tangazo
Thursday, November 22, 2012
WANAJESHI WATATU WAHUKUMIWA KUNYONGWA.
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa askari watatu baada ya kupatikana na hatia ya kumuua, Swetu Fundikira.
Adhabu hiyo ilitolewa jana na Jaji Zainabu Muruke baada ya kuwatia hatiani wanajeshi hao kwa kosa la kumuua kwa makusudi Fundikira, kinyume cha kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu.
MT 1900 Sajenti Roda Robert (42) na MT 85067 Koplo Mohamed Rashid wote wa JKT Mbweni na MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa Kikosi cha JWTZ Kunduchi, walimpiga Fundikira, Januari 23 mwaka huu saa 7:30 usiku wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na baadaye kufariki dunia usiku huohuo wa kuamkia Januari 24, mwaka 2010, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Hukumu hiyo ilifufua upya msiba wa Swetu, baada ya ndugu zake kuangua vilio, huku chumba cha Mahakama kikigeuka kwa muda kuwa sehemu ya msiba.
Sambamba na vilio hivyo, ndugu wawili wa marehemu Swetu walianguka chini na kuzirai kwa muda, kabla ya kupewa huduma ya kwanza na kurejea katika hali ya kawaida.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Muruke alisema ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa washtakiwa hao ndiyo waliomuua Fundikira, ushahidi uliotolewa na upande wa Mashtaka (Jamhuri) ulikuwa ni ushahidi wa mazingira, kwamba Jamhuri imeweza kuthibitisha mashtaka hayo.
Alisema kuwa anakubaliana na mtiririko wa ushahidi wa upande wa mashtaka kama ulivyoelezwa na mashahidi wake sita akiwemo daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu pamoja na askari polisi wawili ambao washtakiwa katika utetezi wao walishindwa kuuvunja.
“Sheria iko wazi ukiondoka na mtu au ukionekana naye kwa mara ya mwisho na baadaye mtu huyo akapatikana na madhara, wewe ndiyo unawajibika kutoa maelezo ya kina kuhusu yaliyompata mtu huyo,” alisema Jaji Muruke na kuongeza;
“Kisheria ukitoa maelezo ambayo hayajakidhi haja na yana utata ni faida kwa upande wa mashtaka ambao hutegemea ushahidi wa mazingira. Maelezo ya kina hayajatolewa na washtakiwa wote.”
Aliendelea, “Ushahidi wa Jamhuri japokuwa ni wa mazingira, umejengwa thabiti na upande wa utetezi haukuweza kujenga matundu, ama kuuvunja mnyororo huo, kidole kinawaelekea wao.”
Jaji Muruke alisisitiza kuwa katika kesi hiyo licha ya kuwa kuna ushahidi wa kimazingira, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha mashaka.
“Hivyo kosa wanaloshtakiwa nalo limethibitishwa na Mahakama imewaona washtakiwa kuwa wana hatia ya kumuua Swetu Abdallah Fundikira,” alisema Jaji Muruke, huku akimuuliza wakili wa Serikali kama washtakiwa wana kumbukumbu zozote za makosa ya jinai.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi aliyejitambulisha kwa jina moja la Kongola alijibu kuwa hakuna kumbukumbu za makosa ya jinai kwa washtakiwa hao.
Kabla ya kutoa adhabu hiyo Jaji Muruke alimpa nafasi wakili wa washtakiwa hao, Karoli Muluge na washtakiwa wenyewe kusema lolote.
Wakili Muluge aliiomba Mahakama iwape adhabu ambayo ni nafuu kutokana na mazingira ya kesi hiyo, kwamba umri wa washtakiwa ni mdogo, bado ni vijana ambao ni nguvukazi ya Taifa na wanategemewa na familia zao.
Mshtakiwa wa kwanza, Sajenti Robert aliiomba Mahakama impunguzie adhabu akidai kuwa mama yake ni mjane na anamtegemea na hakuna mtu mwingine wa kumsaidia, ana watoto wadogo na pia afya yake siyo nzuri.
Hata hivyo, Jaji Muruke alilazimika kumuamuru mshtakiwa wa pili, Koplo Ngumbe kukaa chini baada kuanza kujitetea kuwa japo ametiwa hatiani, hakuhusika na mauaji hayo.
Kwa upande wake, mshtakiwa wa tatu Koplo Rashid aliiomba mahakama imwonee huruma na impunguzie adhabu akidai kuwa yeye bado ni mdogo na kwamba hilo ni kosa lake la kwanza.
Baadaye Jaji Muruke alisema kuwa ni kweli maombi ya mshtakiwa wa kwanza yanatia huruma na kwamba mshtakiwa wa tatu hata kumbukumbu zinaonesha kuwa bado ni mdogo na kwamba hilo ni kosa lake la kwanza, lakini pia kuna roho iliyopotea.
“Kama ilivyo ada, ni adhabu moja tu kwa mtu anayepatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia na hakuna mbadala.” alisema Jaji Muruke na kuongeza;
“Hivyo mahakama hii inatamka kuwa mshtakiwa wa kwanza, mshtakiwa wa pili na mshtakiwa wa tatu mmepewa adhabu ya kifo, mtanyongwa hadi kufa.”
Baada ya kutamka adhabu hiyo Jaji Muruke alitoka katika chumba cha mahakama na ghafla ndugu wa marehemu Fundikira walilipuka kwa vilio ndani ya Ukumbi wa Mahakama, kama vile walikuwa msibani.
Ndugu wawili wa marehemu, Mwasiti Fundikira ambaye ni dada wa marehemu na Shelina Hamisi (mpwa wa marehemu) walianguka chini na kuzirai kwa muda hali iliyowalazimu watu waliokuwa nao karibu kuwapatia huduma ya kwanza hadi walipoanza kurejea katika hali zao za kawaida.
Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Lucy ambaye marehemu alimwacha akiwa na mimba, alisema kuwa alilia kwa sababu hakuamini kama haki ingetendeka.
Dada wa marehemu, Rehema Fundikira alisema kuwa alikuwa akilia kwa uchungu kutokana na jinsi ndugu yao alivyouawa kinyama.
Wakili Muluge alisema hakuridhika na hukumu hiyo na kwamba atakata rufaa.
Alisema hakuna shahidi hata mmoja aliyewaona wakimuua na kwamba hata hayo majeraha yaliyodaiwa kuwa ndiyo chanzo cha kifo cha Fundikira hakuna aliyeeleza jinsi washtakiwa hao walivyoyasababisha, kama ni kwa kumpiga au kwa namna nyingine yoyote.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment