tangazo

Tuesday, December 18, 2012

Tanesco sasa kutekeleza agizo la Simbachawene


SIKU moja baada ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene kulitaka Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), kununua nguzo za umeme zinazozalishwa nchini, shirika hilo limekiri kutekeleza agizo hilo.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema kuwa, agizo hilo ni sehemu ya mkakati wa Tanesco wa kutumia nguzo za ndani kwa ajili ya kusambaza umeme kwa watumiaji, jambo ambalo wanaamini litaungwa mkono na wadau wengi.

Alisema uamuzi huo unatokana na kupunguza gharama za ununuzi wa nguzo hizo kutoka nje ya nchi na kuunga mkono kampuni za ndani zinazozalisha bidhaa hizo.

“Katika kuleta mabadiliko ndani ya shirika letu, tumeamua kununua bidhaa zinazozalishwa ndani zikiwamo za magogo na nguzo ili tuweze kusambaza umeme kwa wateja, hii itasaidia kupunguza gharama za ununuzi wa bidhaa hizo nje ya nchi” alisema Mramba.

Aliongeza, hatua hiyo itaboresha masoko ya ndani pamoja na kuleta ushirikiano mzuri baina ya shirika, wazalishaji wa watumiaji wengine, jambo ambalo litasaidia kukuza soko la bidhaa hizo na huduma.

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kutokana na hali hiyo, Tanesco itatangaza zabuni za ununuaji wa nguzo hizo kama ilivyo taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja na kushindanisha makampuni zitakazojitokeza, lakini yatakayopewa kipaumbele ni kampuni ya ndani na si ya nje kama ilivyokuwa awali.

Alisema kutokana na hali hiyo wamewataka wazalishaji wa ndani kujitokeza kwenye zabuni hiyo ili waweze kushinda na Tanesco kununua nguzo kwenye kampuni hiyo.

Alisema mkakati wao ni kuhakikisha kuwa, huduma wanazozitoa zinakidhi viwango, jambo ambalo linaweza kupunguza malalamiko ya matatizo ya umeme kwa watumiaji.

Juzi, Naibu Waziri, Simbachawene alilitaka shirika hilo kununua nguzo zinazozalishwa na viwanda vya ndani baada ya kuona zinakidhi viwango.

No comments:

Translate