tangazo
Thursday, November 22, 2012
Askofu Mokiwa awashambulia watengenezaji wa ARVs
Akizungumza katika uzinduzi wa semina ya kupambana na unyanyapaa kwa wagonjwa wa Ukimwi kwa viongozi wa Jumuiya ya Kikiristu Tanzania (CCT), iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam, Askofu Mokiwa, alihoji sababu za viwanda hivyo kushindwa kutengeneza dawa za kutibu kabisa ugonjwa huo na badala yake vinatengeneza dawa za kupunguza makali.
Alisema viwanda hivyo vinachelewesha kutoa tiba ya ugonjwa huo kwa makusudi, ili kuendelea kuuza dawa hizo kwa bei ya juu kwa mataifa mbalimbali.
Dk Mokiwa alisema kuendelea kwa viwanda hivyo kuchelewesha tiba ya ugonjwa huo, ni sawa na kufanya mauaji ya makusudi.
“Haiwezekani viwanda hivyo viendelee kutengeneza dawa ya kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi, halafu vishindwe kutengeneza dawa ya kutibu, hiyo ni njia ya kutafuta fedha,” alisema kiongozi huyo wa kidini.
Alisema watafiti wa Kikristo kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali, wanapaswa kuongeza kasi ya kutafuta tiba hiyo, ili kuepuka dhambi ya mauaji ya makusudi.
“Ukimwi umegeuzwa chanzo cha watu kujitafutia fedha, kila siku tunaona watu wanaanzisha miradi na kampeni zinazogharimu fedha nyingi kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huu huku wakisahau kutafuta tiba ya kuutokomeza,”alisema Askofu Dk Mokiwa.
Pia alisema kuna haja ya kutunga sheria itakayowalinda wagonjwa wa Ukimwi dhidi ya vitendo vya kuwanyanyapaa, ili itoe hukumu stahiki.
Dk Mokiwa alisema kitendo cha kuwanyanyapaa wagonjwa hao na kuwaita kuwa ni marehemu watarajiwa ni kosa la jinai linalohitaji sheria kali kulidhibiti.
Mkuu huyo wa kanisa pia alitaka sheria ya kuwaba waajiri wanaowanyanyapaa wagonjwa hao, ili wawape kipaumbele kwa kuwa na wao wana haki ya kufanya kazi.
Aliwaomba Watanzania washirikiane katika kupambana na unyanyapaa dhidi ya wagonjwa wa Ukimwi kwani kufanya hivyo ni kutengeneza ugonjwa wa akili, hofu na ni dhambi ambayo haimpendezi Mwenyezi Mungu.
Semina hiyo imewahusisha wachungaji 33 wanaoandaa vipindi vya redio na televisheni kutoka madhehebu mbalimbali ya Kikristu.
Chanzo Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment