tangazo

Sunday, December 23, 2012

BIBI ACHINJWA KAMA KUKU MKOANI MARA

 
 
   na Berensi Alikadi, Musoma

SIKU mbili baada ya mwendesha bodaboda wa mjini Musoma kuchinjwa na kuporwa pikipiki, mama mmoja mkazi wa Kijiji cha Kwibara wilayani Butiama mkoani Mara, Tabu Makanya (68), ameuawa kwa kukatwa na mapanga kisha kuchinjwa mithili ya kuku na watu wasiojulikana.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana katika katika kijiji hicho kilichoko Kata ya Mugango baada ya wauaji wanaokadiriwa kufikia wanne, kuvunja mlango wa nyumba aliyokuwa amelala bibi huyo na wajukuu zake wawili.
Habari zinasema kuwa, wauaji awali waliomba kupatiwa simu na fedha na baada ya kukosekana kwa vitu hivyo, waliwaamuru wajukuu wa binti huyo kutulia wakati wanamcharanga kisha kumkata kichwa chake chote.
Mmoja wa watoto wa marehemu, Nyasinde Marubira, aliliambia Tanzania Daima Jumapili nje ya chumba cha kuhifadhia maiti mjini Musoma kuwa, mauaji hayo yamewaumiza na akadai huenda yanatokana na imani za kishirikina.
Alisema baada ya kuamriwa kujifunika kichwa, alisikia watu hao wakisema “leta panga kata kichwa” huku mama yake akipiga kelele na baada ya hapo kukawa kimya.
Nyasinde alisema baada ya kusikia mama yake akiwa kimya na watu waliowavamia kuondoka, aliamka na kumfunua mama yake aliyefunikwa na kumkuta akiwa hana kichwa huku wauaji hao wakiwa wameondoka nacho.
Kwa ujasiri mkubwa, alitoka nje na kupiga yowe na ndipo wanakijiji walipoamka na kuanza kuwafukuza wauaji ambao baada ya kuona watakamatwa, waliamua kutupa mfuko uliokuwa na kichwa hicho porini.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa, akizungumzia mauaji hayo, alisema tayari ameiagiza kamati ya ulinzi na usalama wilayani Butiama kuchukua hatua ya kukabiliana na mauaji hayo ikiwa ni pamoja na kutolala hadi wauaji hao wapatikane.
Alisema pamoja na agizo hilo, pia kamati hiyo imekutana jana kupanga mikakati ya kupambana na mauaji hayo, ambapo kesho itakutana na viongozi mbalimbali Wilaya ya Butiama kuweka mikakati ya pamoja ya kudhibiti hali hiyo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema inashangaza kuona kuwa matukio hayo yanatokea ndani ya vijiji, huku viongozi wa vijiji na wananchi wakishindwa kujua wauaji.
Kuongezeka kwa mauaji hayo kulisababisha maandamano makubwa ya waendesha bodaboda juzi mkoani hapa hadi ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara wakimtaka aeleze ni hatua gani zinafanywa na jeshi hilo kukomesha matukio hayo la sivyo ajiuzulu nafasi hiyo.
Hata hivyo, maandamano hayo yalikumbana na ulinzi mkali wa askari wa jeshi la polisi kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) waliokuwa na silaha za moto na mabomu ya machozi.
Akizungumzia matukio hayo Kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma, alisema kuwa watu wanne wanatafutwa na jeshi hilo kwa nguvu baada ya kukimbia.
Taarifa hiyo ya kamanda Mwakyoma, kwa waandishi wa habari ilisema mauaji ya Sabina Mkireri aliyeuawa kisha wauaji kuondoka na kichwa chake katika Kijiji cha Kabegi Kata ya Nyakatende Wilaya ya Butiama, jumla ya watu sita wameshakamatwa na wanahojiwa na polisi.

No comments:

Translate