tangazo

Wednesday, December 26, 2012

CHADEMA YASEMA KATIBA MPYA SI YA WANANCHI


 Mabere Marando 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai kushtukia mchakato wa Katiba Mpya nchini na kubashiri kuwa Katiba hiyo haitakuwa na tija kwani inalenga kuwalinda na kuwanufaisha watawala badala ya wanachi.
Chadema wamedai kuwa pindi kitakaposhika madaraka, chama hicho kitaamua haraka kuisuka upya Katiba hiyo ili iwape nguvu,mamlaka na masilahi wananchi.
Hayo yalisemwa kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Ruaha wilayani Kilosa na Mwanasheria wa chama hicho, Mabere Marando na kufafanua kuwa vifungu vyote vitakavyoondolewa na kuingizwa kwa mizengwe vitaingizwa baada ya chama hicho kushika madaraka.

“Tupo makini na hili wala msihofu, tunajua wanataka iendelee kuwalinda waliopo madarakani ndio maana wanaogopa kuingiza vipengele vinavyowabana hasa kuendeleza ufisadi na kurithshana madaraka,”alisema Marando.
Marando alisema kwa kuwa yeye ni mjumbe wa kamati kuu wa chama hicho, atahakikisha wananchi wananufaika na matunda ya uhuru kwa kujiandikisha na washiriki kupiga kura maana Chadema imeshinikiza daftari kuanza kurekebishwa upya kuanzia sasa.

“Tunajua kuwa,Katiba hii itachakachuliwa tu, sasa sisi tunawaahidi Watanzania kuwa mtakapotupatia madaraka tutawaandalia katiba inayowapa mamlaka ninyi na kiongozi atabaki kama msimamizi tu,” alisema.

Katika hatua nyingine, Marando ametangaza rasmi kubeba mzigo wa kesi zinazowakabili waliokuwa viongozi wa Serikali ya kijiji cha Ruaha kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao wanaendelea kushikiliwa na polisi katika mahabusu ya Kilosa.

Kwa kuanzia alisema, amewasiliana na polisi mkoa na kuelezwa kuwa wanatambua viongozi hao waliondolewa kufuatia mizengwe ya CCM na viongozi wa wilaya kinyume na sheria na kuwa wamekubaliana na polisi mkoa kupitia Mkuu wa Upelele Mkoa (RCO) kuyaagiza majarada ya kesi zote watuhumiwa wote 13 waliokamatwa kijijini hapo na kutoa uamuzi wenye suluhisho la amani.

Alisema baada ya kupunguza kesi za wabunge wa chama hicho, sasa anahamishisa kambi katika kesi zilizopo mkoani Morogoro ili kuwaondoa shaka walionayo wananchi dhidi ya kesi za kusingiziwa za kisiasa na kuahidi kuzishinda zote na kuliaibisha Jeshi la Polisi na washirika wake.

Hata hivyo, Mwanasheria huyo wa Chadema, aliwataka viongozi wa Serikali wilaya na mkoa kuongoza kwa mujibu wa sheria na kuachana na uongozi wa mazoea kwani sasa Chadema hakitawaachia viongozi wanaoongoza kwa lengo la kuwafurahisha mabwana ambao ni chama tawala.

No comments:

Translate