tangazo

Wednesday, December 26, 2012

SERIKALI YASHINDWA KUONDOA BIDHAA BANDIA NCHINI




LICHA ya kueleza kuwa asilimia 20 ya bidhaa zote zinazoingizwa nchini ni bandia, Serikali imeshindwa kutekeleza mikakati yake ya kuhakikisha inasafisha bidhaa hizo sokoni.

Desemba 14 mwaka huu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda aliwaeleza waandishi wa habari kwamba kama hali hiyo itaachwa iendelee itasababisha madhara makubwa kwa wananchi na taifa kwa jumla.

Dk Kigoda aliwataka wafanyabiashara wanaouza bidhaa hizo kuziondoa sokoni haraka kabla Serikali haijaanza kuziondoa kwa nguvu, huku yeye pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara yake, Joyce Mapunjo wakishindwa kueleza zoezi hilo litaanza lini.

Alisema uchunguzi umebaini kuwa, kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo mkoani Pwani, kuna bandari bubu 32, ambazo hutumika kupakua bidhaa hizo bandia.

Lakini jana akizungumza na gazeti hili, Dk Kigoda alisema bado wizara hiyo inapanga mikakati ya kuhakikisha inaondoa bidhaa hizo pamoja na kuwachukulia hatua watakaobainika kuendelea kuziuza.

“Kuna taratibu tunafanya kwanza kabla ya kuanza kwa mchakato wa kuingia sokoni na kuzitambua bidhaa hizo” alisema Dk Kigoda.

Alipoulizwa haoni kwamba kuchelewa kwa operesheni hiyo ndio kunazidi kuwafanya wafanyabiashara hao kuingiza bidhaa hizo na hasa katika kipindi hiki cha sikukuu alisema, “Nimesema bado kuna taratibu zinafanyika mbona unataka kuharakisha.”

Dk Kigoda pia alisema mchakato wa kuunda bodi mpya ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) bado unaendelea kufanywa.

Wiki tatu zilizopita wkaati akifungua kinu cha kuzalisha Cement katika kiwanga cha Twiga nje ya jiji la Dar es Salaam Dk Kigoda aliliambia Mwananchi kwamba bodi hiyo itatangazwa kabla ya Desemba 31 mwaka huu.

Katika maelezo yake ya Desemba 14 alisema kuenea kwa soko la bidhaa bandia nchini kunatokana na bei za bidhaa hizo kuwa ndogo, hivyo kuwavutia wateja wengi.

Alizitaja bidhaa hizo kuwa ni matairi ya magari na pikipiki, mafuta ya kupaka, maziwa ya watoto, nyaya za umeme, simu za mkononi na vyakula mbalimbali.

Alisema katika kukabiliana na hali hiyo, wizara yake inashirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kuchunguza bidhaa zinazoingia nchini kabla hazijasambazwa katika soko.

No comments:

Translate