tangazo

Saturday, November 10, 2012

UTATA WAZUKA KUHUSU THAMANI YA MENO YA TEMBO


UTATA waghubika katika thamani halisi  ya meno ya Tembo yaliyokamatwa yakiwa yamefunikwa na Bendera ya Taifa  katika eneo la Kimara  Stop Over Kinondoni jiji Dar es Salaam, baada ya hati ya mashtaka kutofautiana thamani na  taarifa ya polisi kwa kiwango kikubwa.

Hali hiyo ilijitokeza jana baada  ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Hamidu Mwanga kusoma hati ya mashtaka jana  mbele ya Hakimu Mkazi, Stuart Sanga iliyotaja  meno hayo kuwa na thamani ya Sh438,971,400, huku  taarifa ya awali  iliyotolewa na Kamanda wa Polisi  wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova  ilisema thamani halisi ya meno hayo ya Tembo ni  Sh2.1 bilioni.

Kamanda Kova katika taarifa yake,  alisema baada ya kukamata nyara hizo za Serikali wataalamu wa maliasili walifanya majumuisho na kubaini kuwa yalitokana na idadi ya tembo 91 waliouawa.

Akisoma hati ya mashtaka katika Mahakama ya Kisutu, Wakili Kweka aliwataja washtakiwa waliokamatwa na pembe hizo  kuwa ni Peter  Kabi (41), Leonida  Kabi (42), Charles Wainaina (41) na Polisi Malisa (42).

Kweka alidai kuwa  Oktoba 27, mwaka huu huko Kimara  washtakiwa hao kwa pamoja  walikamatwa wakiwa na kilogramu 210 za vipande vya meno ya Tembo yenye thamani ya dola za Kimarekani 217,830,000 ambapo wakati yanakamatwa yalikuwa na thamani ya Sh 391,571,400.

Pamoja na mifupa ya Tembo  mitano  yenye thamani ya dola za Kimarekani 30,000 ambapo wakati zinakamatwa zilikuwa na thamani ya Sh47,400,000 yote yakiwa na jumla ya thamani ya Sh 438,971,400 mali ya Serikali ya Jamuhuri ya Tanzania bila kuwa na kibali.

Mbali na shtaka hilo, mshtakiwa Wainaina  na Malisa  wanadaiwa kuwa Oktoba 27, mwaka huu  katika Kituo cha Polisi cha Mbezi ya Kimara  wakiwa wanajua kuwa Leonida alikamatwa na nyara za Serikali , walifanya jaribio la kumshawishi polisi ili aweze kumsaidia kuepukana na adhabu.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa  upelelezi bado haujakamilika.

Hakimu Sanga alisema anahirisha kesi hiyo hadi Novemba 15, mwaka huu ambapo atatoa masharti ya dhamana.

Katika taarifa ya jeshi la Polisi watuhumiwa hao wanne waliohusika na uhalifu huo, walikamatwa  baada ya kupokea taarifa kutoka kwa raia wema na kwamba  Nyara hizo zilikutwa ndani ya nyumba ya Peter Kami, ambaye ni raia wa Kenya anayeishi na mwanamke ambaye ni Mtanzania, Leonida Kabi.

Kova alisema anawashukuru raia wema wanaoendelea kushirikiana nao kupambana na uhalifu na aliwaomba waendelee hivyo hivyo, ‘maana hata kukamatwa kwa watu hawa wao ndio wamefanikisha’ Idadi ya meno hayo ni 214 na yalikuwa katika viroba 12 licha ya meno hayo pia kulikutwa pembe za ng’ombe 10 zikiwa zimeshindiliwa chokaa na mifupa mitano ya tembo.

Kwa mujibu wa wataalamu wa maliasili katika kubaini idadi ya tembo waliouawa walitumia utaalamu wao kwa kufanya majumuisho ya kitaalamu ya meno na mifupa hiyo na kugundua kuwa jumla yake ni kilo 450.6 ambazo ni sawa na tembo 91.

No comments:

Translate