VIONGOZI wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar,
wamefikishwa
tena mahakamani na kubadilishiwa shtaka la uvunjifu wa amani chini ya
kifungu cha 3 (d) cha sheria za Usalama wa Taifa.
Washtakiwa
hao ni pamoja na kiongozi wa jumuiya hiyo, Sheikh Farid Hadi Ahmed (41),
Mselem Ali Mselem (52), Mussa Juma Issa (37) na Azzan Khalid Hamdani
(48).
Wengine ni Suleiman Juma Suleiman (66), Khamis Ali Suleiman (59), Hassan Bakari Suleiman (39) na Ghalib Ahmada Omar (39).
Kwa
pamoja watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya uvunjifu wa amani,
ushawishi wa kuchochea na kurubuni watu, kula njama pamoja na kufanya
kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani kosa ambalo linamkabili
Azzan Khalid Hamdani pekee yake.
Watuhumiwa hao waliofikishwa
mahakamani hapo jana chini ya ulinzi mkali wa polisi walisomewa mashtaka
ya uvunjifu wa amani chini ya kifungu cha 3 (d) cha sheria za Usalama
wa Taifa sura ya 47 sheria ya mwaka 2002, kwa kuhusishwa na matukio
yaliyotokea Oktoba 17 na 18 mwaka huu.
Upande wa mashtaka kutoka
ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, ukiongozwa na Ramadhan Nasseeb
ulidai kuwa watuhumiwa kwa pamoja wanadaiwa kuharibu barabara, majengo,
vyombo vya moto ikiwemo na pikipiki na magari na wakufanya hivyo bila
ya kuwepo sababu za msingi za kuharibu na kuteketeza kinyume cha maslahi
ya umma na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi milioni tano.
Katika
shtaka la pili washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Mei 26 hadi Oktoba 19,
2010 walishawishi na kufanya uchochezi kwa kufanya mikutano katika
maeneo tofauti yakiwemo Lumumba, Msumbiji, Fuoni Meli sita na Mbuyuni
ambayo kwa nyakati tofauti walishawisi na kuchochea watu kufanya makosa.
Alidai
kuwa makosa washtakiwa waliweka vizuizi barabarani kwa kutumia mawe,,
makontena ya kuhifadhia taka, matawi ya miti, mapipa ya mafuta, kuchoma
magurudumu ya magari, kuharibu majengo tofauti, magari na kusababisha
huduma muhimu za jamii za Serikali kusimamisha na watu kushindwa kufanya
shughuli zake.
Pia watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kula
njama na kusababisha Sheikh Farid Hadi Ahmed kujificha katika sehemu
isiyojukana na kupelekea uvunjifu wa amani katika jamii kwa siku kadhaa.
Shtaka
la nne ambalo linamkabili Sheikh Azzan Khalid peke yake ni kufanya
kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani, pamoja na kumtolea maneno
ya kashfa na matusi Kamshna wa Polisi wa Zanzibar.
Hata hivo, watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.
Mawakili walalamika wateja wao kunyolewa ndevu
Katika
hatua nyingine, Mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao wamelalamikia
kitendo cha Serikali kukiuka haki za binaadamu na utaratibu mzima wa
kisheria wa uendeshaji wa mashtaka dhidi ya wateja wao.
Watuhumiwa hao wanatetewa na Mawakili wa Abdallah Juma, Suleiman Salum pamoja na Salim Tawfik.
Tawfik
alidai mahakamani hapo kuwa wateja wao tangu wakamatwe siku 17
zilizopita wamekuwa hawatendewi haki ikiwa pamoja na kunyimwa fursa zote
wanazostahiki kupata kama watuhumiwa.
Wakili huyo alitoa mfano
wa uvunjwaji wa haki hizo kuwa ni pamoja na wateja wao kushindwa
kubadili nguo ambapo tangu walipokamatwa hawajaruhusiwa kubadilisha,
kulazimishwa kunyolewa ndevu, kukatazwa kuonana na jamaa zao, pamoja na
kutengwa kila mmoja katika chumba maalumu chini ya ulinzi mkali.
Mambo
mengine ambayo yalalamikiwa ni kulazwa chini ya sakafu, kujisaidia
ndani ya ndoo, kunyimwa fursa ya kufanya ibada jambo ambalo linakwenda
kinyume na Katiba kuhusu haki ya kuabudu na kufungiwa ndani ya vyumba
saa 24.
Wakinukuu baadhi ya vifungu vya Katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1988, inayotoa fursa ya watu wote kuwa sawa mbele ya sheria, haki
ya kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria, Mawakili hao wamedai
kuwa wateja wao wamekuwa wakikosa haki hizo na kutendewa tafauti na
watuhumiwa wengine waliopo rumande.
"Haki za washtakiwa hawa
zinavunjwa wazi wazi na maofisa wa Vyuo vya Mafunzo na serikali kwa
ujumla, hawa raia kama wengine wanapaswa kupatiwa haki zao zote za
msingi wanazostahiki kwani hapo ni watuhumiwa lakini wanafanywa kama
wameshatiwa hatiani Mheshimiwa."
Wakili Tawfik aliiomba mahakama
pamoja na Serikali kuacha kuvunja sheria na haki za watuhumiwa hao kwa
sababu ni miongoni mwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu na mahakama
haipaswi kunyamazia ukiukwaji huo unaotendeka dhidi ya watuhumiwa.
"Mheshimiwa
wateja wetu hawana fursa ya kusali sala ya Ijumaa na wenzao, hawana
vitabu vya dini wakati tunafahamu hawa ni viongozi wa dini, hata ndevu
wamenyolewa ili kuwadhalilisha na wamefanyiwa kwa makusudi ili
kuwavunjia heshima zao katika jamii wakati ni kinyume na katiba kwani
kama tunavyofahamu kufuga ndevu kwa muislamu ni sunna na ni ibada lakini
kumnyoa ndevu ni sawa na mkristo kumvua msalaba."
Akijibu
malalamiko hayo upande wa mashtaka walionekana kutorishika na tuhuma
hizo za kukiuka haki za watuhumiwa na kutaka upande wa utetezi wa
watuhumiwa kufungua kesi ya madai kupinga hayo kwa sababu kesi dhidi ya
watuhumiwa ni kesi ya jinai.
“Sisi kama ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP), hatupendelei kuona haki haitendeki pamoja na ukiukwaji
wa haki za binaadamu unaodaiwa hapa sisi ni wajibu wetu kuhakikisha
vyombo vya sheria vinavyohusika vinatekeleza sheria na kufuata katiba
lakini pamoja na hilo naomba mahakama malalamiko haya yanayotolewa na
upande wa utetezi kuwasilisha hoja zao hizi katika mahakama husika kwa
vile hoja zao hizo zimegusia ukiukwaji wa Katiba na hii ni kosa ya jinai
sasa wamefungue kosa ya madai.”
Hata hivyo jopo la wanasheria wa
Serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), wakiongozwa na
Rashid Fadhil lilidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika
hivyo kuiomba mahakama kuhairisha shauri hilo na kulipangia tarehe
nyengine kwa ajili ya kutajwa ili iweze kupatikana muda wa ziada wa
kuendelea na upelelezi huo.
Hakimu George Kazi baada ya
kusikiliza hoja za pande zote mbili alisema kuwa atatoa uamuzi wa
malalamiko hayo Novemba 20 siku ambayo imepangwa kutajwa kesi hiyo.
No comments:
Post a Comment