MBUNGE wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema John Mnyika, jana
aliwaeleza wakazi wa Kijitonyama kwa Ali Maua ‘A’ Jijini Dar es Salaam
kuwa nchi iko kwenye hali tete kutokana na kusudio la Serikali la kutaka
kupandisha bei ya umeme.
Mnyika aliyasema hayo kwenye mkutano ulioandaliwa na Chama hicho kwa nia ya kumpongeza Diwani wa Kata hiyo, Juma Uloleulole kufuatia ushindi alioupata wa kurudishiwa nafasi yake ya udiwani na Mahakama Kuu ya Tanzania wiki iliyopita.
Alisema kuwa kupanda kwa gharama za umeme kutasababisha kupanda kwa bei ya bidhaa mbali mbali kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji. Aliwaambia wananchi kuwa hivi sasa bei ya vyakula na usafiri iko juu, hivyo kama umeme utapanda unaweza pia kutasababisha kwa mfumuko wa bei.
“Badala ya Serikali kudhibiti kupanda kwa bei ya umeme, yenyewe inachokifanya ni kuipandisha kila kukicha kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya. Bei ya umeme ikipanda hata bei ya bidhaa na huduma zingine pia itapanda hali inayopelekea kuongezeka kwa mfumuko wa bei,” alisema Mnyika.
Kuhusu ushindi alioupata Juma Uloleuloe wa kurudishiwa nafasi yake ya udiwani na Mahakama Kuu ya Tanzania, Mnyika aliwaambia wananchi jinsi mahakama mara nyingine zinavyoweza kuminya haki ya mtu.
Alisema kuwa kazi nzuri ya utetezi iliyofanywa na Profesa Abdallah Safari ndiyo sababu ya ushindi huo baada ya Mahakama Kuu kuridhika na ushahidi wake. Alisema kitendo cha Mahakama kumfutia nafasi ya Udiwani Juma Uloleulole inaonesha ni kwa jinsi gani mahakama mara nyingine zinavyoshindwa kutenda haki hata kama haki hiyo iko wazi.
“Mheshimiwa Ulole baada ya kurudishwa kwenye nafasi yako ya udiwani, ninachokuomba sasa hakikisha unafanya kazi ya kupambana na vitendo vyote vya kifisadi kwenye eneo lako la uongozi kama Diwani. Rasilimali nyingi za Watanzania zinapotea kutokana na vitendo vya wizi, hivyo hakikisha unasimamia matumizi ya rasilimali hizo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi,” alisema Mnyika na kuongeza,
“Sisi Chadema tumekuja na sera ya nguvu ya umma. Sera hii inalenga kuhakikisha mambo mawili, kwanza tunataka wananchi wanufaike na rasilimali zao, na pili tunataka viongozi wawatumikie umma na siyo kuutumikisha umma,” alisisitiza Mnyika.
Mnyika aliwataka wananchi wa Kijitonyama kumpa ushirikiano Diwani wao ili kazi yake ya kusukuma gurudumu la maendeleo iwe nyepesi. Alisema kuwa Chadema inatambua kuwa imebaki miaka 3 tu kabla ya kuingia tena kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, lakini akawasisitiza madiwani wote wa Chama hicho kuwa muda huu unatosha kuwatumikia wananchi vizuri.
No comments:
Post a Comment