tangazo

Wednesday, December 26, 2012

MAJAMBAZI YAPORA SH 23 MILLION MOSHI


WATU wanaodhaniwa kuwa majambazi wakiwa na bastola, juzi walimvamia mfanyabiashara mmoja wa eneo la Majengo, Mjini Moshi na kumpora fedha taslimu Sh23 milioni.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 8:00 mchana wakati mfanyabiashara huyo alipokuwa akipeleka fedha hizo benki.

Habari za kuaminika zinaeleza kuwa mfanyabiashara huyo (jina tunalo) alipofika katika mzunguko wa magari karibu na Shule ya Sekondari ya Majengo, alivamiwa na kuporwa fedha hizo.

Mashuhuda wa tukio hilo walieleza kuwa kabla ya majambazi hao kumpora fedha hizo, walimzuia kwa gari lao aina ya Toyota Noah na kumtishia kwa bastola.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa bado uchunguzi unaendelea.

Kigogo CUF naye alizwa
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Julius Mtatiro jana alisherehekea Krismasi kwa majonzi baada ya wezi kupasua kioo cha gari lake kwa dawa maalumu kisha kuiba vitu mbalimbali.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake Makuburi, Dar es Salaam na mwenyewe aligundua ilipofika asubuhi baada ya kurejea kutoka kanisani.

Katika taarifa yake aliyoiweka kwenye mtandao wa Kijamii wa Facebook, Mtatiro alilielezea tukio hilo kuwa ndiyo Krismasi yake… “Hii ndiyo Krismasi yangu. Kwenda kanisani tu, ndiyo haya yamenikuta. Jamaa wamebeba hadi ‘Dash Board’ ya katikati,” alisema Mtatiro kwenye mtandao huo ambako pia aliweka picha ya gari hilo aina ya Toyota Lexus.

Baadaye Mtatiro alimwambia mwandishi wetu kuwa hajui hasa tukio hilo lilitokea saa ngapi... “Sikuwa najua chochote. Nilipoamka asubuhi nilikwenda kanisani. Mimi nasali katika Kanisa la Katoliki, Parokia ya Makuburi, nilikwenda bila gari kwani siyo mbali ni kama mita 300 tu kutoka nyumbani kwangu.”

“Hata hivyo, wakati naondoka nyumbani niliwaacha vijana wengi tu hivyo sikuwa na wasiwasi wowote. Lakini niliporudi nikakuta wizi huo umeshatendeka.”

Mtatiro alisema wezi hao waliiba vitu hivyo baada ya kuvunja kioo kidogo cha mlango wa nyuma wa gari hilo kwa kutumia dawa maalumu ambayo ilikifanya kiwe chengachenga, kisha kufungua mlango na kuingia ndani ya gari.

Alisema pia waliiba vifaa vya kufungulia vioo (power window) pamoja na redio ya gari hilo… “Vilevile wamepekuapekua ndani ya gari, lakini hawakufanikiwa kupata kitu kingine kwa kuwa sikuwa nimeweka nyaraka zozote muhimu ndani ya gari. Hawakuchukua leseni yangu nimeikuta.”

Mtatiro alisema atatoa taarifa polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe.

No comments:

Translate