tangazo

Sunday, February 3, 2013

MBUNGE WA MTWARA MJINI MATATANI.



Mbunge wa Mtwara mjini, Hasnain Murji  
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mtwara kimedai kauli zilizotolewa na mbunge wake jimbo la Mtwara mjini, Hasnain Murji kuungana na wananchi wanaoshinikiza gesi kutotoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam, ni sawa na kukihujumu chama.
Akizungumza na gazeti hili jana Katibu wa CCM mkoani humo, Alhaji Masoud Mbengula alisema chama kilishangazwa na kauli za mbunge huyo, kwa mba alionekana wazi kuwaunga mkono wapinzani na siyo wananchi.
“Tayari tumemwita katika vikao na kumhoji kuhusiana na kauli alizozitoa, pia taarifa rasmi zipo na tumezipeleka makao makuu ya chama ambapo ndiyo watatoa uamuzi,” alisema Mbengula na kuongeza;
“Tumesikitishwa sana na kauli ya Murji. Kauli yake ilionekana kuwaunga mkono wapinzani kwa kuwa msimamo na nia yao ni kuona Ilani ya CCM haitekelezwi. Kama alikuwa na hoja alitakiwa kutafuta njia za kusema na siyo kuzungumza jambo hilo hadharani. Kwa namna moja au nyingine yeye amechangia kukihujumu chama.”
Wakati katibu huyo akieleza hayo, Desemba 29 mwaka jana baada ya Murji kutoonekana kwenye maandamano ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara ya kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam yaliyofanyika Desemba 27, aliibuka na kusema anaunga mkono wananchi hao kutetea maslahi yao.
Alisema hoja ya msingi ni kujadili kwa namna gani bomba la gesi litanufaisha Wanamtwara, kufafanua kuwa kwa kiasi fulani hakubaliani na hoja ya gesi isiende Dar es Salaam lakini naungana na wananchi kudai jinsi watakavyonufaika na gesi hiyo.
Alisema anakubalina na gesi iende Dar es Salaam kwa sharti la kuzalisha umeme, si kwa matumizi mengine, kwamba wakianza kuitumia kwenye viwanda watakuwa wameiua Mtwara kabisa, huku akiunga mkono wana nchi kuandamana kwa maaelezo kuwa ni haki yao ya msingi na hawapaswi kubezwa na mtu yeyote kwa sababu wanateteta haki yao ya msingi ya kufaidika na rasilimali yao.
Katika maelezo yake Mbengula alisema chama hicho kilihujumiwa huku akitoa mfano wa matukio ya kuchoma moto nyumba. Nyumba hizo nyingi zilikuwa za viongozi wa CCM wakiwamo wabunge pamoja na ofisi, hasa zipo zilizochomwa wilayani Masasi mkoani humo.
“Nyumba zilizochomwa moto zote ni za viongozi na wabunge wa CCM. Mpango huu ulionekana kupangwa na kuratibiwa na watu fulani kwa lengo la kukihujumu chama” alisema Mbengula.
Murji
Mwananchi Jumapili jana lilizungumza na Murji ambapo pamoja na mambo mengine alisema kuwa kauli alizozitoa nazo ziliungwa mkono na CCM.
“Hata siku moja zikuwahi ku pinga gesi kwenda Dar es Salaam.Lengo langu ni kutaka wananchi wafaidike kwanza na gesi, watu walitaka kujua watanufaika vipi na si vinginevyo,” alisema Murji na kuongeza;
“Hata katika ufafanuzi alioutoa Waziri Mkuu alieleza jambo hilo, hata CCM waliungana na mimi kutaka gesi iwanufaishe wakazi wa Mtwara.”
Alisema kuwa kwa sasa hali imekuwa shwari mkoani humo, huku akiwataka wananchi kuwa watulivu, kwani tayari Serikali imeshaeleza msimamo wake na jinsi itakavyotekeleza mradi huo.
Akizungumzia kauli za mbunge huyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema, “Taarifa rasmi za Murji bado hatujazipata, lakini inawezekana zikawa zimefika makao makuu kwa kuwa hivi sasa pale ofisini Sekretarieti yote ipo mkoani Kigoma katika sherehe za miaka 36 ya chama.”
Alifafanua kwamba taarifa za mbunge kwanza zinajadiliwa na wilaya na mkoa, baadaye kupelekwa taifa, kusisitiza kuwa huenda zikawa zimeshafika.
CUF wahusishwa na vurugu
Katika hatua nyingine Mbengula alikirushia lawama CUF kwamba kinahusika na vurugu zilizotokea mkoani humo. “Mfano mzuri ni matukio yaliyotokea Masasi, CUF walikodi watu kwa ajili ya kuihujumu CCM , watu hao waliharibu nyumba za wabunge wawili wa chama na ofisi ya chama wila yani humo”alisema Mbengula.
Alisema lengo la CUF ni kuona watu wote wanaunga mkono maandamano ya kupinga gesi kwenda Dar es Salaam.
“Watu waliotumiwa na CUF kufanya vurugu walitokea wilaya ya Tandahimba, hata waliokamatwa walisema wanatokea huko, walipelekwa Masasi kwa magari na kujaziwa mafuta” alisema na kuongeza;
“Gesi ilikuwa ni kisingizio tu, wao walikuwa na malengo ya kisiasa.”
Katibu huyo wa CCM mkoa aliwataka wananchi kuwa watulivu na kusubiri utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Serikali zitatekelzwa.
Alisema kwa kiasi kikubwa vurugu hizo ziliibuka kutokana na wananchi kutokuwa na elimu kuhusu gesi, huku akifafanua kuwa kuna wananchi ambao walilipwa fidia kutokana na mradi huo, lakini baadhi ya wananchi waliposikia kuwa bomba linatandazwa kwenda Dar es Salaam ndiyo wakaanza kupinga mradi huo.
Akizungumzia kauli kwamba CCM haina chake baada ya vurugu hizo, alisema kuwa hilo haliwezekani kwa kuwa tangu zimetokea vurugu hizo hakuna hata mwanachama mmoja aliyerudisha kadi.
“CCM bado itaendelea ku shinda hata kama uchaguzi utafanyika kesho, ila kwa sasa tunachotakiwa kufanya ni kuwarudisha wanachama kuwa kitu kimoja kwa sababu waligawanyika. Hivyo tunatakiwa kuwarudisha ili waendelee kuiamini Serikali yao” alisema.
Akijibu tuhuma hizo Naibu Katibu Mkuu wa CUF taifa, Julius Mtatiro alisema kuwa CCM iache kutafuta mchawi na kuitaka kutekeleza Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2010, ambapo kiliahidi kuwa Mikoa ya Lindi na Mtwara itaunganishwa katika gridi ya taifa.
“Watanzania wanadai haki zao, hizo kauli wanazozitoa CCM ni za kikorofi tu. Wanatakiwa kutekeleza ahadi walizozitoa katika Ilani yao ya Uchaguzi ya mwaka 2010 na si vinginevyo” alisema Mtatiro.
Akizungumzia tuhuma kuwa CUF ndiyo chanzo cha vurugu hizo alisema kuwa jambo hilo siyo la kweli kwa kuwa hata katika mikutano yao iliyofanyika mkoani humo, hakuna hata kiongozi mmoja aliyewataka wananchi kufanya vurugu.
“Kama wana ushahidi waseme, ila sisi tuna mikanda yetu ya video na hata siku moja hatujawahi kutoa kauli za uchochezi wala vurugu, hicho kilichosemwa na CCM siyo cha kweli” alisisitiza.
Wakati hayo yakiendelea, Mbunge wa Mtwara Vijijini na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI), Hawa Ghasia amesema ana mwachia Mungu wote waliohusika kuteketeza nyumba yake kwa moto katika vurugu za hivi karibuni mkoani Mtwara.
Akizungumza kwenye Viwanja vya Bunge Mjini Dodoma juzi baada ya kipindi cha maswali na majibu, alisema: “Wamenichomea kila kitu, kwa kweli imeniuma sana, lakini nitasema nini, yote namwachia Mungu.”
Ghasia pamoja na viongozi wengine akiwamo Anna Abdallah (Mbunge Viti Maalumu Mtwara), alichomewa nyumba yake pamoja na nyumba ya Diwani wa Kata ya Chikongola kuharibiwa kwa kupigwa mawe, huku jengo la Ofisi ya Kata ya Ufukoni lilichomwa moto na nyaraka mbalimbali kuunguzwa.
Akizungumza huku akionyesha uso wa huzuni, Ghasia alisema kuwa amefarijika kuwa Serikali inawajengea upya nyumba zao, lakini akasema kwa upande mwingine imewarudisha nyuma katika mipango yao.
Ghasia alisema pia kwamba uharibifu huo umeisababishia Halmashauri ya Mtwara (Masasi) pekee hasara ya takriban Sh1.5 bilioni kwa hesabu za haraka walizoziwasilisha katika ofisi yake.
Hata hivyo, alimpongeza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa jitihada mbalimbali alizochukua pamoja na watu wengine kuhakikisha amani Mtwara inakuwepo, huku akiwataka viongozi wa kisiasa kutotumia suala la gesi ya Mtwara kutimiza matakwa yao ya kisiasa.
Katika vurugu hizo Mahakama ya Mwanzo ya Mjini Mtwara pia ilichomwa moto na kuteketeza nyaraka mbalimbali. Nyumba ya askari mmoja katika eneo la Sabasaba, duka la Diwani wa Kata ya Ufukoni nazo zilitekete zwa kwa moto.
Katika vurugu nyingine, wilayani Masasi ulifanyika uharibifu mkubwa wa mali za Serikali, viongozi na raia ikiwamo kuchomwa moto kwa nyumba ya mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kasembe, ofisi za ununuzi Halmashauri ya Masasi,   ofisi ya elimu ya Msingi na nyaraka zote.
Pia Ofisi ya Ukaguzi wa Shule na TSD na nyaraka zote ziliunguzwa kama ilivyokuwa kwa Ofisi ya Maliasili na nyaraka zote, kuharibiwa kwa baadhi ya Ofisi za Halmashauri ya  Wilaya ya Masasi kwa kuchomwa moto na kuteketea kabisa kwa magari 11 ya Halmashauri yakiwamo sita ya Serikali na ya watu binafsi.
Kati ya magari ya Serikali yaliyochomwa moto yako magari mawili ya wagonjwa, pikipiki nne na baiskeli moja, pamoja na kuharibiwa kwa vifaa mbalimbali vya Ofisi za Halmashauri.
Vilevile, kuvunjwa kwa geti kuu la kuingilia Halmashauri, kuondolewa kwa uzio wa mabati katika jengo linalojengwa na Halmashauri, kuunguzwa kwa chumba cha kutunzia nyaraka na vitu vyenye thamani ya Idara ya Maliasili, kuteketea kwa bunduki moja na kuunguzwa kwa shehena ya mbao, zilizokuwa zimekamatwa na Halmashauri.

No comments:

Translate