MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbarali,
mkoani Mbeya, Mathayo Mwangomo, amewataka wananchi wilayani humo
kutokukubali maneno ya uchochezi yanayodhoofisha maendeleo na juhudi za
Serikali katika kutatua matatizo ya wananchi wake.
Mwangomo alitoa kauli hiyo wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ruiwa wilayani humo.
Alisema kuwa, hivi sasa Chama cha Mapinduzi ambacho kipo madarakani
kinatekeleza sera zake hivyo wananchi hawana sababu za kuendelea kusikiliza maneno ya kubeza maendeleo yanayofanywa na chama hicho.
“Wananchi mnatakiwa kutokubali maneno ya uchochezi yanayotolewa na wanachache ambayo msingi wake ni kudhoofisha maendeleo na juhudi za Serikali katika kutatua matatizo yenu,”alisema Mwangomo.
Alisema kuwa, CCM imefanya mambo mazuri katika jamii ikiwa ni pamoja na kujenga shule za msingi na sekondari za kata, ambazo zimeongeza kiwango cha elimu nchini.
Mbali na kuwaleeza hivyo wananchi hao, Mwenyekiti huyo pia alipokea kero za wananchi wa kata hiyo ya Ruiwa ikiwa ni pamoja na ubadhilifu wa fedha zaidi ya Sh60 milioni zilizochangwa na wananchi hao kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Gwili ambazo zinadaiwa kutafunwa na diwani wa kata hiyo, Alex Mdimilage, anayedaiwa kumtorosha mhasibu wa shule hiyo na kutoroka na fedha za wananchi zaidi ya Sh27milioni na kuiacha shule hiyo ikiwa haina chochote.
Sambamba na hilo wananchi hao pia walilalamikia vitendo vya diwani wao kuwa, amekuwa kikwazo cha maendeleo ya kata hiyo kutokana na uwajibikaji wake mbovu uliopelekea wananchi wengi kukihama chama hicho.
Akijibu tuhuma hizo mbele ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa wilaya, Diwani wa kata ya Ruiwa , Alex Mdimilage alikanusha tuhuma hizo na kudai kuwa mambo yote yanayozungumzwa dhidi yake ni chuki za kisiasa na kwamba kwa kipindi chake hiki amesimamia miradi mbalimbali kijijini hapo na kata kwa ujumla.
Mwenyekiti wa CCM huyo alikiri kuwepo kwa viongozi wazembe wilayani humo, hivyo amewataka viongozi wanaohusika na tuhuma hizo kujiengua mapema na hawatasubiri Takukuru na Polisi na kero zote zilizowasilishwa na wananchi atazifanyia kazi.
No comments:
Post a Comment