Na: Raymond Kaminyoge,Mwananchi.
FAMILIA ya aliyekuwa mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi anayedaiwa kuuawa na polisi akiwa kazini, inakusudia kuishtaki serikali na Idara ya Polisi kwa kusababisha mauaji hayo.
Mwangosi aliuawa Septemba 2, mwaka huu wakati akikusanya habari za ufunguzi wa tawi la Chadema Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi.
Kusudio la kuishtaki serikali limekuja huku askari anayedaiwa kumuua Mwangosi, Pacificius Cleophase Simon akiwa amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa, kesi inaendelea.
Akizungumza kwa simu jana, mke wa Mwangosi, Itika alisema familia hiyo imeamua kuchukua uamuzi huo baada ya kuona viongozi wa serikali hawajali.
Itika alisema hadi sasa familia hiyo inajiuliza maswali ya kilichosababisha polisi watumie nguvu kubwa kumuua mume wake na kwamba, wanadhani wanao wajibu wa kuishtaki serikali na polisi.
“ Ukiangalia picha ile unaona kwamba Mwangosi kabla ya kuuawa alikuwa amezungukwa na askari saba, ni kwanini aliuawa kama jambazi, bado wingu zito limetanda katika familia na tunadhani haki itapatikana mahakamani,” alisema Itika.
Alisema wako katika mazungumzo na wanasheria watakaowasaidia katika kesi hiyo na kwamba, wakikamilisha wananchi watajulishwa.
Ripoti ya kamati iliyoundwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuchunguza kifo hicho, ilisema Mwangosi aliuawa kwa makusudi na polisi chini ya usimamizi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
No comments:
Post a Comment