MSICHANA wa jamii ya wafugaji wa Wamang’ati anayesoma kidato cha
pili Sekondari ya Tongani, Kata ya Mkaramo, wilayani Pangani, Mkoa wa
Tanga, ametoroka kwao na kukimbilia kwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni,
kuomba msaada kukwepa kufungishwa ndoa kwa nguvu.
Agnes Mhina (14), ambaye ni mkazi wa Mbugani
Kijiji cha Mkaramo, alilazimika kukimbia kwao kwenda kulala porini,
baada ya kulazimishwa kuacha shule ili aolewe.
Akizungumza eneo la ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Handeni jana, Mhina alisema tukio hilo lilitokea Ijumaa kijijini hapo.
Alisema aliamua kuchukua uamuzi huo mgumu na wa
kushangaza, baada ya kuona akifikisha suala hilo serikalini wilayani
ambayo amesikia ina mradi wa kukomboa wasichana, atasaidiwa ili amalize
masomo yake.
“Naishi kwa babu yangu, alitaka kuniozesha
mwanaume ambaye wala sijawahi kumuona, lakini nadhani naye ni Mang’ati.
Alitaka niache shule ili niolewe, nikamkatalia kwa vile nataka nisome,
alivyoona vile alitaka kunipiga,” alisema Mhina na kuongeza:
“Nilivyoona anataka kunipiga nikakimbilia porini
kujificha tangu saa 5:00 asubuhi hadi saa 10:00 usiku, nikapanda gari ya
kwenda Mkata, nilipofika huko nikapata gari nyingine iliyonifikisha kwa
Mkuu wa Wilaya. Lengo langu ni kuomba msaada serikali inisaidie nisome
au ikibidi niweze kufika kwa ndugu zangu Dodoma ili nisome.”
Binti huyo ambaye ni mmoja kati ya watoto wanne wa familia yao, ndiye pekee msomi.
Alisema babu yake alihamia katika eneo hilo tangu
mwaka 2006, akitokea mkoani Dodoma, akiwa na mifugo yake kwa nia ya
kutafuta malisho.
“Sijui mwenyewe alitaka kupewa mahari kiasi gani,
maana kuna aina mbili ya mahari katika kabila letu. Kuna ng’ombe watatu
na debe tatu za asali, nyingine ni ng’ombe saba, labda alitaka apate
mali,” alisema Juma na kuongeza:
“Pia, huku nimesikia serikali inawasaidia wasichana ili wasome kwa kuvunja ndoa za wanafunzi.”
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya
Handeni, Muhingo Rweyemamu alisema anaona faraja kubwa na mafanikio
makubwa kwa Mradi wa ‘Niache Nisome’.
Mradi huo ulianzishwa kumkomboa mtoto wa kike katika mimba na ndoa za utotoni wilayani hapa.
“Huyu mtoto amenishangaza sana, ameonyesha ujasiri wa ajabu kwenda kulala porini ni jambo la ujasiri wa hali ya juu. Pia, nimeshangaa kwa mabinti sasa kutambua kwamba Serikali yao inawajali katika elimu kwa kuwatetea ili wafikie malengo yao,” alisema Rweyemamu.
“Huyu mtoto amenishangaza sana, ameonyesha ujasiri wa ajabu kwenda kulala porini ni jambo la ujasiri wa hali ya juu. Pia, nimeshangaa kwa mabinti sasa kutambua kwamba Serikali yao inawajali katika elimu kwa kuwatetea ili wafikie malengo yao,” alisema Rweyemamu.
No comments:
Post a Comment