Farijala Hussein (kushoto) na Rajabu Maranda wakisindikizwa na Askari
Magereza kwenda kupanda gari kurejeshwa gerezani baada ya Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu ya jijini Dar es Salaam, jana, kuwakuta na hatia ya
kesi nyingine ya wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA)
iliyokuwa ikiwakabili. Picha na VenanceNestory
KWA mara ya tatu, Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu
Maranda amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela na kuamriwa kurejesha
Sh616.4 milioni.
Binamu yake, Farijala Hussein ambaye walishtakiwa pamoja alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kuamriwa kurejesha Sh81 milioni na mfanyabiashara Ajay Soman akihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, sawa na Maranda lakini yeye akiamriwa arejeshe Sh400 milioni.
Washtakiwa wengine ambao ni wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Iman Mwakosya, Ester Komu na Sophia Kalika walitiwa hatiani kwa kosa la kuisababishia Serikali hasara na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela ama kulipa fidia ya Sh5 milioni.
Kabla ya kusoma hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya saa 4, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Ilvin Mugeta alisema washtakiwa wote wamepatikana na hatia katika makosa ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kuwasilisha nyaraka za uongo BoT na kuisababishia Serikali hasara ya Sh3.8 bilioni.
Hakimu Mugeta alisema wafanyakazi wa BoT hawatahusika katika mpango wa kurejesha fedha kwa sababu ushahidi unaonyesha hawakunufaika na chochote katika wizi huo.
Alisema Maranda, Farijala na Soman hawa kuna ushahidi ambao unaonyesha kuwa walijinufaisha na fedha hizo hivyo wanatakiwa kuzirejesha na kwamba iwapo watashindwa kutekeleza amri hiyo, mali zao zikamatwe.
Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro awali, aliiambia mahakama kuwa Maranda na Farijala walikwisha tiwa hatiani kwa makosa ya aina hiyo katika kesi namba 1161/2008 na 1163/2008 na kwamba hawana kumbukumbu ya kutenda makosa ya uhalifu kwa washtakiwa Ajay, Iman, Ester na Sophia.
Kimaro alisema kutona na aina ya makosa na fedha za umma aliomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa waharifu wengine wenye tabia kama hiyo.
Pia aliiomba mahakama itumie mamlaka yao yaliyopo katika kifungu cha 348 (1) ama cha 358 (1) cha sharia ya mwenendo wa mashauri ya jinai sura ya 20, kuwaamuru washtakiwa hao kurejesha fedha wanazodaiwa kuiba BoT, kama walivyojipatia.
Magafu akijibu hoja hizo, alidai kuwa Maranda na Farijala wasipewe adhabu kali kwa sababu kesi hizo zilifunguliwa wakati mmoja na kwamba tofauti ilikuwa ni majina ya kampuni na kuwa aliyestahili kupewa onyo kama hilo ni yule aliyefanya uhalifu na akarudia tena.
Maranda na binamu yake Farijala Hussein tayari wanatumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh 1.8 bilioni za Akaunti ya Madeni ya Nje ( Epa) iliyopo BoT na kuamuriwa kurejesha kiasi hicho cha fedha.
Licha ya kutumikia kifungo hicho, pia wanatumikia kifungo kingine cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya tuhuma za kuchota Sh 2.2 bilioni za EPA.
Hukumu hiyo ya tuhuma za wizi wa Sh3.8 bilioni za Epa, ilisomwa na jopo la Mahakimu watatu linaloongozwa na Jaji Samuel Kalua, Jaji Beatrice Mutungi na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Ilvin Mugeta.
Katika kesi hiyo, washtakiwa hao, kwa pamoja wanadaiwa kuwa, kati ya Januari 18 na Novemba 3, 2005, kinyume na kifungu namba 384 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 ya sheria, walikula njama ya wizi wa fedha kutoka BoT.
Pia wanadaiwa kughushi hati ya usajili yenye namba 46218 na kuonyesha kuwa zimesainiwa na kutolewa na Msajili wa Biashara kwa Kampuni ya Mibale Farm wakati si kweli.
Wanaendelea kudaiwa kujipatia Sh3.8 bilioni baada ya kudanganya kuwa kampuni yao ya Mibale Farm imepewa deni na kampuni ya Textile Mills Ltd ya nchini India.
Chanzo na mwananchi habari
No comments:
Post a Comment