Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad
BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar, imeagizwa kuacha mara moja upendeleo wa kutoa mikopo kwa watoto wa vigogo kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad alitoa agizo hilo jana alipozungumza na uongozi na watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar Mnazi Mmoja mjini hapa.
Seif alisema yapo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na wazazi, kwamba Bodi hiyo inatoa mikopo kwa watu ambao hawana sifa, wakiwamo watoto wa vigogo.
“Yapo malalamiko mengi ya wananchi na wazazi kuhusu Bodi hii, ikiwamo kutoa mikopo kwa njia ya upendeleo kwa watu ambao hawana sifa na watoto wa wakubwa,” alisema.
Alikumbusha watendaji wa Bodi hiyo, kwamba taasisi hiyo imeanzishwa kusaidia maendeleo ya watoto masikini wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za masomo.
“Hayo ndiyo malengo ya kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, kutoa mikopo kwa watoto wa masikini wasiokuwa na uwezo wa kugharimia masomo,” alisisitiza.
Alisema wakifanikiwa kutekeleza malengo hayo kwa kiasi kikubwa, Bodi itatoa mikopo kwa wanafunzi wengi na kuepusha urasimu na kutiwa shinikizo kutoka kwa wakubwa.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Iddi Khamis alisema Bodi imezidiwa na maombi na mahitaji ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaohitaji mikopo hiyo wakiwamo wenye sifa.
Akifafanua, Iddi alisema kwa sasa vipo vyuo vya elimu ya juu vinne vikiwa na wanafunzi wenye mahitaji ya mikopo kwa ajili ya kujiendeleza zaidi, lakini Bodi haina uwezo huo.
“Tumezidiwa na idadi ya wanafunzi wanaohitaji mikopo ya elimu ya juu sasa…vipo vyuo vikuu vinne vyenye wanafunzi wanaohitaji mikopo,” alisema.
Hata hivyo, Khamis alisema kwa bajeti ya mwaka 2012/13, Bodi imeongezwa bajeti ya fedha kutoka Sh bilioni 4 hadi Sh bilioni 8 ingawa bado hazitoshi.
Alifafanua, kuwa maombi ya mikopo kwa wanafunzi yameongezeka kutoka 800 hadi 1,800 na Bodi imeshindwa kuwapa mikopo wanafunzi hao wa ziada hivi sasa.
Hata hivyo, wanafunzi wanaokosa mikopo kutoka Bodi hiyo bado wana nafasi ya kuomba kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment