Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisoma hotuba yake wakati wa
sherehe za kuupokea Mwaka mpya wa Kiislamu 1434 Hijriyya, zilizofanyika
katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, leo Desemba 16, 2012.
Picha na OMR
Dk. Bilal aongoza Waislamu kuupokea
mwaka mpya wa Kiislamu 1434 Hijriyya
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib
Bilal ameongoza waumini wa Kiislamu kuupokea mwaka mpya wa Kiislamu
katika hafla iliyoandaliwa na Jumuiya ya Istikaama (ISTIQAAMA) tawi la
Dar es salaam.
Sherehe hizo za kuukaribisha mwaka mpya wa Kiislamu 1434 Hijriyya ambazo
zilifanyika leo katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam
zilihudhuriwa na waumini wa Kiislamu kutoka nchi mbalimbali pamoja na
mabalozi wa Sudan, Oman na Iran nchini Tanzania.
Akizungumza na waumini hao Dk. Bilal aliwataka Waislamu kuuanza mwaka
mpya wa Kiislamu kwa kuepuka machafuko na kudumisha amani ambao ndio
msingi mkuu wa dini ya Kiislamu.
Makamu wa Rais alisema katika serikali wameanza kuingia wasi wasi
kutokana na vurugu za hivi karibuni ambazo zimeashiria kuvunjika kwa
amani nchini.
“Mimi na wenzangu Serikalini tumeanza kuingia wasi wasi. Hivi karibuni
katika nchi yetu kumetokea vurugu ambazo hatimaye zimeashiria kuvunjika
kwa amani ya nchi yetu. Mali zimepotea na wengine wamepoteza maisha kwa
kisingizio cha dini,” alisema Dk. Bilal na kuongeza
“Machafuko hayo yametufanya tujiulize hawa watu wanafuata misingi ipi ya
Dini ambayo imewafanya wao wawe na jazba kiasi cha kushindwa kuwa na
busara katika maamuzi yao. Je ni vipimo vipi vya msingi wa Dini ambavyo
wao wanavifuata. Tunashindwa kupata jawabu”.
Makamu wa Rais aliwaeleza waumini hao kuwa kwa mawazo yake anaona
matatizo mengi yanayolenga Uislam ni ukosefu wa elimu, ile ya Uislam
wenyewe, na elimu ya dunia na kuwataka Waislamu kusoma kwa dhati jambo
ambalo anaamini linaweza kusaidia mambo ya jazba yakapungua na hatimaye
kutokomea kabisa.
“Tukiendeleza jazba ndio ziwe na nguvu kuliko mafunzo ya Quran tukadhani
kuwa mwenye jazba ndiye Muislamu wa kweli tutaharibikiwa,” alibainisha.
Akisoma risala ya Jumuiya hiyo, Sheikh Juma Nassor Alhinai aliiomba
serikali kuifanya siku ya kwanza ya mwaka mpya wa Kiislamu kuwa ni ya
mapumziko
Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, AlhajiMussa Salum
alikubaliana na wazo hilo lakini aliwataka Waislamu wenyewe kubadilika
kwa kuitangaza tarehe hiyo ya kwanza ya mwaka mpya kwa kuipa nafasi
katika maisha yao ya Kiislamu ili iweze kutambulika ipasavyo.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
Jumapili – Disemba 16, 2012
No comments:
Post a Comment