Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro,Leonidas Gama, amevalia njuga suala la wanaofanya magendo mpakani
POLISI wamefanikiwa kumtia mbaroni mfanyabiashara wa bidhaa za
magendo anayedaiwa kumgonga kwa makusudi na gari, mwandishi wa Tanzania
Daima, Mkoa Kilimanjaro, Charles Ndagulla.
Kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo, kumekuja siku moja tu baada ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Leonidas Gama kuwaagiza polisi kuhakikisha wanamsaka na kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo.
Mbali na kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo, polisi pia wamefanikiwa kulikamata gari aina ya Toyota RAV4J linalodaiwa kutumika katika tukio hilo usiku wa Novemba 4 katika eneo la Holili.
Mfanyabiashara huyo ambaye ni mashuhuri katika Miji ya Moshi na Himo, alikamatwa juzi jioni katika Mji wa Himo na kusafirishwa hadi Moshi yalipo makao makuu ya polisi Kilimanjaro.
Gama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kilimanjaro, jana alilithibitishia gazeti hili juu ya polisi kumwarifu kuwa wamemtia mbaroni mfanyabiashara huyo.
“RPC (kamanda wa polisi) ameshanitaarifu rasmi juu ya kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo pamoja na gari lililohusika na wanaendelea kumhoji kuhusu ushiriki wake katika tukio hilo”alisema.
Tayari Ndagulla jana aliitwa Makao Makuu ya Polisi Kilimanjaro na kulitambua gari hilo kuwa ndilo lililomgonga kwa makusudi wakati huo likiwa na watu wawili mmoja akiwa ni mwanamke.
“Wapelelezi wameniita na kunionyesha hilo gari na nimelitambua kwa rangi yake, aina na nambari zake za usajili na tayari nimeshaandikisha maelezo ya nyongeza ya kulitambua gari hilo”alisema.
Tukio la kugongwa kwa makusudi kwa Ndagulla lilitokea Novemba 4 usiku wakati mwandishi huyo na mwandishi wa habari hizi walipokwenda eneo hilo kuchunguza biashara ya magendo ya sukari.
Taarifa za raia wema walizowatumia waandishi wa habari siku hiyo, zilisema malori 12 yaliyosheheni sukari yalikuwa yavuke mpaka na hadi wanafika, tayari malori sita yalikuwa yameshavuka mpaka.
Waandishi walifanikiwa kuyazuia malori mawili yakiwa na shehena ya sukari na ndipo wakati wakisubiri msaada wa polisi ndipo Toyota RAV4 ilipofika ikiwa na watu wawili ndani yake.
Watu hao wanaoaminika ndio walikuwa wamiliki wa shehena hilo, waliamuru magari yale yaondolewe kwa nguvu kwenda Kenya na hapo hapo kumfuata Ndagulla na kumgonga na kutokomea Kenya.
Wakati mfanyabiashara huyo akikamatwa, taarifa zilisema jana asubuhi malori mawili yalifanikiwa kuvuka mpaka na kwenda Kenya saa 12:30 asubuhi kupitia barabara ya Holili na Lower Rombo.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya polisi na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanashiriki katika mtandao wa uvushaji magendo kwa kupewa rushwa kwa kila gari linalovuka.
Habari zinadai kuwa kabla ya lori kuvuka, wafanyabiashara hao hununua njia (Line) kwa polisi na maofisa hao wa TRA kwa kati ya Sh300,000 na Sh800,000 kulingana na ukubwa wa gari.
chanzo na mwananchi habari
No comments:
Post a Comment