Mkuu wa Jeshi la Polisi Said Mwema
WAKATI ujangili unaotishia kutoweka kwa baadhi ya wanyama katika
hifadhi za taifa nchini ukiendelea kushika kasi, imebainika kuwa baadhi
ya mahakimu, polisi na waendesha mashtaka ni wahusika wakuu wa matokeo
ya ujangili ambao ni chimbuko la biashara ya nyara za Serikali zikiwamo
pembe za ndovu.
Inakadiriwa kuwa tembo wapatao 30 huuawa kila
mwezi na mtandao wa ujangili ambao pia unaundwa na wafanyabiashara
wakubwa wa ndani na nje ya nchi, ambao wamekuwa wakifanikisha uhalifu
huo kwa msaada wa baadhi ya maofisa na askari wa wanyamapori.
Hapa nchini ujangili umekuwa ukifanywa na makundi
ya watu wenye silaha haramu katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba na
maeneo mengine ya wazi, huku kukiwa na taarifa kwamba baadhi ya nyara
hasa pembe za ndovu huingizwa nchini kutoka nchi jirani ya Msumbiji.
Wanunuzi wakuu wanadaiwa kuwapo hapa nchini.
Mkurugenzi wa Tanapa, Allan Kijazi anasema hali ni
mbaya kwa kuwa taifa linatumia gharama kubwa kuwalinda na kukabiliana
na ujangili, lakini wahalifu wanapokamatwa wamekuwa wakiachiwa kinyemela
hata pale ambapo kuna ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.
“Ujangili huu ni mtandao mkubwa sana. Wanatumia
silaha za kisasa zaidi kuliko hata za kwetu…hata kibali cha kununua
silaha hatupati kwa wakati, hali ambayo inadhoofisha jitihada hizi…hapa
tulipofikia ushirikiano wa vyombo vyote ni muhimu,” alisema Kijazi.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa, njia kubwa
ya kuingizia pembe hizo zipo katika wilaya za Tunduru, Namtumbo na
Mbinga mkoani Ruvuma ambako pikipiki hutumika kuvusha kabla ya
kusafirishwa kwa kificho hadi Dar es Salaam ambako hupakiwa kwenda nje
ya nchi kuuzwa kupitia bandarini.
Kushamiri kwa vitendo vya ujangili kumesababisha
kuwapo jitihada za kuukabili, lakini kama alivyosema Kijazi, imebainika
kuwa jitihada hizo zinakwazwa na baadhi ya watumishi katika vyombo vya
dola, wakiwamo baadhi ya mahakimu, polisi na waendesha mashtaka.
Uchunguzi wa Mwananchi ulibaini kuwa baadhi ya
watuhumiwa ambao wamewahi kunaswa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za
ujangili, wametoweka katika njia za kutatanisha na kuacha kesi
zikiendelea.
Mchezo mahakamani
Uchunguzi umebaini kuwa, baadhi ya mahakimu wa
mahakama za wilaya katika mikoa ya Mara, Simiyu, Shinyanga na Kigoma ni
sehemu ya mtandao huo, hivyo watuhumiwa wengi wanaokamatwa na nyara,
zikiwamo silaha hupewa dhamana na hawarudi mahakamani.
Taarifa za uchunguzi zilizothibitishwa na baadhi
ya maofisa wa Tanapa, askari wa wanyamapori na wanasheria wa Serikali
zinadai kesi nyingi za nyara licha ya kuwa na uzito, baadhi ya mahakimu
walioko chini ya mtandao huo hutoa dhamana kwa masharti nafuu na
watuhumiwa huruka dhamana na kuendelea na kazi ya ujangili.
Uchunguzi umebaini mtuhumiwa aliyekamatwa kwa
tuhuma za kuwinda faru, nyani na ngiri ndani ya Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti mwaka 2010, Madubu Masunga Dusara (33), mkazi wa Ng’walali,
haonekani mahakamani baada ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Shinyanga,
Lydia Ilunda kumpa dhamana kwa masharti nafuu.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 6 ya mwaka 2010 hakimu alitoa
dhamana kwa mtuhumiwa kwa masharti nafuu bila kuzingatia thamani ya
wanyama aliokuwa amedaiwa kuua ambayo ni Sh10.304 milioni.
Kwa mujibu wa sheria, ili mtuhumiwa apewe dhamana
anapaswa kuwasilisha fedha taslimu kiasi ambacho ni nusu ya thamani ya
wanyama anaotuhumiwa kuwaua au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika,
lakini katika kesi hiyo wadhamini hawakuwa wakifahamika na baadaye
ilitolewa taarifa kwamba mtuhumiwa haonekani mahakamani.
Kadhalika hakimu huyo alitoa dhamana pia kwa
Malango Dusara (42) ambaye ni kaka yake na mtuhumiwa wa awali, Madubu
ambaye alikamatwa akiwa na risasi 348, lakini pia akiwa chini ya dhamana
taarifa zilifikishwa mahakamani kwamba amefariki dunia.
Hata hivyo, Hakimu Ilunda alisema kuwa chanzo cha kuharibika kwa kesi hizo ni waendesha mashtaka kutopeleka ushahidi kwa wakati.
“Watuhumiwa wanakaa mahabusu miaka bila dhamana
wakati wana haki ya kudhaminiwa. Waendesha mashtaka kila wakati wanadai
ushahidi haujakamilika na sisi tunatekeleza hitaji la sheria kwa kuwa
kupata dhamana kwa makosa kama hayo ni haki ya mshtakiwa,” alisema
hakimu huyo.
Alisema tatizo kubwa la waendesha mashtaka wa
jamhuri wanasababisha kesi nyingi kufutwa ama washtakiwa kuachiwa huru
kwa kuwa hawatoi ushahidi. Hata hivyo, licha ya kudaiwa kwamba
amekwishafariki dunia, Malango ambaye anakabiliwa na kesi ya uhujumu
uchumi namba 3 ya 2010 kwa kukutwa na risasi 548, amekamatwa tena na
sasa yuko mahabusu.
Wakili wa Serikali
Wakili wa Serikali Mwandamizi katika Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kanda ya Shinyanga, Hashimu Ngole
alilithibitishia Mwananchi kwa simu kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
“Alipewa dhamana kwa masharti nafuu na hata sisi
hatukushirikishwa, akaruka dhamana …taarifa zikawa zinakuja kuwa
amekufa…hilo tulilitegemea maana mwanzoni kabisa tuliitahadharisha
mahakama, tukapuuzwa kwa misingi ambayo hatujui…amekamatwa Desemba 14
mwaka huu na sasa yuko mahabusu,” alisema Ngole.
Alisema mdogo wa mtuhumiwa huyo ambaye ana kesi ya
kuua faru naye inasemekana yupo hai licha ya mahakama kuarifiwa kwamba
alishafariki dunia. Uchunguzi umebaini kwamba kabla ya kudaiwa kwamba
wamefariki, tayari mashahidi sita walikuwa wametoa ushahidi wao
mahakamani.
Kuhusu kesi zao, Ngole alisema zinaendelea kwa
kuwa walijua hawajafa kama ilivyodaiwa kwamba kesi ya mtuhumiwa
aliyekamatwa shahidi amebaki mmoja. “Shahidi anatoka Bariadi kuja
Shinyanga …amefika mara tatu hakimu hayupo… anarudi kesi ilikuwa Desemba
2 hakimu hakuwapo, imepangwa Desemba 31 mwaka huu sijui kwa tarehe hizo
zilizopangwa kama itasikilizwa,”alisema Ngole.
Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa, hata mawakili wa
Serikali Mkoa wa Shinyanga ambao walikuwa wakiendesha kesi hizo
hawakuulizwa wakati wa watuhumiwa kupewa dhamana na kama sheria
ingezingatiwa, Serikali ingekuwa na uwezo wa kukamata mali za wadhamini
baada ya watuhumiwa kuruka dhamana.
“Makosa yao ni makubwa ambayo yanazidi thamani ya Sh10 milioni.
Sheria inahitaji dhamana yao walipe nusu ya fedha taslimu na wawe na
wadhamini wenye mali isiyohamishika, lakini wao walidhaminiwa na watu
wasiofahamika bila hata kutushirikisha sisi, matokeo yake hawaonekani na
ujangili unazidi,”alisema na kuongeza:
“Tulichotahadharisha mapema ndicho kimetokea, hii
ni hatari watu wameua faru bila hata kuangalia thamani ya mnyama
wanapewa dhamana kirahisi namna hiyo?” alihoji.
Alikwenda mbali zaidi na kudai mwaka 2010 waliamua
kwenda Meatu kuhakikisha kesi za watuhumiwa wa nyara zinashu ghulikiwa
na kuisha, lakini kati ya kesi 80 watuhumiwa wote walikuwa nje ya
dhamana na hawaonekani mahakamani.
“Waliokuwa wanafika hawafiki 10 tukalazimika
kufuatilia na lugha huwa hiyo kuwa wamekufa…kama hakutafanyika mageuzi
katika vyombo vyetu vya uamuzi hata operesheni zingefanyika nyingi
hakuna mafanikio…Tanapa wanafanya kazi sana tena katika mazingira
magumu, wanaleta watu wanaachiwa tutegemee nini,” alisema.
Hukumu nyingine
Ngole alisema hukumu ambazo zimekuwa zikitolewa
zinakatisha tamaa, huku akitoa mfano wa kesi namba 3 ya uhujumu uchumi
ya mwaka 2010 ya Masanja Maguzu ambaye alikamatwa akiwa na silaha aina
ya SMG, risasi 31 na magazine 3.
Alisema Maguzu kabla ya kukamatwa na silaha hizo
alikuwa tayari ametumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kutiwa
hatiani kwa kosa la kuua wanyama ndani ya hifadhi.
“Kimsingi baada ya kutumikia kifungo cha miaka
mitano alitolewa, lakini baadaye alikamatwa na silaha ya kivita
nyumbani, risasi na magazine lakini alifungwa kifungo cha nje.”
Alisema hata wanapoomba kukata rufaa hawapewi
nakala za hukumu na mwenendo wa shauri. ”Inachukua mpaka miaka mitatu
watu wanamaliza vifungo vyao hujapata nakala hiyo…kwa madai kuwa
vitendea kazi ni shida,”alisema.
Alisema baadhi ya watoa uamuzi wanatumia udhaifu
wa sheria kutekeleza matakwa yao na kwamba uamuzi huo unazidi
kuligharimu taifa, hivyo aliomba sheria zilizopo zirekebishwe iwe kama
ilivyo kwa makosa ya ubakaji adhabu zake zinakuwa kali.
Wasajili Mwanza, Tabora
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Isaya
Alphan alipoulizwa kuhusu tuhuma za mahakimu hao alisema hakuna taarifa
sahihi na kwamba amekuwa akizisikia kwenye vyombo vya habari.
“Hilo la Shinyanga liko Kanda ya Tabora naomba uwatafute hao,…
hili la watuhumiwa walioachiwa katika mahakama ya Wilaya ya Serengeti
mpaka niangalie kwenye faili… kwa sasa siko ofisini niko likizo mpaka
Januari,”alisema Alphan kwa simu.Naye Msajili wa Mahakama Kanda ya
Tabora, Thomas Simba aliliambia Mwananchi kwa simu kuwa hajapokea
taarifa zozote za malalamiko kuhusu suala hilo.
“Haya masuala ya dhamana ni very complicated (yana
mkanganyiko) …sijui kwa hilo la hao wa nyara kupewa dhamana kisha
hawaonekani mahakamani…kwa kifupi ni kwamba dhamana ni haki ya mshtakiwa
kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya
15,”alisema Simba na kuongeza:
“Katika ibara ya (1) kila mtu anayo haki ya kuwa
huru na kuishi kama mtu huru, (2) Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu
kuwa huru na kuishi kwa uhuru, itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote
kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa kwa nguvu
au kunyang’anywa uhuru wake isipokuwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na
sheria.”
Hata hivyo, alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu
masharti ya dhamana kwa watu walioua wanyama wenye thamani ya zaidi ya
Sh10 milioni Simba alisema:
“Kwa kuwa hilo liko mahakamani sipendi kulisemea
nini kilipaswa kufanyika… kama kuna mambo hayaendi vizuri wahusika
wanatakiwa kukata rufaa kuja mahakama ya juu kupinga uamuzi huo.”
Hata hivyo, Mwananchi lilibaini kuwa msajili huyo
ni mgeni katika kituo hicho cha kazi kwani amekaa kituoni hapo kwa muda
usiozidi miezi minane, akitokea Kanda ya Kigoma alikokuwa akifanya kazi.
Itaendelea kesho Jumapili….
No comments:
Post a Comment