tangazo

Sunday, December 23, 2012

SERIKALI YAAMUA KUIFUMUA KAMPUNI YA TANESCO.

 
                   Waziri wa Nishati na Madini,Sospeter Muhongo 

SERIKALI imetoa msimamo wake kwamba bei ya umeme haitapanda kama Shirika la Umeme nchini (Tanesco) lilivyopendekeza, huku ikiahidi kufanya mabadiliko makubwa ndani ya shirika hilo kuanzia Januari mwakani.

Imesema lengo la mabadiliko hayo ni kuhakikisha yanaenda sambamba na kutafuta kampuni nyingine za kuzalisha umeme nchini  ili kuboresha huduma hiyo kwa wateja.

Akizungumza na wadau wa umeme katika Ukumbi wa Halmashauri wa Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema kwamba mapendekezo ya Tanesco kupandisha gharama za umeme na ambayo Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) iliyapokea, hayalengi kutatua matatizo ya shirika hilo.

Alisema  kuwa tatizo ndani ya Tanesco siyo pesa, bali ni mfumo mbovu wa uendeshaji, ambao unalifanya shirika hilo kuwa mzigo na kushindwa kutoa huduma bora kwa wateja wake, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wateja.

“Msimamo wa Serikali ni kwamba, bei haitapanda kwa kuwa  matatizo ya Tanesco yanaeleweka kuwa ni mfumo mbovu,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza:

“Tunategemea kuifumua Tanesco na kuangalia uwezekano wa kupata kampuni zaidi ya mbili za kuzalisha umeme, maana mfumo wa menejimenti ni mbovu na umepitwa na wakati.”

Alifafanua kuwa kuanzia Januari mwakani watabadilisha muundo huo ili kupata kampuni ya kuzalisha na ya kusambaza umeme nchini.

Waziri huyo aliongeza kwamba baada ya mabadiliko hayo, ndipo Tanesco inaweza kutoa maoni ya kuomba kuongeza gharama za nishati hiyo.

Alisema  kutokana na mfumo mbovu ulio ndani ya shirika hilo sasa, wananchi wengi wameshindwa kutumia nishati ya umeme na kwamba hali hiyo inachangia kutokukua kwa uchumi.

“Huwezi kutegemea kupanda kwa uchumi kama uzalishaji wa umeme ni mdogo kwa kuwa hata uzalishaji viwandani utapungua na wananchi wa kawaida nao hawapati umeme kama inavyotakiwa. Tunataka kuliboresha shirika hili,” alisema Profesa Muhongo.

Atangaza vita
Waziri Muhongo pia ametangaza azma ya kuwafukuza kazi vigogo wa shirika hilo watakaoshindwa kutekeleza agizo la Serikali la kuwaunganishia umeme wateja kwa bei ya punguzo.

“Kuanzia Januari mosi mwakani bei ya kuunganisha umeme inaanza kutumika ya punguzo kutoka 455,108 hadi 177,000 sawa na asilimia 61.11, kinyume na hapo mtakuwa mmejiachisha kazi,” alisema.

Alisema kuwa watakaoshindwa kutekeleza watafukuzwa kazi bila barua ya onyo wala kesi na nafasi zao zitazibwa na vijana wasomi ambao wanazunguka kila kona ya nchi wakitafuta ajira.

“Nasisitiza kwamba asiyeweza kazi awapishe wanaoweza mapema, maana umeme ni uchumi…, kama Mkoa wa Mara unawatu takribani 2 milioni, lakini wanaotumia umeme ni watu 18,911 sawa na asilimia 6 tu,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza:
Katika mkutano huo Profesa Muhongo alishangazwa na kitendo cha wananchi kutoalikwa wakati wao ndiyo wadau wakubwa wa nishati hiyo, badala yake walialikwa viongozi wa vijiji, madiwani na watumishi wa Halmashauri.

No comments:

Translate