KUTOKANA vurugu zilizotokea juzi mjini hapa kati ya wafuasi wa
Chadema na wale wa CCM, uongozi wa Chadema Wilaya ya Dodoma umepanga
kumburuta mahakamani Mbunge wa Tabora mjini, Ismail Aden Rage.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Katibu wa Chadema wilaya hiyo, Jella Mambo, wafuasi wawili wa Chadema wamefungua jalada la kesi hiyo na huenda leo akafikishwa mahakamani.
Mambo alisema kuwa wafuasi hao waliamua kumfungulia kesi mbunge huyo kutokana kuhusika moja kwa moja kuwapiga pale walipokuwa wamekamatwa na wakereketwa wa CCM.
Mbali na Rage, mwingine atakayehusishwa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma Mjini, Shaaban Bwanga.Waliofungua jalada hilo ni Idd Kizota ambaye anawalalamikia Bwanga na Rage kwa kumpiga ilihali Anord Swai akimlalamikia Rage kuwa ndiye aliyempiga.
Juzi kulizuka vurugu katika eneo la Mji Mpya karibu na zilipo Ofisi za Chadema na kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa huku baadhi wakiripotiwa kukamatwa na polisi.
Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, Mbunge wa Tabora Ismail Rage alipokea simu na kumwambia mwandishi wa habari amtafute baadaye kwani alikuwa katika shughuli zingine.
Baadaye mbunge huyo simu yake ya mkononi iliita bila kuwa na majibu na hata alipotumiwa ujumbe wa mkononi hakuweza kujibu.
Akizungumzia suala hilo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alikanusha wabunge wa CCM kuhusika na vurugu hizo na akasema kuwa kilichotokea ni kuwa wabunge hao walikuwa na kazi ya kuamua ugomvi.
“Pale kama wasingekuwapo wabunge hali ingekuwa mbaya sana na yule kijana angeumizwa, kwani uwapo wao ulisaidia katika kuamua ugomvi ule,” alisema Ndugai.
Kamanda wa Polisi David Misime hakupatikana kuthibitisha tukio hilo baada ya wasaidizi wake kueleza kuwa alikuwa katika msiba wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma waliyemtaja kwa jina la Urio.
No comments:
Post a Comment