TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewataka wananchi kuendelea na shughuli
zao kama kawaida na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimedhibiti hali
ya ulinzi na imeimarishwa katika maeneo yote ya Zanzibar.
Taarifa ya Serikali iliyotolewa leo
usiku na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud
Mohammed imesema Zanzibar bado ni shwari na inaendelea kuwa katika hali
ya amani na utulivu.
Akizungumzia tukio la vurugu zilizofanywa na wananchi wachache, Waziri
Mohamed Aboud alisema vikundi vya vijana vinavyosadikiwa kuwa ni wafuasi
wa Sheikh Farid Hadi walifanya vurugu hizo katika mitaa ya Darajani,
Michenzani, Muembeladu,Magomeni,Amani wakidai Sheikh wao haonekani na
kudhani amekamatwa na vyombo vya Dolan a kuwekwa ndani.
Waziri Mohamed Abud alisema Serikali
imewasiliana na vyombo vya Dola ikiwemo Polisi,Jeshi la wananchi wa
Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa, Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar,KMKM,JKU,Chuo cha Mafunzo,Zimamoto na Valantia ambapo vyombo
vyote hivyo vimeeleza kutoelewa chochote kuhusu Sheikh Farid.
Waziri huyo alisema kwamba Jeshi la
Polisi limepokea taarifa ya kutoonekana kwa Sheikh Farid ambapo kwa
sasa Jeshi hilo linaendelea kumtafuta na kufanya uchunguzi juu ya tukio
hilo ili kupata ukweli wake na kuchukua hatua zinazofaa.
Alisema kwamba wakati Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi wake,
wananchi wameombwa kutoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa vituo vya Polisi
au kupitia Masheha, Ofisi za Wilaya na Mikoa katika maeneo yao.
Waziri Mohamed Aboud amesema Serikali
inawasihi wwananchi waache kujiingiza katika vitendo vya fujo na vurugu
kwani kutenda hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na Serikali
haitovumilia vitendo hivyo.
Katika tukio la leo mchana, vijana hao wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa
Sheikh Farid Hadi walifanya vitendo vya vurugu ikiwemo kuchoma moto
Maskazini za CCM,kuvunja maduka,kupora mali za watu na kuharibu
miundombinu ya barabara na kusababisha hasara kubwa.
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR
17/10/2012
ZANZIBAR,TANZANIA
No comments:
Post a Comment