Na: Raymond Kaminyoge Dar na Joseph Lyimo, Simanjiro
WAKATI Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), likihaha kumtafuta
aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akiwa
amevaa sare za jeshi hilo, mtu huyo ameibuka na kusema yuko tayari
kufukuzwa kazi kuliko kuacha kuishabikia Chadema.
Kauli hiyo ya JWTZ imekuja baada ya jana,
gazeti hili kuchapisha picha ya mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni
askari wa JWTZ akiwa amepiga picha na Lema pamoja na Mbunge wa Arumeru
Mashariki, Joshua Nassari, huku akiwa amenyoosha vidole viwili alama
inayotumiwa na Chadema.
Baada ya taarifa hiyo, JWTZ lilitoa taarifa
likieleza kushtushwa na tukio hilo na kusema kwamba linamtafuta mtu
huyo kwa udi na uvumba ili kujiridhisha kama kweli ni askari wake.
‘‘Kimsingi Jeshi linafanya uchunguzi wa kumtambua
mtu huyo kama kweli ni askari,’’ ilisema sehemu ya taarifa ya Kurugenzi
ya Habari na Uhusiano ya jeshi hilo ambayo iliyatilia shaka mavazi
aliyokuwa amevaa mtu huyo kama ndiyo yanayotumiwa na jeshi hilo sasa.
Taarifa hiyo ya JWTZ, ilisema ingekuwa rahisi kumtambua mtu huyo kwa kuangalia paji la uso lakini alilifunika ili asitambulike.
‘‘Pamoja na hayo, jeshi linamtafuta ili
kumchukulia hatua za kinidhamu kutokana Kanuni za Majeshi ya Ulinzi
likisema Sheria namba Nne ya Mabadiliko ya Nane katika Katiba ya Nchi ya
mwaka 1992, Ibara ya 147(3), mwanajeshi yeyote hatakiwi kujihusisha na
masuala ya kisiasa,’’ ilisema taarifa hiyo.
Mbali ya taarifa hiyo, Msemaji wa JWTZ,
Kanali Kapambala Mgawe alisema endapo itabainika kuwa aliyevaa sare hizo
ni mwanajeshi, moja ya hatua dhidi yake ni kufukuzwa kazi mara moja.
Mbali na hatua hiyo, Kanali Mgawe alisema
kuanzia sasa, Jeshi limepiga marufuku mtu yeyote kuvaa sare zake katika
mikutano yote ya siasa na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za
kinidhamu.
Kuhusu kitendo cha askari huyo kupiga picha na
Lema, Kanali Mgawe alisema moja ya masharti muhimu ya askari
anapiojiunga na jeshi ni kutambua na kutii sheria inayomzuia kujihusisha
na masuala ya siasa na kwamba kitendo cha mtu huyo kimemshangaza na
kumfanya amtilie shaka kama kweli ni askari aliyekamilika.
Msimamo wa mtuhumiwa
Kwa upande wake, mtu huyo aliyejitambulisha kuwa
ni askari wa Kikosi cha Chuo cha Mafunzo Monduli (TMA), mkoani Arusha,
alisema ni bora afukuzwe kazi kuliko kunyimwa kujiunga na Chadema.
Akizungumza jana kwa sharti la kutotajwa jina
akiwa Mirerani, Simanjiro mtu huyo alisema Chadema ni chama makini
chenye uwezo wa kuongoza nchi kwani kinatetea wanyonge na kujali
masilahi ya jamii.
No comments:
Post a Comment