tangazo

Sunday, December 30, 2012

KESI YA PEMBE ZA NDOVU UTATA MTUPU KUMBE VIGOGO PIA WAHUSIKA


                                Mkuu wa Jeshi la Polisi Said Mwema  

WAKATI ujangili unaotishia kutoweka kwa baadhi ya wanyama katika hifadhi za taifa nchini ukiendelea kushika kasi, imebainika kuwa baadhi ya mahakimu, polisi na waendesha mashtaka ni wahusika wakuu wa matokeo ya ujangili ambao ni chimbuko la biashara ya nyara za Serikali zikiwamo pembe za ndovu.
Inakadiriwa kuwa tembo wapatao 30 huuawa kila mwezi na mtandao wa ujangili ambao pia unaundwa na wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya nchi, ambao wamekuwa wakifanikisha uhalifu huo kwa msaada wa baadhi ya maofisa na askari wa wanyamapori.
Hapa nchini ujangili umekuwa ukifanywa na makundi ya watu wenye silaha haramu katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba na maeneo mengine ya wazi, huku kukiwa na taarifa kwamba baadhi ya nyara hasa pembe za ndovu huingizwa nchini kutoka nchi jirani ya Msumbiji. Wanunuzi wakuu wanadaiwa kuwapo hapa nchini.
Mkurugenzi wa Tanapa, Allan Kijazi anasema hali ni mbaya kwa kuwa taifa linatumia gharama kubwa kuwalinda na kukabiliana na ujangili, lakini wahalifu wanapokamatwa wamekuwa wakiachiwa kinyemela hata pale ambapo kuna ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.
“Ujangili huu ni mtandao mkubwa sana. Wanatumia silaha za kisasa zaidi kuliko hata za kwetu…hata kibali cha kununua silaha hatupati kwa wakati, hali ambayo inadhoofisha jitihada hizi…hapa tulipofikia ushirikiano wa vyombo vyote ni muhimu,” alisema Kijazi.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa, njia kubwa ya kuingizia pembe hizo zipo katika wilaya za Tunduru, Namtumbo na Mbinga mkoani Ruvuma ambako pikipiki hutumika kuvusha kabla ya kusafirishwa kwa kificho hadi Dar es Salaam ambako hupakiwa kwenda nje ya nchi kuuzwa kupitia bandarini.
Kushamiri kwa vitendo vya ujangili kumesababisha kuwapo jitihada za kuukabili, lakini kama alivyosema Kijazi, imebainika kuwa jitihada hizo zinakwazwa na baadhi ya watumishi katika vyombo vya dola, wakiwamo baadhi ya mahakimu, polisi na waendesha mashtaka.
Uchunguzi wa Mwananchi ulibaini kuwa baadhi ya watuhumiwa ambao wamewahi kunaswa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ujangili, wametoweka katika njia za kutatanisha na kuacha kesi zikiendelea.
Mchezo mahakamani
Uchunguzi umebaini kuwa, baadhi ya mahakimu wa mahakama za wilaya katika mikoa ya Mara, Simiyu, Shinyanga na Kigoma ni sehemu ya mtandao huo, hivyo watuhumiwa wengi wanaokamatwa na nyara, zikiwamo silaha hupewa dhamana na hawarudi mahakamani.
Taarifa za uchunguzi zilizothibitishwa na baadhi ya maofisa wa Tanapa, askari wa wanyamapori na wanasheria wa Serikali zinadai kesi nyingi za nyara licha ya kuwa na uzito, baadhi ya mahakimu walioko chini ya mtandao huo hutoa dhamana kwa masharti nafuu na watuhumiwa huruka dhamana na kuendelea na kazi ya ujangili.
Uchunguzi umebaini mtuhumiwa aliyekamatwa kwa tuhuma za kuwinda faru, nyani na ngiri ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mwaka 2010, Madubu Masunga Dusara (33), mkazi wa Ng’walali, haonekani mahakamani baada ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Shinyanga, Lydia Ilunda kumpa dhamana kwa masharti nafuu.


Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 6 ya mwaka 2010 hakimu alitoa dhamana kwa mtuhumiwa kwa masharti nafuu bila kuzingatia thamani ya wanyama aliokuwa amedaiwa kuua ambayo ni Sh10.304 milioni.
Kwa mujibu wa sheria, ili mtuhumiwa apewe dhamana anapaswa kuwasilisha fedha taslimu kiasi ambacho ni nusu ya thamani ya wanyama anaotuhumiwa kuwaua au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika, lakini katika kesi hiyo wadhamini hawakuwa wakifahamika na baadaye ilitolewa taarifa kwamba mtuhumiwa haonekani mahakamani.
Kadhalika hakimu huyo alitoa dhamana pia kwa Malango Dusara (42) ambaye ni kaka yake na mtuhumiwa wa awali, Madubu ambaye alikamatwa akiwa na risasi 348, lakini pia akiwa chini ya dhamana taarifa zilifikishwa mahakamani kwamba amefariki dunia.
Hata hivyo, Hakimu Ilunda alisema kuwa chanzo cha kuharibika kwa kesi hizo ni waendesha mashtaka kutopeleka ushahidi kwa wakati.
“Watuhumiwa wanakaa mahabusu miaka bila dhamana wakati wana haki ya kudhaminiwa. Waendesha mashtaka kila wakati wanadai ushahidi haujakamilika na sisi tunatekeleza hitaji la sheria kwa kuwa kupata dhamana kwa makosa kama hayo ni haki ya mshtakiwa,” alisema hakimu huyo.
Alisema tatizo kubwa la waendesha mashtaka wa jamhuri wanasababisha kesi nyingi kufutwa ama washtakiwa kuachiwa huru kwa kuwa hawatoi ushahidi. Hata hivyo, licha ya kudaiwa kwamba amekwishafariki dunia, Malango ambaye anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 3 ya 2010 kwa kukutwa na risasi 548, amekamatwa tena na sasa yuko mahabusu.
Wakili wa Serikali
Wakili wa Serikali Mwandamizi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kanda ya Shinyanga, Hashimu Ngole alilithibitishia Mwananchi kwa simu kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
“Alipewa dhamana kwa masharti nafuu na hata sisi hatukushirikishwa, akaruka dhamana …taarifa zikawa zinakuja kuwa amekufa…hilo tulilitegemea maana mwanzoni kabisa tuliitahadharisha mahakama, tukapuuzwa kwa misingi ambayo hatujui…amekamatwa Desemba 14 mwaka huu na sasa yuko mahabusu,” alisema Ngole.
Alisema mdogo wa mtuhumiwa huyo ambaye ana kesi ya kuua faru naye inasemekana yupo hai licha ya mahakama kuarifiwa kwamba alishafariki dunia. Uchunguzi umebaini kwamba kabla ya kudaiwa kwamba wamefariki, tayari mashahidi sita walikuwa wametoa ushahidi wao mahakamani.
Kuhusu kesi zao, Ngole alisema zinaendelea kwa kuwa walijua hawajafa kama ilivyodaiwa kwamba kesi ya mtuhumiwa aliyekamatwa shahidi amebaki mmoja. “Shahidi anatoka Bariadi kuja Shinyanga …amefika mara tatu hakimu hayupo… anarudi kesi ilikuwa Desemba 2 hakimu hakuwapo, imepangwa Desemba 31 mwaka huu sijui kwa tarehe hizo zilizopangwa kama itasikilizwa,”alisema Ngole.
Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa, hata mawakili wa Serikali Mkoa wa Shinyanga ambao walikuwa wakiendesha kesi hizo hawakuulizwa wakati wa watuhumiwa kupewa dhamana na kama sheria ingezingatiwa, Serikali ingekuwa na uwezo wa kukamata mali za wadhamini baada ya watuhumiwa kuruka dhamana.


“Makosa yao ni makubwa ambayo yanazidi thamani ya Sh10 milioni. Sheria inahitaji dhamana yao walipe nusu ya fedha taslimu na wawe na wadhamini wenye mali isiyohamishika, lakini wao walidhaminiwa na watu wasiofahamika bila hata kutushirikisha sisi, matokeo yake hawaonekani na ujangili unazidi,”alisema na kuongeza:
“Tulichotahadharisha mapema ndicho kimetokea, hii ni hatari watu wameua faru bila hata kuangalia thamani ya mnyama wanapewa dhamana kirahisi namna hiyo?” alihoji.
Alikwenda mbali zaidi na kudai mwaka 2010 waliamua kwenda Meatu kuhakikisha kesi za watuhumiwa wa nyara zinashu ghulikiwa na kuisha, lakini kati ya kesi 80 watuhumiwa wote walikuwa nje ya dhamana na hawaonekani mahakamani.
“Waliokuwa wanafika hawafiki 10 tukalazimika kufuatilia na lugha huwa hiyo kuwa wamekufa…kama hakutafanyika mageuzi katika vyombo vyetu vya uamuzi hata operesheni zingefanyika nyingi hakuna mafanikio…Tanapa wanafanya kazi sana tena katika mazingira magumu, wanaleta watu wanaachiwa tutegemee nini,” alisema.
Hukumu nyingine
Ngole alisema hukumu ambazo zimekuwa zikitolewa zinakatisha tamaa, huku akitoa mfano wa kesi namba 3 ya uhujumu uchumi ya mwaka 2010 ya Masanja Maguzu ambaye alikamatwa akiwa na silaha aina ya SMG, risasi 31 na magazine 3.
Alisema Maguzu kabla ya kukamatwa na silaha hizo alikuwa tayari ametumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuua wanyama ndani ya hifadhi.
“Kimsingi baada ya kutumikia kifungo cha miaka mitano alitolewa, lakini baadaye alikamatwa na silaha ya kivita nyumbani, risasi na magazine lakini alifungwa kifungo cha nje.”
Alisema hata wanapoomba kukata rufaa hawapewi nakala za hukumu na mwenendo wa shauri. ”Inachukua mpaka miaka mitatu watu wanamaliza vifungo vyao hujapata nakala hiyo…kwa madai kuwa vitendea kazi ni shida,”alisema.
Alisema baadhi ya watoa uamuzi wanatumia udhaifu wa sheria kutekeleza matakwa yao na kwamba uamuzi huo unazidi kuligharimu taifa, hivyo aliomba sheria zilizopo zirekebishwe iwe kama ilivyo kwa makosa ya ubakaji adhabu zake zinakuwa kali.
Wasajili Mwanza, Tabora
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Isaya Alphan alipoulizwa kuhusu tuhuma za mahakimu hao alisema hakuna taarifa sahihi na kwamba amekuwa akizisikia kwenye vyombo vya habari.

“Hilo la Shinyanga liko Kanda ya Tabora naomba uwatafute hao,… hili la watuhumiwa walioachiwa katika mahakama ya Wilaya ya Serengeti mpaka niangalie kwenye faili… kwa sasa siko ofisini niko likizo mpaka Januari,”alisema Alphan kwa simu.Naye Msajili wa Mahakama Kanda ya Tabora, Thomas Simba aliliambia Mwananchi kwa simu kuwa hajapokea taarifa zozote za malalamiko kuhusu suala hilo.
“Haya masuala ya dhamana ni very complicated (yana mkanganyiko) …sijui kwa hilo la hao wa nyara kupewa dhamana kisha hawaonekani mahakamani…kwa kifupi ni kwamba dhamana ni haki ya mshtakiwa kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 15,”alisema Simba na kuongeza:
“Katika ibara ya (1) kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru, (2) Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kuwa huru na kuishi kwa uhuru, itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa kwa nguvu au kunyang’anywa uhuru wake isipokuwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria.”
Hata hivyo, alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu masharti ya dhamana kwa watu walioua wanyama wenye thamani ya zaidi ya Sh10 milioni Simba alisema:
“Kwa kuwa hilo liko mahakamani sipendi kulisemea nini kilipaswa kufanyika… kama kuna mambo hayaendi vizuri wahusika wanatakiwa kukata rufaa kuja mahakama ya juu kupinga uamuzi huo.”
Hata hivyo, Mwananchi lilibaini kuwa msajili huyo ni mgeni katika kituo hicho cha kazi kwani amekaa kituoni hapo kwa muda usiozidi miezi minane, akitokea Kanda ya Kigoma alikokuwa akifanya kazi.
Itaendelea kesho Jumapili….

No comments:

Translate