Rais Jakaya Kikwete
----
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne,
Novemba 2012, amelitumia Kanisa Katoliki Tanzania salamu za rambirambi
kuomboleza kifo cha Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Mhashamu Baba
Askofu Aloysius Balina aliyefariki dunia majira ya saa tano asubuhi
kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza.
Katika salamu zake za
rambirambi kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania Mshahamu Baba Askofu
Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea
kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Mhashamu Baba Askofu Aloysius
Balina ambaye nimeambiwa ameaga dunia asubuhi ya leo kwenye Hospitali ya
Rufaa ya Buganda, Mwanza, kwa ugonjwa wa kansa.”
Amesema Rais Kikwete katika salamu zake hizo: “Mhashamu
Baba Askofu Balina alikuwa kiongozi hodari na mwadilifu ambaye siyo tu
alichangia kipekee katika mwenendo mzuri wa kiroho wa waumini wa Kanisa
Katoliki bali pia katika maendeleo ya Watanzania wote kwa jumla.”
“Kifo chake
kimetuondolea kiongozi mwema ambaye tutazikosa busara zake na uongozi
wake. Lakini napenda kukuhakishia Mshahamu Baba Askofu kuwa sisi ndani
ya Serikali tutaendelea kutambua na kuthamini mchango wa Askofu Balina
alioutoa kwa nchi yetu katika maisha yake,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Baba
Askofu, nakuomba upokee salamu za rambirambi za Serikali ninayoiongoza
na zangu binafsi kufuatia msiba huu mkubwa. Aidha, kupitia kwako,
naomba uwafikishie salamu zangu viongozi na waumini wote wa Kanisa
Katoliki kwa kuondokewa na kiongozi na muumini mwenzao. Naungana nanyi
kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweka pema peponi roho ya Marehemu. Amen.”
No comments:
Post a Comment