tangazo

Wednesday, January 16, 2013

WANANCHI WAYAKIMBIA MAKAZI YAO MBEYA


IDADI kubwa ya wakazi wa Kijiji cha Karungu, mkoani Mbeya wameyakimbia makazi yao wakihofia kukamatwa na polisi kutokana na tukio la watu wawili kuzikwa wakiwa hai pamoja na maiti ya marehemu Nongwa Hussein katika tukio linalohusishwa na imani za kishirikina.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho kilichopo Kata ya Ivuna, Wilaya ya Momba, Credo Martin alisema jana kwamba wananchi wa kijiji hicho walianza kuyakimbia makazi yao Jumapili jioni baada ya polisi kufika kijijini hapo kuwasaka waliohusika na tukio la kuwazika wenzao wakiwa hai.

Waliozikwa hai ni Ernest Molela anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 60 na Bibi Mizinala Nachela ambaye umri wake unakadiriwa kuwa zaidi ya miaka 50, ambao walifanyiwa unyama huo kwa tuhuma kwamba walihusika na kifo cha marehemu Hussein.

Polisi waliofika kijijini Karungu walifukua kaburi hilo na kuwatoa Molela na Nachela wakiwa wamekwishafariki dunia na baada ya miili yao kufanyiwa uchunguzi ilikabidhiwa kwa ndugu na jamaa zao kwa ajili ya maziko yaliyofanyika juzi mchana.

Martin alisema licha ya kwamba hivi sasa hali ni tulivu, idadi kubwa ya wakazi wa kijiji hicho, hasa wanaume, hawapo kwani wamekimbia kukwepa msako wa polisi waliokuwa wakiwawinda watuhumiwa wa tukio la kuwafukia wenzao.

“Ukijaribu kuzunguka ni kama watu hawapo, wengi wao, hasa wanaume wamekimbia na ukienda kwenye nyumba zao unakuta watoto na kinamama tu, kuna habari kwamba wengine wameondoka kabisa na baadhi yao wanarejea usiku sana na kuondoka alfajiri kwenda mafichoni,” alisema Martin na kuongeza:

“Cha kushangaza ni kwamba hata pale kwenye msiba wa Nongwa, hakuna watu wengi wapo kinabibi tu, jambo ambalo siyo kawaida kwa sababu huku kwetu msiba huwa ni kama siku tatu na baada ya matanga watu wa mbali huondoka halafu wale wa karibu huondoka mmoja baada ya mwingine.”

Ofisa Mtendaj huyo wa Kijiji alisema baadhi ya watu walioyakimbia makazi yao walitajwa kushiriki katika uhalifu huo lakini wengine hawakutajwa na kwamba wamekuwa na hofu na taharuki kutokana na tukio hilo kutokuwa la kawaida.

Martin alisema siku ya tukio hilo, kundi la vijana waliokuwa na marungu, fimbo na mawe lilikuwa likizunguka kijijini hapo kuwasaka watu waliowatuhumu kuwa wachawi na kwamba ndiyo waliosababisha kifo cha Hussein.

Alisema kutokana na hali hiyo, baadhi ya watu waliondoka kwenye msiba na wale waliokuwa wametoka vijiji vya jirani waliondoka wakihofia kudhuriwa na vijana hao, hivyo mazishi yalifanywa na ndugu na jamaa wa karibu na kundi hilo pekee.

“Kwa ufupi ni kwamba hata walioshiriki mazishi ni ndugu tu wa karibu maana watu walikimbia kutokana na tafrani hiyo, hakuna ambaye aliweza kuwazuia kufanya kile walichokiamua maana mtu yeyote aliyejaribu kuonyesha kutokukubaliana nao walitishia kumdhuru,” alisema Martin.

Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ivuna, Joseph Silwimba alisema jana kwa simu kwamba idadi kubwa ya wanaume katika Kijiji cha Karungu wameyakimbia makazi yao wakihofia kukamatwa na polisi.

Vitendo hivyo viliambatana na tukio la kukamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi, Mwenyekiti wa Kitongoji, Alfred Kukwe ambaye alifungwa kamba miguuni na mikononi, kulazwa kifudifudi, kisha kumnyang’anya simu yake ya kiganjani ili asiweze kutoa taarifa kokote.

Jana, Silwimba alisema Kukwe alifikwa na mkasa huo alipofika katika eneo la msiba ambako alikwenda kupeleka jeneza la kumzikia Hussein ambalo alikwenda kulitengeneza kwa mafundi waliopo kijiji jirani cha Ivuna.

Kabla ya Molela na Nachela kuzikwa katika kaburi moja na marehemu, Silwimba alikaririwa juzi akisema kwamba kwa nyakati tofauti, walipigwa hadi kuzirai na vijana walioshiriki kuchimba kaburi hilo maalumu kwa ajili ya kumzika Hussein.

Silwimba alisema Hussein alifariki Dunia Jumamosi saa 10 jioni baada ya kuugua kwa muda mrefu, lakini ilionekana kuwa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walihusisha ugonjwa wake wa muda mrefu ambao ulisababisha kifo chake na ushirikina.

Jumapili kati ya saa 5.30 na saa 6 mchana, vijana hao walifanya uharibifu kwa kuchoma moto nyumba ya George Hussein ambaye ni kaka wa marehemu baada ya kumkosa nyumbani hapo, kwani naye alikuwa akituhumiwa kuhusika na kifo cha ndugu yake.

Alisema baada ya kufanya uharibifu huo, walikwenda nyumbani kwa Mzee Molela ambaye alipigwa hadi kuwa katika hali mbaya na waliporejea msibani walimkuta Nachela ambaye pia walimpiga hadi akazirai.

Silwimba alisema Molela na Nachela baada ya kupigwa, walivutwa hadi kwenye eneo la maziko ambako baada ya jeneza la marehemu Hussein kushushwa kaburini nao walitumbukizwa humo kisha kufukiwa wakiwa hai.

No comments:

Translate