MBUNGE wa Mkanyageni (CUF) Zanzibar, Habib Mnyaa amesema,
atawasilisha maombi ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara katika kikao cha kumi
cha Bunge kupinga gesi iliyogundulika mkoani humo kusafirishwa kwenda
Jijini Dar es Salaam.
Mnyaa akizungumza na wandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam alisema kwa muda sasa kumekuwapo na mjadala kutoka makundi mbalimbali kuhusu sakata hilo huku yakiwa hayajaonyesha ufumbuzi wa mgogoro huo.
Mnyaa ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha Wananchi (Cuf), alisema atatumia ibara ya 34 ya kanuni za Bunge kuwasilisha maombi hayo bungeni ili kupatiwa suluhisho.
Alisema Katibu wa Bunge amemtaka kuandaa maombi hayo kwa maandishi na lugha fasaha kisha aiwasilishe kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Mbunge huyo alisema amekwisha mwandikia barua Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kuhusu adhima hiyo ya kutaka wananchi wa Mtwara kupatiwa majibu kwa ufasaha.
“Madai ya wananchi wa Mtwara yana msingi kwani wanatakiwa kujua fidia kwa athari za kijamii, kiuchumi na kimazingira zinazoweza kujitokeza hasa kwa wananchi wanaoishi katika rasilimali hizo zinazovunwa,” alisema Mnyaa na kuongeza:
“Kitendo cha wananchi hao kuhoji na kutaka kuhakikishiwa ni kwa namna gani watafaidikia na fursa ya rasilimali ya gesi ni cha msingi ikizingatia kuwa mkoa huo ni moja ya mikoa ya pembezoni iliyosahaulika kimaendeleo kwa muda mrefu,” alisema.
Mbunge huyo alisema madai ya wananchi wa Mtwara yasitafsiriwe kwa mtazamo hasi na kinachotakiwa ni kuwaelimisha na kujua watakavyonufaika na rasiliamali hiyo.
Mapema wiki hii Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, alitoa tamko kutaka suluhu ya mgogoro wa gesi unaoendelea baina ya Serikali na wakazi wa mikoa ya Mtwara na Lindi kwa kuzitaka pande hizo kuacha kulumbana na badala yake wajiandae kukaa meza moja na kutafuta mwafaka kwa njia ya amani.
Rais Mkapa alisema anafedheheshwa na mgogoro huo huku akiwataka wananchi na wadau wa maendeleo Mkoa wa Mtwara, kusitisha harakati za maandamano na mihadhara.
“Fujo, vitisho, kupimana nguvu na malumbano siyo masharti ya maendeleo,” alisema Mkapa na kuongeza;
“Nikiwa kama mwana-Mtwara na Raia mwema mpenda nchi, nimefedheheshwa sana na matukio haya ya siku za karibuni Mtwara. Kwa sababu hiyo natoa wito kwa wadau wote wa maendeleo ya Mtwara, kusitisha harakati hizi na maandamano na mihadhara.”
Mkapa aliendelea kueleza katika tamko hilo kuwa “Badala yake wajipange
kukaa pamoja katika meza moja, kupitia historia,kutathimini mipango,
kuchambua kwa kina mikakati ya utekelezaji wake,hatimaye kufikia mwafaka
wa ujia wa maendeleo. Liwezekanalo leo lisingoje kesho.”
Chanzo na mwananchi
No comments:
Post a Comment