti maalumu hadi kufikia asilimia 50 pamoja na kuwapo kwa mabunge mawili ili kuboresha utendaji kazi wa Serikali.

Kama alivyopendekeza Spika wa Bunge, Anne Makinda hivi karibuni, Malecela naye alisema ili kuhakikisha Serikali inafanya kazi yake vizuri, ni vyema Katiba Mpya ikaweka mfumo wa kuwa na mabunge mawili.

No comments:

Translate