tangazo

Sunday, January 27, 2013

WAKAZI WA KIGAMBONI WAVAMIA AFISI YA WIZARA YA ARDHI


WAKAZI wa Kigamboni Dar es salaam, wamelalamikia usiri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi katika mchakato wa kupata Mamlaka ya Kuendeleza Mji wa Kigamboni (KDA) pamoja na ujenzi wa mji huo.

Malalamiko hayo yamekuja siku moja baada ya Waziri, Profesa Anna Tibaijuka kuanzisha KDA itakayoshughulikia usimamizi wa maendeleo ya ujenzi wa Mji mpya wa Kigamboni na kuufanya ujitegemee kutoka kwenye Manispaa ya Temeke.

KDA imeanzishwa chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali ya 1997, ili iweze kuhakikisha mji huo unajengwa na unakuwa bora.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti Dar es salaam jana, wananchi hao walisema wana hofu na hatma ya masilahi yao kutokana na mchakato wa ujenzi wa mji huo kufanywa kwa siri bila kushirikishwa katika hatua za awali.

Walisema hawaupingi uamuzi wa Serikali kujenga mji huo, lakini wanapinga kitendo cha serikali kutokufuata taratibu za ushirikishwaji wananchi hao ambao ndiyo wadau muhimu.

Mwenyekiti wa Mtaa wa, Feri Juma Mihambo alisema ujenzi wa mradi huo umekua ukisuasua tangu mwaka 2008,lakini walishtushwa na taarifa za kuanzishwa kwa KDA kutoka kwenye vyombo vya habari kuwa ndiyo chombo kitakachowasimamia.

“Serikali ishuke chini kwa wahusika halafu iwaeleze kwa kina kwa nini mradi umechelewa kwa takriban miaka minne na pia kwa nini imefanya usiri kuanzisha wakala ambaye atashirikiana nao bila wao kujua” alisisitiza Mihambo.

Naye Nassoro Chano alisema KDA isimamie mpango mji pekee na kuwaachia wananchi uhuru wa kukubaliana na wawekezaji katika masuala ya viwanja na mali nyingine.

“KDA ituachie jukumu la kuingia ubia na mwekezaji ili tupate masilahi stahiki na mwekezaji huyo atatakiwa kujenga kwa kufuata mipango na ramani iliyotolewa na wakala,” alisema Chano.

Ngoroka Ngoroka alisema serikali iwafuate wananchi hao na izungumze nao upya kwa kuyasikiliza mawazo yao juu ya kuendeleza mradi huo, lakini sio kwa utaratibu wa kuwafanya wapokeaji wa uamuzi kutoka ngazi za juu.

Titus Lugoe alisema serikali iache tabia ya kukurupuka na kuwalazimisha wananchi kuwa wapokeaji wa taarifa na maamuzi wakati nao ni wadau muhimu wa kufanikisha mipango ya serikali.

“Mwaka 2008 tulitangaziwa tusiendelee na ujenzi wa miradi yetu, lakini baada ya hapo hakuna kilichoendelea mpaka jana(juzi) tulivyosikia kwenye vyombo vya habari kuwa mradi unaendelea”

No comments:

Translate