tangazo

Thursday, November 8, 2012

Rais Jakaya Kikwete atuma salamu za rambirambi kwa Kanisa Katoliki Tanzania Kufwatia kifo cha Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Mhashamu Baba Askofu Aloysius Balina

Rais Jakaya Kikwete
----
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Novemba 2012, amelitumia Kanisa Katoliki Tanzania salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Mhashamu Baba Askofu Aloysius Balina aliyefariki dunia majira ya saa tano asubuhi kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania Mshahamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Mhashamu Baba Askofu Aloysius Balina ambaye nimeambiwa ameaga dunia asubuhi ya leo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Buganda, Mwanza, kwa ugonjwa wa kansa.”
Amesema Rais Kikwete katika salamu zake hizo: “Mhashamu Baba Askofu Balina alikuwa kiongozi hodari na mwadilifu ambaye siyo tu alichangia kipekee katika mwenendo mzuri wa kiroho wa waumini wa Kanisa Katoliki bali pia katika maendeleo ya Watanzania wote kwa jumla.”
“Kifo chake kimetuondolea kiongozi mwema ambaye tutazikosa busara zake na uongozi wake. Lakini napenda kukuhakishia Mshahamu Baba Askofu kuwa sisi ndani ya Serikali tutaendelea kutambua na kuthamini mchango wa Askofu Balina alioutoa kwa nchi yetu katika maisha yake,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Baba Askofu, nakuomba upokee salamu za rambirambi za Serikali ninayoiongoza na zangu binafsi kufuatia msiba huu mkubwa. Aidha, kupitia kwako, naomba uwafikishie salamu zangu viongozi na waumini wote wa Kanisa Katoliki kwa kuondokewa na kiongozi na muumini mwenzao. Naungana nanyi kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweka pema peponi roho ya Marehemu. Amen.”

No comments:

Translate