tangazo

Friday, November 30, 2012

WANANCHI WA WILAYA YA GEITA WATAKA MAFISADI WANYONGWE HADI KUFA.


WANANCHI wa Wilaya ya Geita mkoani Geita wamesema ili kurudisha ari ya viongozi kutumikia umma, wale viongozi watakaokumbwa na kashfa za rushwa ama ufisadi wapewe adhabu kali ikiwa ni pamoja na kunyongwa hadi kufa.

Wakitoa maoni yao kwa ajili ya uundwaji wa Katiba Mpya, baadhi ya wakazi hao kwa nyakati tofauti walisema kwamba tatizo la rushwa na ufisadi limekuwa ni jambo la kawaida kiasi cha kuathiri maendeleo ya nchi na hivyo kuitaka Katiba Mpya kubainisha adhabu ya wala rushwa kuwa ni kunyongwa hadi kufa.

Akitoa maoni yake Elisha Ngeleja alieleza kwamba ili kukomesha rushwa nchini, ipo haja ya Katiba ijayo kubainisha kuwa adhabu ya wala rushwa wote watoaji na wapokeaji pale wanapopatikana na hatia, iwe ni kunyongwa.

“Hatua zinazochukuliwa sasa hazijasaidia tatizo linazidi kukua kila siku, rushwa inaongezeka, ili kukomesha katiba inapaswa kutamka bayana kwamba kila anayepatikana na hatia ya kula rushwa anyongwe hadi kufa,” alieleza.

Sylvester Mwanole yeye alipendekeza katiba ijayo inapaswa kubainisha wazi kuwa wanaohujumu mali za umma wafungwe kifungo cha maisha pale wanapopatikana kuwa na hatia.

Alisema tatizo la kuhujumu mali za umma linazidi kuongezeka kila uchao hii ni kutokana na kutokuwa na adhabu kali kwa wanaohujumu na hivyo kubainisha wafungwe kifungo cha maisha.

Naye Mary Mrungu akitoa maoni yake alipendekeza katika Katiba Mpya ufisadi ubainishwe kama kosa kubwa sawa na kosa la kuuwa na adhabu yake iwe kali kwani itasaidia kuwafaanya viongozi waliopewa dhama ya kuongoza nchi kuogopa.

No comments:

Translate