Wanajeshi wa Ivory Coast wakilinda mpaka wa nchi hiyo na Ghana
Taifa la Ivory Coast litafungua rasmi mipaka yake na Ghana hii leo.
Mipaka kati ya mataifa haya mawili ilikuwa imefungwa kwa kipindi cha zaidi ya wiki mbili baada ya mashambulizi kutekelezwa dhidi ya maafisa wa polisi na wale wa kijeshi katika mipaka ya ivory coast.
Kwa mujibu wa waziri wa ulinzi wa ivory coast mataifa ya ivory coast na ghana yameweza kuimarisha ulinzi katika mipaka hiyo na kudokeza kuwa mashambulizi hayo yamekuwa yakitekelezwa na wanamgambo wanaomuunga mkono aliyekuwa Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo
Watu kadhaa waliuawa wakati watu waliokuwa wamejihami waliposhambulia kizuizi cha polisi katika mji wa mpakani wa Noe tarehe 21 mwezi Septemba.
Maafisa walilaumu wafuasi wa Rais aliyeondoka mamlakani Laurent Gbagbo.
Ivory Coast ilijibu shambulizi hilo kwa kufunga mipaka yake ya majini, ardhini na angani na Ghana lakini ikaanza tena safari za ndege kati ya nchi hizo siku chache baadaye.
Hatua ya kufunga mipaka imefunga njia rasmi ya usafiri katika ghuba ya Guinea, kutoka upande wa Ivory Coast hadi Nigeria.
Baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata mnamo mwaka 2010, bwana Gbagbo alikataa kukubali kushindwa na Rais Ouattara, ambaye hatimaye alimwondoa mamlakani kwa usaidizi wa Umoja wa Mataifa na Ufaransa.
Gbagbo kwa sasa yuko katika mahakama ya kimataifa ya Hague, akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake ya uhalifu wa kivita.
No comments:
Post a Comment