tangazo

Tuesday, December 18, 2012

BIFU LA SUMAYE NA NAGU NGOMA NZITO

 
 Waziri Mkuu Mstaafu,Frederick Sumaye  


Joseph Lyimo, Hanang’

TOFAUTI za kisiasa baina ya makada wawili wa CCM, Mary Nagu na Frederick Sumaye zimezidi kufukuta, baada ya vigogo hao, kupingana hadharani kuhusu tuhuma za rushwa ndani ya chama hicho tawala.

Sumaye ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu na Nagu ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), wameingia katika mgongano na mgogoro huu ulishika kasi wakati wa uchaguzi wa kumpata mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa, kupitia Wilaya ya Hanang’ ambapo Sumaye alibwagwa.

Katika uchaguzi huo uliofanyika, Nagu alimshinda Sumaye kwa kura, na baadaye, waziri huyo Mstaafu aliibuka na kueleza kuwa kushindwa kwake kulitokana na rushwa iliyokithiri kwenye uchaguzi huo, ikiwa inasukumwa na makada kadhaa wa CCM.

Juzi, Sumaye alirudia kuituhumu CCM kwa ufisadi na akaenda mbali zaidi kwa kuwataka wanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), kupiga vita kwa nguvu zote matumizi a rushwa aliyeeleza kuwa hivi sasa, yamekithiri kwenye chaguzi za chama hicho.

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula alipoulizwa kuhusiana na madai hayo ya Sumaye kuhusiana na chama hicho kutuhumiwa mfululizo kwa rushwa alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa.“Nipo katika shughuli kidogo siwezi kuzungumzia hilo kwa sasa,” alisema Mangula na kukata simu.

Hata hivyo, wakati Sumaye anaeleza hayo wakati wa uchaguzi wa mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Hanang’, Nagu akiwa mjini Babati siku hiyo, alisema ufisadi ni upungufu wa mtu na siyo chama.

Dk Nagu alisema hayo alipokuwa akizindua shina la wakereketwa wa Mrara, kabla ya kufungua kikao cha Baraza Kuu la (UVCCM) la mkoa.

Akizungumza kwenye uchaguzi wa Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Hanang’ uliofanyika juzi mjini Katesh, Sumaye alisema matumizi ya rushwa kwenye chaguzi za nafasi mbalimbali ndani ya CCM, yanatakiwa kupigwa vita na wanachama wa UVCCM, kwani vijana ndiyo jeshi la CCM linalotakiwa kuwa mstari wa mbele kuongoza mapambano.

Dk Nagu alisema ufisadi ni mapungufu ya mtu, hayahusiani na CCM na unaweza kuondolewa na Serikali iliyopo madarakani kupitia chama hicho peke yake. Dk Nagu, ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Hanang’ mkoani Manyara aliyasema hayo jana mjini Babati, wakati akizindua shina la wakereketwa wa Mrara kabla ya kufungua kikao cha Baraza Kuu la (UVCCM) la mkoa huo.

Waziri huyo ambaye pia ni Kamanda wa UVCCM wa mkoa huo, alisema ufisadi ni mapungufu ya mtu binafsi kwani hayahusiani na chama, ndiyo sababu CCM haitukani wala kutoa kashfa kwenye mikutano yake.

“Hivi sasa neno fisadi limeenea kila mahali, jamani na kila mtu mwenye uwezo anaitwa fisadi, kwani mimi nimefisadi nini cha mtu, hayo ni maneno ya wapinzani tu, ufisadi utaondolewa na CCM,” alisema Dk Nagu.

Katika uzinduzi huo, Dk Nagu alitoa ahadi kwenye kikundi hicho kwa kuwapa mkopo wa pikipiki 20 na vyerehani 12 ambavyo vitawanyanyua kiuchumi kwani maendeleo ya kupachikwa na kupeperushwa hayatakiwi kwenye chama hicho.
 Akizungumza wakati akifungua Baraza la UVCCM la mkoa huo, Nagu aliwataka vijana kujituma na kuchangamkia fursa zinazojitokeza ikiwemo kuendesha matrekta, pikipiki, kushona kwa vyerehani na mengine kuliko kukaa na kusubiri.

Alisema vijana ndiyo nguzo ya CCM hivyo wanatakiwa wanyanyue vichwa vyao juu na kutazama mbele huku wakiwa kifua mbele badala ya kuinamisha vichwa chini,kwani huu ni wakati wa kujishughulisha na kuchacharika siyo kubangaiza.

No comments:

Translate