tangazo

Saturday, November 10, 2012

WAKUU WA KUNDI LA UAMSHO WABADILISHIWA MASHTAKA

Sehemu ya umati wa wafuasi wa kikundi cha Uamsho Zanzibar wakiwa katika moja ya mikutano yake ya kuhamasisha kile wanachokiita 'uhuru wa nchi yao'. 

VIONGOZI wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar,
wamefikishwa tena mahakamani na kubadilishiwa shtaka la uvunjifu wa amani chini ya kifungu cha 3 (d) cha sheria za Usalama wa Taifa.  
 
Washtakiwa hao ni pamoja na kiongozi wa jumuiya hiyo, Sheikh Farid Hadi Ahmed (41), Mselem Ali Mselem (52), Mussa Juma Issa (37)  na Azzan Khalid Hamdani (48).

Wengine ni Suleiman Juma Suleiman (66), Khamis Ali Suleiman (59), Hassan Bakari Suleiman (39) na Ghalib Ahmada Omar (39).

Kwa pamoja watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya uvunjifu wa amani, ushawishi wa kuchochea na kurubuni watu, kula njama pamoja na kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani kosa ambalo  linamkabili Azzan Khalid Hamdani pekee yake.

Watuhumiwa hao waliofikishwa mahakamani hapo jana chini ya ulinzi mkali wa polisi walisomewa mashtaka ya uvunjifu wa amani chini ya kifungu cha 3 (d) cha sheria za Usalama wa Taifa sura ya 47 sheria ya mwaka 2002, kwa kuhusishwa na matukio yaliyotokea Oktoba 17 na 18 mwaka huu.

Upande wa mashtaka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, ukiongozwa na Ramadhan Nasseeb ulidai kuwa watuhumiwa kwa pamoja wanadaiwa kuharibu barabara, majengo, vyombo vya moto ikiwemo na pikipiki na magari na wakufanya hivyo bila ya kuwepo sababu za msingi za kuharibu na kuteketeza kinyume cha maslahi ya umma na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi milioni tano.

Katika shtaka la pili washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Mei 26 hadi Oktoba 19, 2010 walishawishi na kufanya uchochezi kwa kufanya mikutano katika maeneo tofauti yakiwemo Lumumba, Msumbiji, Fuoni Meli sita na Mbuyuni ambayo kwa nyakati tofauti walishawisi na kuchochea watu kufanya makosa.

Alidai kuwa makosa washtakiwa waliweka vizuizi barabarani kwa kutumia mawe,, makontena ya kuhifadhia taka, matawi ya miti, mapipa ya mafuta, kuchoma magurudumu ya magari, kuharibu majengo tofauti, magari na kusababisha huduma muhimu za jamii za Serikali kusimamisha na watu kushindwa kufanya shughuli zake.

Pia watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kula njama na kusababisha Sheikh Farid Hadi Ahmed kujificha katika sehemu isiyojukana na kupelekea uvunjifu wa amani katika jamii kwa siku kadhaa.

Shtaka la nne ambalo linamkabili Sheikh Azzan Khalid peke yake ni kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani, pamoja na kumtolea maneno ya kashfa na matusi Kamshna wa Polisi wa Zanzibar.

Hata hivo, watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.

Mawakili walalamika wateja wao kunyolewa ndevu
Katika hatua nyingine, Mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao wamelalamikia kitendo cha Serikali kukiuka haki za binaadamu na utaratibu mzima wa kisheria wa uendeshaji wa mashtaka dhidi ya wateja wao.

Watuhumiwa hao wanatetewa na Mawakili wa Abdallah Juma, Suleiman Salum pamoja na Salim Tawfik.

Tawfik alidai  mahakamani hapo kuwa wateja wao tangu wakamatwe siku 17 zilizopita wamekuwa hawatendewi haki ikiwa pamoja na kunyimwa fursa zote wanazostahiki kupata kama watuhumiwa.

Wakili huyo alitoa mfano wa uvunjwaji wa haki hizo kuwa ni pamoja na wateja wao kushindwa kubadili nguo ambapo tangu walipokamatwa hawajaruhusiwa kubadilisha, kulazimishwa kunyolewa ndevu, kukatazwa kuonana na jamaa zao, pamoja na kutengwa kila mmoja katika chumba maalumu chini ya ulinzi mkali.

Mambo mengine ambayo yalalamikiwa ni  kulazwa chini ya sakafu, kujisaidia ndani ya ndoo, kunyimwa fursa ya kufanya ibada jambo ambalo linakwenda kinyume na Katiba kuhusu haki ya kuabudu na kufungiwa ndani ya vyumba saa 24.

Wakinukuu baadhi ya vifungu vya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1988, inayotoa fursa ya watu wote kuwa sawa mbele ya sheria, haki ya kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria, Mawakili hao wamedai kuwa wateja wao wamekuwa wakikosa haki hizo na kutendewa tafauti na watuhumiwa wengine waliopo rumande.

"Haki za washtakiwa hawa zinavunjwa wazi wazi na maofisa wa Vyuo vya Mafunzo na serikali kwa ujumla, hawa raia kama wengine wanapaswa kupatiwa haki zao zote za msingi wanazostahiki kwani hapo ni watuhumiwa lakini wanafanywa kama wameshatiwa hatiani Mheshimiwa."

Wakili Tawfik aliiomba mahakama pamoja na Serikali kuacha kuvunja sheria na haki za watuhumiwa hao kwa sababu ni miongoni mwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu na mahakama haipaswi kunyamazia ukiukwaji huo unaotendeka dhidi ya watuhumiwa.

"Mheshimiwa wateja wetu hawana fursa ya kusali sala ya Ijumaa na wenzao, hawana vitabu vya dini wakati tunafahamu hawa ni viongozi wa dini, hata ndevu wamenyolewa ili kuwadhalilisha na wamefanyiwa kwa makusudi ili kuwavunjia heshima zao katika jamii wakati ni kinyume na katiba kwani kama tunavyofahamu kufuga ndevu kwa muislamu ni sunna na ni ibada lakini kumnyoa ndevu ni sawa na mkristo kumvua msalaba."

Akijibu malalamiko hayo upande wa mashtaka walionekana kutorishika na tuhuma hizo za kukiuka haki za watuhumiwa na kutaka upande wa utetezi wa watuhumiwa kufungua kesi ya madai kupinga hayo kwa sababu kesi dhidi ya watuhumiwa ni kesi ya jinai.

“Sisi kama ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), hatupendelei kuona haki haitendeki pamoja na ukiukwaji wa haki za binaadamu unaodaiwa hapa sisi ni wajibu wetu kuhakikisha vyombo vya sheria vinavyohusika vinatekeleza sheria na kufuata katiba lakini pamoja na hilo naomba mahakama malalamiko haya yanayotolewa na upande wa utetezi kuwasilisha hoja zao hizi katika mahakama husika kwa vile hoja zao hizo zimegusia ukiukwaji wa Katiba na hii ni kosa ya jinai sasa wamefungue kosa ya madai.”

Hata hivyo jopo la wanasheria wa Serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), wakiongozwa na Rashid Fadhil lilidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo kuiomba mahakama kuhairisha shauri hilo na kulipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa ili iweze kupatikana muda wa ziada wa kuendelea na upelelezi huo.

Hakimu George Kazi baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alisema kuwa atatoa uamuzi wa malalamiko hayo Novemba 20 siku ambayo imepangwa kutajwa kesi hiyo.

No comments:

Translate