tangazo

Wednesday, October 10, 2012

Rais wa Kenya atibua njama ya wabunge


Kero la wananchi wa Kenya kwa wabunge wao

Rais wa Kenya Mwai Kibaki, amekataa kuidhinisha mipango ya wabunge wa taifa hilo kujipatia kitita kikubwa cha pesa kama marupurupu ya kuhudumu kama wabunge.

Wabunge hao walipanga kujilipa dola alfu mia moja na kumi kila mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Lakini bwana Kibaki amesema kuwa hatua hiyo inakiuka katiba na haiwezi kutekelezwa wakati ambapo walimu pamoja na madaktari nchini Kenya wamekuwa wakigoma kudai nyongeza ya mishahara.

Waandamanaji waliojawa na ghadhabu nchini Kenya walijitokeza hapo jana kulaani hatua ya wabunge hao kutaka kujilipa mamilioni ya pesa kama pesa za ziada wakati bunge litakapofunga vikao vyake kwa maandalizi ya uchaguzi mwaka ujao.

Waliwataja wabunge hao kama fisi wenye ulafi.

Wabunge wa Kenya ni baadhi ya wale wanaopokea mishahara mikubwa sana barani Afrika , wakipokea takriban dola elfu 10,000 kama mshahara kila mwezi.

Malipo hayo ya ziada ya dola 110,000 kwa kila mmoja walitaka yalipwe wakati watakapofunga vikao vyao kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka 2013.

Wadadisi wanasema kuwa wananchi wangetozwa kodi zaidi ili kugharamia malipo hayo ya dola milioni 23.

Hatua hii imewakasirisha watu wengi, hasa ikizingatiwa kuwa inakuja baada tu ya migomo katika sekta ya umma ambapo madaktari, walimu na hata wahadhiri wa vyuo vikuu walisusia kazi wakidai nyongeza ya mishahara.

Mswaada huo ulipitishwa siku ya Alhamisi ikiwa sehemu ya mabadiliko yaliyofanyiwa mswaada wa fedha bungeni.

Mnamo mwezi Septemba, shule za umma zilifungwa kwa wiki tatu wakati walimu walipogoma wakidai nyongeza ya mishahara na huku madaktari nao wakitaka mazingira bora ya kazi.

No comments:

Translate